Jumapili, 26 Novemba 2023

JAJI RAIS MAHAKAMA KUU ZIMBABWE AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA SIKU TATU

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube leo tarehe 26 Novemba, 2023 amewasili nchini kwa ziara ya kikazi siku tatu kuitembelea Mahakama ya Tanzania kwa malengo mbalimbali, ikiwemo kujifunza shughuli za utoaji haki kwa wananchi. 

Kiongozi huyo amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere majira ya saa 2.30 usiku na kupokelewa na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Salma Maghimbi.

Viongozi wengine wa Mahakama waliokuwepo kumlaki kiongozi huyo kutoka nchini Zimbabwe ni Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Mhe. Benazetha Maziku na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Philibert Matotay.

Mhe. Dube ameambatana na Viongozi wengine akiwemo Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana, Msajili wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Kudzai Maronga, Mkuu wa Fedha wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Milton Shadaya na Mkuu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Obey Mayenga.

 

Katika siku yake ya kwanza, Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe atakutana na mwenyeji wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na kufanya naye mazungumzo mafupi katika ofisi yake katika jengo la Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

 

Taarifa iliyotolewa na Mahakama kuhusu ziara hiyo inaonesha baada ya mazungumzo hayo, ujumbe wa Mahakama Zimbabwe utatembelea Kituo cha Uendeshaji wa Mitandao kwenye jengo hilo la Mahakama kabla ya kuelekea katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

 

Akiwa katika Kituo hicho, Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe na ujumbe wake utapata taarifa ya maboresho na kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa maboresho ya Mahakama nchini Tanzania na kupata ufahamu kuhusu safari ya Mahakama kidijitali.

 

Katika siku ya pili, Kiongozi huyo wa Mahakama Zimbabwe atakuwa pia katika Kituo hicho Temeke kupata ufahamu wa masuala mbalimbali ya Mahakama na uunganishaji wa mtandao kwa ngazi zote za Mahakama.

 

Baadaye mchana, Mhe Dube atamtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake katika jengo la Mahakama ya Rufani na kufanya naye mazungumzo mafupi na kujadiliana naye masuala mbalimbali ya kimahakama.

 

Jaji Kiongozi wa Zimbabwe na ujumbe wake ataitumia siku ya tatu ya ziara yake kufafanya mambo mengine ya kimahakama kabla ya kuhitimisha na kuondoka nchini siku inayofuata ya tarehe 30 Novemba, 2023.

 

Mhe. Dube siyo kiongozi wa kwanza wa Mahakama kutoka nchi mbalimbali duniani kuitembelea Mahakama ya Tanzania. Viongozi wengine ambao wameshaitembelea Mahakama ya Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni ni Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo ambaye aliwasili nchini tarehe 24 Mei 2022 kwa ziara ya siku tatu.

 

Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt.Flavian Zeija ambaye aliwasili nchini ltarehe 15 Agosti, 2023 kwa ziara ya siku tano na Naibu Jaji Mkuu na Makamu wa Rais wa Mahakama ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Yang Linping ambaye tarehe 1 Novemba, 2023.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Salma Maghimbi (kulia) akimwongoza mgeni wake, Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (katikati) mara baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu. Kushoto ni Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus 

Kahyoza.

Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Salma Maghimbi (kushoto juu na chini) akibadilishana mawazo na mgeni wake, Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube katika chumba cha wageni maarufu kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza (kulia) akizungumza na Msajili wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Kudzai Maronga.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Salma Maghimbi (katikati) akifurahia jambo na wageni wake. Kulia ni Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube na kushoto ni  Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana.
Viongozi wa Mahakama Zimbabwe ambao ni sehemu ya jumbe wa ziara ya Jaji Rais Dube. Kushoto ni Mkuu wa Fedha wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Milton Shadaya na kulia ni Mkuu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Obey Mayenga.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni