Jumatano, 29 Novemba 2023

KITUO CHA USULUHISHI MAHAKAMA YA TANZANIA MAMBO SAFI

·Jaji Rais Mahakama Kuu Zimbabwe avutiwa namna kinavyofanya kazi

·Ataka kujua mafanikio kutumia Wasuluhishi binafsi

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Jaji Mhe. Mary Dube leo tarehe 29 Novemba, 2023 ametembelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi kama sehemu ya ziara yake ya kujifunza na kuvutiwa jinsi kinavyofanya kazi.

Mhe. Dube alifika Kituoni hapo majira ya saa 9.15 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi, Mhe Zahra Maruma. Baada ya kusaini Kitabu cha Wageni, alipokea taarifa fupi kuhusu kuanzishwa kwa Kituo hicho.

Jaji Maruma alimweleza Jaji Rais na ujumbe wake kuwa Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2015 na hadi sasa kimefanikiwa kupatanisha migogoro mingi ya madai.

Alieleza kuwa kuanzia mwaka 2015, walianza usuluhishi wa mashauri katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam na baadaye masuala ya ardhi baada ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kutaka nayo yasuluhishwe ili kuepuka mlundikano.

"Tunatazamia hapo mbeleni kusuluhisha pia mashauri kutoka Divisheni ya Biashara ya Mahakama Kuu, lakini tunajitahidi kuona jinsi gani sheria itakavyowezesha utaratibu huu wa kisheria kufanyika," Jaji Mfawidhi alisema.

Baada ya taarifa hiyo, Mhe. Dube alipelekwa kwenye moja ya vyumba vinavyotumika kwa usuluhishi na kupata wasilisho linaloonyesha jinsi Kituo cha Usuluhishi kinavyofanya kazi. Jaji Mfawidhi alitoa wasilisho la kina, ambalo limekidhi matarajio ya wajumbe hao.

Akizungumza baada ya uwasilishaji huo, Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe alimweleza mwenyeji wake kuwa wao hawana mfumo wa usuluhishi kama ule wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Tuna utaratibu wa kufanya mikutano ya awali kwenye mashauri ambao umeingizwa kwenye kanuni zetu, hii inahusisha Jaji kukaa na wahusika ili kuwasaidia kutatua mgogoro. Ikiwa Jaji anaweza kusuluhisha suala hilo, basi wahusika watakuja na makubaliano yao wenyewe ya namna ya kufanya,” alisema.

Mhe. Dube alidokeza kuwa ni Majaji pekee wanaohusika katika mfumo wa usuluhishi kabla ya shauri kusikilizwa na unahusisha masuala ya madai pekee na siyo kwenye jinai wala masuala ya ardhi.

“Kiwango cha usuluhishaji kwa sasa kimekuwa kizuri, lakini hatuwashirikishi Wasuluhishi binafsi, labda haya ndiyo mabadiliko tunayoangalia, tungetaka kusikia kiwango cha mafanikio ni kipi, ambapo usuluhishi unahusisha Majaji tofauti na pale unapomshirikisha mtu wa tatu katika kujaribu kufanya usuluhishi.

"Vinginevyo, tuna mfumo mbadala wa utatuzi wa migogoro ambao unahusisha Majaji, labda tungeangalia Wasuluhishi binafsi na kuona inakuwaje kama tukisikia kutoka kwenu ni mafanikio gani ya kuwashirikisha badala ya Majaji pekee," alisema.

Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe aliwasili nchini Novemba 26, 2023 kwa ziara ya siku tatu katika Mahakama ya Tanzania.

Ameambatana na maafisa wengine, akiwemo Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana, Msajili wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Kudzai Maronga, Mkuu wa Fedha wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Milton Shadaya na Mkuu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Obey Mayenga.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi, Mhe Zahra Maruma akimpokea mgeni wake, Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube baada ya kuwasili kwa ajili ya kutembelea kituo hicho.


Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (katikati) akisindikizwa Kituoni hapo na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi, Mhe. Zahra Maruma (kushoto). Kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Kitengo cha Mboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu, Mhe. Zahra Maruma (kulia) akimkabidhi zawadi mgeni wake, Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube.

Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube akiwasalimia baadhi ya wafanyakazi wa Kituo cha Usuluhishi.


Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Kituo cha Usuluhishi. Picha ya chini ,Mhe. Dube anapokea taarifa ufupi kuhusu Kituo cha Usuluhishi kinavyofanya kazi.



Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (kulia) akiwa katika picha na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi, Mhe Zahra Maruma. Picha ya chini, Jaji Rais akiwa na Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.


Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu, Mhe. Zahra Maruma (juu) akisisitiza jambo wakati akieleza kwa wageni wake (picha chini) namna Kituo kinavyofanya kazi.


Wajumbe kutoka Mahakama Zimbabwe (juu) na Maafisa waandamizi wa Mahakama ya Tanzania (chini) wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu, Mhe. Zahra Maruma (hayupo pichani).















 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni