Na Faustine Kapama-Mahakama, Arusha
Majaji Wakuu kutoka Umoja
wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika wanaoendelea na Mkutano wa Mwaka
jijini hapa leo tarehe 24 Octoba, 2023 wametembelea mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa
na wadau mbalimbali wa Mahakakama ya Tanzania kujionea shughuli wanazofanya
katika muktadha mzima wa utoaji haki.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwaongoza Majaji hao na wageni wengine kutembelea mabanda hayo pembezoni mwa Mkutano huo na wameonyesha kuvutiwa na maendeleo ya kisasa ya teknolojia na miundombinu yanayotukati katika shughuli za kimahakama.
Mabanda hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Uhamiaji, Shirika la Maendeleo la Taifa, Shirika la Ndege la Taifa, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na wengine.
Wakiwa katika mabanda
hayo, Majaji Wakuu hao walichukua muda mrefu katika banda la Mahakama ya Tanzania
baada ya kuvutiwa na mambo kadhaa yanayofanywa katika kutoa haki kwa wananchi.
Akizungumza akiwa katika
banda hilo, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, ambaye pia
ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amesema Majaji Wakuu wote wamewatembele
na kujionea mambo makubwa yanayofanyika, hivyo kuelekeza wataalam wao kuja
Tanzania kujifunza zaidi.
“Kuna nchi ambazo zimesema
hazitatuma watu wao, zinataka wataalam wetu waende kule. Miaka yote Tanzania imekuwa
kiongozi wa Nchi za Afrika katika masuala mbalimbali. Sisi tumekuwa Makao Makuu
ya ukombozi wa Bara la Afrika.
“Hivyo, tukiwa Makao
Makuu ya ukombozi kwa masuala ya utoaji haki, bado tunaona tunatekeleza wajibu
wetu na sisi tumewaambia tupo tayari muda wowote ule, tutakwenda kuwashirikisha
wenzetu,” amesema.
Ametaja baadhi ya maeneo
ambayo Majaji hao wamefurahishwa walipotembelea banda la Mahakama, ikiwemo
matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyofanywa
na Mahakama ya Tanzania katika utoaji haki.
Mhe. Dkt. Rumisha ameeleza
kuwa nchi zingine zilikuwa na mifumo ambayo wameinunua, hali ambayo ni tofauti
kwa Tanzania. Amesema mifumo yote katika Mahakama ya Tanzania imejengwa na wataalam
wa ndani, yaani watumishi wa Mahakama.
Amebainisha faida nyingi
za kufanya hivyo, ikiwemo uwezo wa kuongeza au kupunguza kitu chochote kwenye
mfumo bila kutafuta mtu mwingine, tofauti na nchi zingine ambazo zimenunua
mifumo iliyotengenezwa ulaya ambayo hairuhusu kufanya chochote.
Faida nyingine ni kwamba Mahakama
ya Tanzania hailipii chochote kwa mwaka kwa kuwa mfumo umetengenezwa na
wataalam wa ndani, tofauti na nchi nyingine ambazo hutoa gharama za uendeshaji.
Jaji Rumisha ametaja
jambo jingine lililopelekea mafanikio hayo kama matumizi bora ya rasimimali na
katika jambo hilo Majaji Wakuu hao walitaka kujua fedha zilizotumika kufanya
yote hayo ilitoka wapi na makisio yao yalikuwa ni mabillioni ya fedha.
Aliwaeleza kuwa fedha
iliyotumika haifiki hata robo ya kile walichokuwa wanafikiria kwa sababu mambo
yote yaliyofanyika yametumia fedha ambazo hazizidi Dola za Kimarekani millioni
60, ambazo ni sawa na dola millioni tisa kwa mwaka kwa kugawanya muda
uliotumika.
“Nimewapa mfano wa ujenzi
wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita katika Mikoa ya Dar es Salaama, Mwanza,
Arusha, Dodoma na Morogoro ambapo tulibakisha shillingi billioni 3.6 za
Kitanzania baada ya kukamilisha ujenzi huo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Menejimenti ya Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha
amesema kuwa Majaji hao wamepata kufahamu mambo makubwa yanayofanywa mahakamani
na wamevutiwa na mambo kadhaa, ikiwemo dhana hiyo ya uwepo wa Vituo Jumuishi
vya Utoaji Haki.
“Wamevutiwa namna gani
ambapo unaweza kuwakusanya wadau wote wa haki katika jengo moja na kuwepo na ngazi
zote za Mahakama. Hili ni jambo ambalo wamelipenda sana na wametamani kwenda
kwenye majengo yetu hayo kujionea,” amesema.
Mhe. Kamugisha ametaja suala
lingine ambalo Majaji Wakuu hao wamevutiwa ni maendeleo ya kusogeza huduma za
Mahakama karibu na wananchi, hususani matumizi ya Mahakama zinazaotembea.
Amesema wamewaeleza namna Mahakama hizo zinavyofanya kazi na mpango wa kuongeza
Mahakama zingine sita ambazo zitaanza kufanya kazi kufikia Januari mwakani.
“Wamevutiwa kuona kwamba
huduma hizi zinawalenga wananchi ambao hawana uwezo wa kusafiri muda mrefu, wanawake
wajane na wale ambao wamedhurumiwa haki zao na wafanyabiashara wadogo, kwamba
tunawafuata katika maeneo yao ya biashara,” amesema.
Matumizi ya TEHAMA pia ni
eneo ambalo limeleta mvuto na wageni wengi wakataka kuendelea kukaa katika
banda la Mahakama, japo muda ulikuwa umeisha. Mhe. Kamugisha amewaelezea mifumo
ya kitehama, mpango wa menejimenti ya mashauri na mfumo mpya unaokuja ambao utaanza
kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi ujao wa Novemba.
“Wamevutiwa sana kuona
namna gani Mahakama inaweza kufahamu kile kinachoendelea nchi nzima ndani ya
muda huo huo, kwa maana hata Jaji Mkuu akiwa ofisini anaweza kuona kitu gani
Jaji au Hakimu mmoja mmoja anafanya na hali ya mashauri katika Mahakama zote kwa
wakati mmoja,” amesema.
Kiupekee, Mkurugenzi huyo
aliwaelezea Majaji Wakuu teknolojia mpya inayokuja ya kunukuu na kutafsiri
mienendo ya kimahakama na wamevutiwa namna itakavyosaidia kuwaondolea Majaji na
Mahakimu jukuku la kuandika mwenendo kwa mkono na kutafsiri mwenendo au hukumu
kwa njia za kawaida.
“Kama tulivyoeleza jana, tumesikiliza
mashauri mengi katika kipindi cha Uviko-19, hivyo wakataka kujua namna gani
tuliweza kufanya hivyo, tumewaonyesha teknolojia yetu na mfumo wa kusikiliza
mashauri kwa njia ya mtadao, hivyo wakavutiwa namna gani mtu anaweza kuwa yupo
nyumbani na Jaji yupo ofisini, lakini shauri likasikilizwa, hili nalo limeleta
mvuto mkubwa,” amesema.
Majaji Wakuu hao
wanaoshiriki kwenye Mkutano huo wanatoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Namibia, Zimbabwe, Eswatini, Msumbiji,
Seychelles, Botswana, Angola, Zanzibar, Malawi, Lesotho, Mauritius, Zambia na
Afrika ya Kusini.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo kwenye picha) kwenye banda la Mahakama ya Tanzania baada ya Majaji Wakuu kutoka Umoja wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika kutembelea banda hilo pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Viongozi hao jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni