Jumatano, 11 Oktoba 2023

ELIMU HUDUMA BORA KWA MTEJA YAWAFIKIA WANANCHI MOROGORO

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

Kufuatia kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma Bora kwa mteja katika Mahakama ya Tanzania, watumishi na wateja wa mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki wamepatiwa elimu ya namna ya kupata huduma kupitia kituo hicho.

Elimu hiyo ilitolewa na wataalamu toka ndani ya kituo hicho, Mahakimu Wakazi Waandamizi, Mhe. Lilian Silayo na Mhe. Adelf Sachore, ambao walitoa elimu na kuzungumza na wateja wa Mahakama kwa siku mbili kuanzia jana terehe 10 Oktoba, 2023.

Akitoa elimu hiyo, Mhe. Sachore alisema kuwa kituo chao ni sehemu ya mpango mkakati wa maboresho ya Mahakama na Mahakama hukitumia kujitathmini na kufanya maboresho kutokana na maoni yanayotolewa na wadau wa Mahakama.

“Naomba niwatoe wasiwasi, kuna usiri mkubwa baina ya mteja na mtu anayempatia huduma, hivyo msisite kuwasiliana na huduma yetu kwa kuhofia kuwa tutavujisha siri,” alisema na kubainisha kuwa kituo kitampatia mteja majibu kwa ufasaha mara baada ya suala lake kushughulikiwa.

Naye Mhe. Silayo akigusia namna mteja anavyoweza kuwasiliana na huduma ya kituo hicho kwa kutimia simu, tovuti na ujumbe wa WhatsApp. Alitaja mawasiliano hayo kama namba ya simu 0752 500 400 na tovuti maoni@judiciary.go.tz.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Agustina Mmbando aliwasihi wateja hao kutokaa na malalamiko bali walitumie dawati lililoko ndani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ili yatapatiwe ufumbuzi.

Tangu kuanzishwa kwa kituo cha huduma kwa mteja mnamo tarehe 1 Machi, 2022, kimeweza kupokea maoni na malalamiko 2,751 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba, 2023. Kati ya hayo, 2,740 yametatuliwa na 11 yaliyobaki yanaendelea kufanyiwa kazi.


 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Agustina Mmbando (wa kwanza kushoto), Mhe. Liliani Silayo (wa pili) na Mhe. Adelf Sachore wakitoa elimu ya huduma bora kwa mteja katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.

Mhe. Adelf Sachore kutoka Kituo cha Huduma Bora kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania akizungumza na wateja ndani ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro wakati akitoa elimu juu ya huduma kwa mteja.

Mhe. Lilian Silayo kutoka Kituo cha Huduma Bora kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania akizungumza na wateja ndani ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro wakati akitoa elimu juu ya huduma kwa mteja.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Agustina Mmbando akizungumza na wateja wakati wa zoezi hilo la utoaji elimu.

Wateja wakifuatilia elimu ikiendelea kutolewa (juu na chini).

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)

 

 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni