Jumanne, 24 Oktoba 2023

AKILI BANDIA YAANZA KUTUMIKA MAHAKAMANI

Na Faustine Kapama-Mahakama, Arusha

Mahakama ya Tanzania imeshaanza kutumia Akili Bandia kuendesha na kuratibu mashauri katika Mahakama mbalimbali hapa nchini, hatua itakayochochea uharakishaji wa utoaji wa haki kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasilisnao (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock alipokuwa anawasilisha mada kwenye Mkutano wa Majaji Wakuu kutoka Nchi za Kusini na Mashariki ya Afrika unaoendelea jijini hapa.

Bw. Kalege amewaambia Majaji hao na Viongozi wengine wanaohudhuria Mkutano huo kuwa tayari kuna Mahakama 11 ambazo zimewekewa viwezeshi vya kutumia Akili Bandia katika kunukuu na kutafsiri mienendo ya mashauri. Huo mfumo wa kunakiri na kutafsiri unatumia Akili Bandia na tayari umeshaanza

Kwa hatua za majaribio umeshaanza katika Mahakaka Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Kutuo Jumuishi cha Masula ya Familia Temeke. Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni na sasa usimikaji wa miundombinu hiyo wezeshi unaendelea katika Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki Arusha, Mwanza, Morogoro, Dodoma, Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Akiwasilisha mada kuhusu Akili bandia katika utoaji wa haki, mfumo na huduma za kunukuu na kutafsiri za kielektoniki katika Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa ikiangalia namna ilivyopiga hatua kuanzia ilipoanza kuweka jitihada za makusudi za utekelezaji wa mpango ya uwekaji wa TEHAMA mpaka hapo ilipofikia.

“Baada ya kupitia hiyo safari tukaangalia maeneo gani ambayo Mahakama imeanza kutumia Akili Bandia na tukabaini kwenye mfumo wake mpya wa usajili, uendeshaji na usimamizi wa mashauri na pamoja na mambo mengine, mfumo huu unatumia Akili Bandia kwenye upangaji wa mashauri,” amesema.

Mkurugenzi huyo amewaambia Majaji Wakuu hao kuwa utaratibu huo unapunguza dalili au upendeleo kutoka kwa Jaji au Hakimu mmoja kuwa anapangiwa aina fulani ya mashauri au kunakuwa na uwajibishaji au ubadilishwaji wa mpango wa mashauri.

Amesema mfumo wa sasa unakuwa unamtaka msimamizi wa kituo kutoa sababu kwa nini ahamishe shauri hili kutoka kwa Hakimu huyu kwenda kwa hakimu yule na unasaidia kuthibiti upendeleaji wa aina fulani ya mashauri kusikilizwa na huyu na mengine yanasikilizwa na yule.

“Lakini pia kwenye utoaji na uchakataji wa taarifa mbalimbali au data kwa kutumia ‘business intelligence’ unaweza ukatoa ‘insights’ kwa ajili ya kusaidia taasisi kufanya maamuzi ya kimkakati,” Bw. Kalege amewaambia washiriki wa Mkutano huo.

Sambamba na hilo, amesema kuwa matumizi ya Akili Bandia yamewekwa kwenye mfumo wa kunakili na kutafsiri mwenendo wa mashauri na pia kuzalisha taaarifa wakati huo huo kila baada ya shauri kumalizika kusikilizwa.

Wajumbe wa Mkutano walipata nafasi ya kuuliza maswali, likiwemo utaratibu inayotumia Mahakama ya Tanzania kuhakikisha wananchi waliopo pembezoni ya nchi wanapata nafasi ya kuzifikia huduma za TEHAMA.

Bw, Kalage amewaeleza wajumbe kuwa Mahakama ilishafanya tafiti pamoja na takwimu zilizopo na kujua wananchi walio wengi wanasimu za kiganjani, hivyo ikatengeneza progamu inayoitwa ‘Mobile App’ inayowawezesha wananchi kufuatilia na kujua mwenendo na hatua za mashauri yao yamefikia wapi.

“Kwa hiyo, pragramu hii inawasaidia wananchi waliopo maeneo ya pembezoni kupata nafasi ya kupata huduma kwenye Mahakama ya kidijitali,” amesema.

Akili bandia ni uwezo wa komputa kufanya kazi kama binadamu. Komputa inakuwa na uwezo wa kujifunza na kuakisi anayoyafanya binadamu na kufikiri na kutoa maamuzi kama binadamu.

Lakini, Akili Bandia inaongeza ufanisi, kwa maana ya muda wa kufanya maamuzi na uharaka wa kufanya hayo maamuzi. Hii ni mbinu ambayo inachukuliwa na inaongezwa kwenye mfumo.

Majaji Wakuu wanaoshiriki kwenye Mkutano huo wanatoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Namibia, Zimbabwe, Eswatini, Msumbiji, Seychelles, Botswana, Angola, Zanzibar, Malawi, Lesotho, Mauritius, Zambia na Afrika ya Kusini.

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasilisnao (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enockakiwasilisha mada kwenye Mkutano wa Majaji Wakuu kutoka Nchi za Kusini na Mashariki ya Afrika unaoendelea jijini hapa.


Sehemu ya Majaji Wakuu kutoka Nchi za Kusini na Mashariki ya Afrika (juu na chini) wanaoshiriki mkutano unaoendelea jijini hapa.


Sehemu nyingine ya Majaji na Viongozi wa Mahakama (juu na chini) wanaoshiriki mkutano huo.

Sehemu nyingine ya tatu ya Majaji na Viongozi wa Mahakama (juu na chini) wanaoshiriki mkutano huo.

(Picha na Lyidia Churi na Jeremia Lubango-Mahakama).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni