Alhamisi, 26 Oktoba 2023

JMAT TAWI LA SINGIDA YAPONGEZWA KWA KAZI NZURI

Na Eva Leshange, Mahakama-Singida

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe. Alisile Mwankejela amewapongeza Viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) Tawi la Singida kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha Mahakimu wanakutana mara kwa mara ili kubadilisha uzoefu na kutatua changamoto mbalimbali za kikazi.

Akifungua kikao cha Chama hicho kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe.Allu Nzowa kilichofanyika Wilaya ya Iramba, Mhe. Alisile alisema vikao hivyo vimekuwa vikifanyika mara kwa mara.

“Niwapongeze Viongozi wa JMAT kwa kazi nzuri mnayofanya kuhakikisha Mahakimu wanakutana na kubadilishana uzoefu, vikao hivi ni muhimu kwani vinaleta Mahakimu kwa pamoja na kujadiliana masuala ya kazi,” alisema Mhe. Mwankejela.

Kikao hicho ni muendelezo wa vikao ambavyo wamekuwa wakifanya mara kwa mara katika kujengeana uwezo na kujadili masuala mbalimbali wanayokutana nayo Mahakimu Vituoni kutatua changamoto, kupeana uzoefu na mbinu mbalimbali za stadi za maisha.

Kadhalika, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Singida, Bw. Yusuph Kasuka naye aliupongeza Uongozi wa JMAT kwa umoja na ushirikiano ambao wamekuwa wakiuonesha na Ofisi yake.

Aidha katika kikao hicho, Bw. Kasuka alipata fursa ya kuwaeleza mabadiliko ya Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri Mahakamani (Advance e-Case Management) na kuwajulisha baadhi ya Mahakimu ambao hawana komputa mpakato suala lao linashughulikiwa na watazipata muda mfupi ujao.

Kikao hicho kilikuwa na watoa mada wawili mmoja kutoka TAKUKURU Iramba, Bw Michael Ngomo ambaye aliwasilisha mada juu ya makosa ya rushwa na adhabu zake na mtoa mada mwingine alikuwa Daktari kutoka Hospitali ya Wilaya Iramba, Dkt. Adamu Mashenene ambaye alitoa mada juu ya magonjwa yasiyo ambukiza, ulaji wa mlo kamili na  kufanya mazoezi.

Akihitimisha kikao hicho Mhe. Mwankejela alisisitiza Mahakimu kuufanyia mazoezi ya kutosha Mfumo mpya wa kusajili na kusiliza kesi mahakamani ili kubaini changamoto na kuziwasilisha, kuchapa kazi kwa kuhakikisha hakuna mlundikano wa mashauri mahakamani na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe. Alisile  Mwankejela aliyesimama) akifungua kikao cha Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mkoa wa Singida, Mhe. Allu Nzowa. Aliyeketi mbele kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Singida, Mhe. Fadhili Luvinga.

Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka (aliyesimama) akizungumza na Mahakimu hawapo katika picha.

Afisa kutoka TAKUKURU Wilaya ya Iramba, Bw. Michel Ngomo akiwasilisha mada ya Makosa ya rushwa na adhabu zake katika kikao hicho.

Daktari kutoka Hospitali ya Wilaya Iramba, Dkt.Adam Mashenene (aliyesimama) akitoa mada kuhusu elimu ya masuala ya afya katika kikao hicho.

 Sehemu ya Mahakimu wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakijiri katika kikao hicho.

Sehemu ya Mahakimu wakifuatilia kikao hicho, aliyeketi  wa kwanza (kushoto) ni Hakimu Mahakama ya Mwanzo Shelui, Mhe. Archad Byabajuka akifuatiwa na Hakimu Mkuu Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe.Joyce Shilla na aliyeketi katikati ni Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Kintinku-Manyoni, Mhe. Faraja Kombe.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni