Alhamisi, 12 Oktoba 2023

WANANCHI KIGOMA WAKUMBUSHWA KUTII WITO WA MAHAKAMA

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina amewasihi wananchi mkoani humo kutii wito wa Mahakama (Summon) kwa kufika ili kuisaidia Mahakama kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Mhe. Kagina aliyasema hayo jana tarehe 11 Oktoba, 2023 alipokuwa akitoa elimu kuhusu ‘Taratibu za Wito wa Mahakama’ kwa wananchi waliofika mahakamani hapo kupata huduma mbalimbali. 

“Mahakama ya Tanzania katika ngazi zote hutoa wito (summons)  kumtaka mlengwa wa jambo fulani kufika mahakamani kujibu au kuisaidia Mahakama kuhusu jambo fulani lililopo mbele ya Mahakama husika, hivyo nawasihi ukipata wito fika Mahakama husika ili kujua nini umeitiwa na Mahakama hiyo,” alisema Mhe. Kagina.

Alisema endapo mtu ukiukaidi wito huo unaweza kukufanya kuingia hatiani kwa kosa la kudharau wito huo kwa Kifungu cha Sheria Na. 114 ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2019, ambacho kinampa mamlaka Jaji au Hakimu wa Mahakama kutoa onyo au adhabu ya kifungo cha miezi isiyopungua 12 Jela. 

Mhe. Kagina alibainisha kuwa, wito wa Mahakama umekuwa ukidharaulika kwa wahusika bila kujua madhara yake, hivyo amewataka kutofanya hivyo kwani inaweza kuleta madhara makubwa kwa mlengwa.

Aliongeza kuwa, endapo mhusika akijificha ili kuepuka kusaini wito wa Mahakama ili mkono wa sheria usimfikie, wito (summons) huo huchapishwa kwenye gazeti linalosomwa na watu wengi na mara tangazo linapotoka katika gazeti Mahakama inaamini ya kwamba wito huo umemfikia mlengwa bila kuzingatia kama amesoma gazeti hilo au la na hivyo, kumtaka mlengwa wa jambo fulani kufika mahakamani kujibu au kuisaidia Mahakama kuhusu jambo husika lililopo mbele yake. 

Kwa upande wake Wakili wa Kujitegemea mkoani humo, Bw. Michael Mwangati alisema Wito (summons) kwao Mawakili ni muhimu maana bila wito hawawezi kuendelea  na shauri mahakamani kwakuwa shauri ni la pande mbili hivyo, ni lazima upande unaodaiwa upelekewe wito wa Mahakama ili kufika mahakamani na kujibu madai yanayowakabili mbele ya Mahakama hiyo.

Mmoja kati ya wananchi waliofaidika na elimu hiyo, Bw. Obadia Boniface, ameipongeza Kanda hiyo kwa kuweka muda wa kuwaelimisha kwani elimu aliyopata pamoja na wenzake ni kubwa na muhimu kwa watanzania wote kwani watu wengine wanaogopa wito wa Mahakama, hivyo amewatoa wasiwasi wananchi wengine kutii wito na kukiri kwamba, kushitakiwa ni mahakamani ni bora kuliko mahali pengine kwakuwa Mahakama inatoa haki. 

 Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Leonard Kagina, akitoa elimu kwa wananchi (hawapo katika picha) waliofika Mahakama Kuu kupata huduma mbalimbali jana tarehe 11 Oktoba, 2023.


Baadhi ya wananchi waliofika Mahakama Kuu Kigoma kupata huduma mbalimbali wakimsikiliza Mhe. Kagina (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa mada kuhusu Wito wa Mahakama 'Summons'.

Mwananchi aliyeonyesha kufurahishwa na mada hiyo, Bw. Obadia Boniface, akifuatilia kwa makini ufafanuzi wa mtoa mada juu ya Wito wa Mahakama (Summons).


Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina (kulia) pamoja na Wakili wa Kujitegemea, Bw. Michael Mwangati wakishirikiana  kuwafafanulia wananchi (hawapo katika picha) juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Wito wa Mahakama 'Summons'. 

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni