Alhamisi, 12 Oktoba 2023

WATUMISHI MAHAKAMA SINGIDA WANOLEWA MFUMO MPYA WA KURATIBU MASHAURI MAHAKAMANI

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo amewataka watumishi wa Mahakama mkoani Singida kujifunza kwa ufasaha na kuyaelewa vema mafunzo juu ya Mfumo mpya wa Kieletroniki wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri mahakamani (Advanced Case Management System). 

Akifungua Mafunzo hayo jana tarehe 11 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Dkt. Masabo aliwashukuru Viongozi wa Kanda yake na wa mkoani hapo kwa kuwezesha mafunzo na hivyo kuwataka watumishi kuyaelewa na kutokuwa sehemu ya kukwamisha utekelezaji wa maboresho ya Mfumo huo. 

“Ndugu watumishi mafunzo haya ni muhimu kwenu kuyaelewa tofauti na hapo tutakwamisha utekelezaji wake, ikitokea tumekwama iwe ni nje ya uwezo wetu na sio suala la mtumishi kukwamisha,” alisema Mhe. Dkt. Masabo.

Mwezeshaji wa Mafunzo hayo ambaye ni Afisa Tehama, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bi. Amina Ahmad aliwaeleza watumishi hao kuwa, Mfumo huu ni mzuri zaidi na wenye maboresho ukilinganisha na ule wa awali, kwakuwa umerahisisha kazi kwa kila mmoja.

Bi. Amina alibainisha kuwa, Mfumo huo utaanza kutumika rasmi tarehe 01 Novemba, 2023 na hivyo kuwasihi watumishi kuwa tayari kujifunza na kuutumia.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu kutoka Wilaya za Iramba na Manyoni.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyesimama mbele) akitoa neno la ufunguzi alipokuwa akifungua Mafunzo kuhusu Mfumo mpya wa Kieletroniki wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri mahakamani (Advanced Case Management System) jana tarehe 11 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida. Aliyeketi mbele (kulia) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya  Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa na aliyeketi mbele kushoto ni Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka. 

Afisa Tehama kutoka Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bi. Amina Ahmad (aliyesimama mbele) akiwasilisha mada kuhusu Mfumo mpya wa Kieletroniki wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri mahakamani (Advanced Case Management System) kwa Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Singida wakimsikiliza mtoa mada (aliyesimama mbele).

Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mafunzo hayo kwa umakini.
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni