·Mahakama Sports yashangaza wengi
·Hujuma, mbeleko zatawala mpira wa miguu
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Ikulu inayoundwa
na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Netiboli Tanzania leo tarehe 11 Octoba, 2023
imenusurika kichapo baada ya kukabwa koo na Timu ya Mahakama ya Tanzania
(Mahakama Sports) katika mchezo wa nusu fainali kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya
Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa.
Mchezo uliofanyika kwenye
viwanja vya Chuo Kikuu cha Kikristo Ruaha kuanzia majira ya saa 10:00 jioni ulikuwa
wa vuta ni kuvute huku Mahakama Sports ikitoa upinzani mkali kiasi cha
kuwafanya Ikulu kutoamini kilichokuwa inatokea.
Mahakama Sports
inayoundwa na vijana wadogo wadogo ambao hawana uzoefu mkubwa walionyesha
mchezo mzuri uliowainua mashabiki mara kwa mara na kuwafanya Ikulu kufanya mabadiliko
mara tatu.
Hadi mchezo unamalizika,
Ikulu ikafanikiwa kutinga katika hatua ya nusu fainali kwa mbinde baada ya kutumbukiza
vikapu 77 kwa 8 walivyopatya Mahakama Sports. Kwa matokeo hayo, Mahakama Sports
itajitupa kesho tarehe 12 Octoba, 2023 kuwania katika nafasi ya tat una Hazina.
Wakati huo huo, hujuma za
wazi zimetawala kwenye mchezo wa mpira wa miguu uliochezwa kwenye uwanja wa
Samora saa 10:00 jioni, kuwakutanisha Mahakama Sports na Hazina, ambao
wameibuka na ushindi kwa faida ya mwamuzi.
‘Man of the match’ kwenye
mtanange huo alikuwa mwamuzi na dalili za upendeleo zilianza kuonekana mapema
baada ya kuwazawadia Hazina tuta katika mazingira ya kutatanisha, dakika chache
baada ya kuanza mchezo huo.
Hazina ambao ni vibonde
na hawakuwa na lolote la maana zaidi ya kubebwa na mwamuzi walitumia nafasi
hiyo na kufanikiwa kupata bao ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo.
Mahakama Sports
walionesha kandanda safi na kupata nafasi nyingi, lakini walikumbana na mchezo
mbaya kwa kukanyagwa na kupigwa viwiko mara kwa mara na wachezaji wa Hazina, huku mwamuzi akiwa hachukui
hatua yoyote.
Kadhalika, Mahakama Sports
ilipata matuta ya wazi matatu katika kipindi cha kwanza na dakika za mwisho mwisho za mtanange huo, lakini
mwamuzi akang’ata filimbi, jambo lililowashangaza wanamichezo waliofurika
katika uwanja kushuhudia kabumbu hilo.
Kufuatia matokeo hayo,
Mahakama Sports itamenyana na ndugu zao, Wizara ya Katiba na Sheria kesho
tarehe 12 Octoba, 2023, ili kumtafuta mshindi wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni