· Yapeleka Majaji, wageni 150 Ngorongoro
·Nao waahidi kurudi Tanzania kujionea vivutio zaidi
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Arusha
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe Prof Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 25 Octoba, 2023 amewaongoza Majaji Wakuu
kutoka Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro
mkoani Arusha.
Hatua hiyo ni mwitikio wa
ombi la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
alipokuwa anafungua Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu kutoka nchi hizo katika
Hoteli ya Mount Meru jijini hapa hivi karibuni.
Safari kuelelea katika Hifadhi
hiyo ilianza mapema asubuhi saa 12.00 katika Hoteli hiyo na msafara wa Majaji
hao ulipokelewa na Viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi katika lango kuu la kuingilia
hifadhini.
Wakiwa katika Hifadhi
hiyo, Majaji Wakuu kutoka nchi hizo, Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na
Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na wageni wengine mbalimbali wamejionea utajiri
wa wanyama pori na misitu ya kupendeza.
Watalii hao wamefanikiwa
kuwaona baadhi ya wanyama maarufu duniani wanaofahamika kama Big-5
wanaopatikana kwa urahisi katika Hifadhi hiyo kama Tembo, Simba, Nyati na Faru.
Chui, ambaye ni miongoni mwa Wanyama hao maarufu hakuweza kuonekana. Kwa
kawaida, Twiga hapatikani katika hifadhi hiyo kutokana na umbo lake.
Kadhalika, Majaji
Wakuu hao pamoja na wageni wengine wamefanikiwa kuwaona wanyama wengine kama
swala, pundamilia, mbuni, nyani, fisi, Kiboko na ndege wa aina mablimbali
wakiwemo Filamingo.
Viongozi hao wameonesha
kufurahishwa na utalii huo na wamefarijika kujionea kwa macho wanyama
wanaowaona kwa picha kwenye vitabu na runinga. Wameahidi kuja tena Tanzania kwa
ajili ya kufanya shughuli za utalii.
Akizungumza kwenye lango
kuu la kuingilia na kutokea kwenye Hifadhi hiyo baada ya Viongozi hao kufanya
utalii, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Watendaji Wakuu wa Mahakama kutoka nchi hizo, Prof Elisante Ole Gabriel
amewaambia Waandishi wa Habari kuwa wageni takribani 150 wametembelea kivutio
hicho cha Ngorongoro ambacho kipo umbali wa mita 610 kutoka juu hadi chini na wameona
wanyama wengi, wamefurahi na wengi wameonesha nia ya kutaka tena kuja kwa mara
nyingine.
“Leo wageni hawa kutoka
nchi 16 wameona Tembo, Simba, Nyati na Faru na wengine wengi na baadhi yao
wamesema walikuwa hawajawahi kuwaona. Hii tunaifanya Tanzania iheshimike na
watu wanaona nchi yetu ni ya kipekee kwa sababu ya heshima hii,” Prof. Ole
Gabriel amesema.
Amesema kuwa kila Taasisi,
ikiwemo Mahakama inawajibu wa kuona jinsi gani ya kutangaza vivutio vyetu vya
kitalii, ni utajiri na dhamana ambayo Tanzania Mungu ameiipa, hivyo ni vyema kuthamini
hali hiyo.
Amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kufungua
Mkutano huo cha Majaji Wakuu ambao wameonesha kukuguswa na kitendo hicho, wamefarijika
na wameona wametendewa heshima ya hali ya juu.
“Sisi kama Watendaji
Wakuu wa Mahakama tumejifunza mengi na wenzangu wameahidi kwamba katika ngazi
ya familia nao watafanya jitihada za kuja kutembelea vivutio vyetu,” amesema.
Majaji Wakuu wanaoshiriki
kwenye Mkutano huo wanatoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Namibia, Zimbabwe, Eswatini, Msumbiji,
Seychelles, Botswana, Angola, Zanzibar, Malawi, Lesotho, Mauritius, Zambia na
Afrika ya Kusini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni