Na James Kapele, Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la (PAMS Foundation) wanaendesha mafunzo ya siku tano kwa Wadau wa Haki Jinai nchini juu ya namna bora ya kusimamia na kuendesha mashauri ya wanyamapori mkoani Katavi.
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 13 Novemba, 2023 yamewakutanisha pamoja Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kutoka katika Mikoa mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Katavi, Mgeni rasmi ambaye alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru, alikipongeza Chuo hicho kwa kuona umuhimu wa kufanya mafunzo hayo kwa wadau wa haki jinai huku akisisitiza juu ya ushirikishwaji na uwajibikaji wa wadau wote katika uhifadhi wa maliasili za nchi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kwa Dunia ya sasa lazima tukubali kuzilinda rasilimali zetu hasa tukizingatia kwamba hata wahalifu wanatumia mbinu mpya katika kutekeleza uhalifu wao na wakati mwingine ujangili unafanyika ndani ya mipaka yetu na nje ya mipaka pia (cross borders). Kwa mantiki hiyo lazima niwapongeze sana Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuona umuhimu wa kufanyika kwa mafunzo haya hasa kwa wadau hawa ambao ndiyo wahusika wakuu wa kusimamia na kuendesha mashauri haya ya wanyapori,” alisema Mhe. Ndunguru.
Akitoa neno la ukaribisho, Hakimu Mkazi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama katika Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda aliwaeleza washiriki kwamba mafunzo hayo ni muhimu kwao kwa kuwa tafiti zimefanyika na kubaini kuwa kuna mapungufu mbalimbali ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi ili kuwa na uelewa wa pamoja katika uendeshaji na usimamaizi wa mashauri ya wanyamapori.
“Baada ya kufanyika kwa utafiti yapo mapungufu na changamoto zilizobainika katika usimamizi na uendeshaji wa mashauri haya ya wanyapori kwa wadau wote wakiwemo watoa maamuzi, Waendesha Mashtaka na Wadau wengine katika kusimamia na kuendesha mashauri haya, alisisitiza Dkt. Kisinda.
Mafunzo hayo yanatolewa ikiwa ni moja kati ya majukumu muhimu yanayofanywa na Chuo hicho kwa wadau wake kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wadau wa Tasnia ya Sheria kwa lengo la kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni