Alhamisi, 2 Novemba 2023

MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA YAFUNGUA VILABU VYA UTOAJI ELIMU SHULE ZA SEKONDARI

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma imefungua Vilabu (clubs) mbili za utoaji elimu katika Shule za Sekondari (Secondary School Clubs) za Mlole na Kigoma ‘Grands’ ikiwa ni hatua ya kutekeleza Mpango Mkakati wa utoaji elimu shuleni kuhusu taratibu mbalimbali za Mahakama pamoja na huduma zitolewazo.

Zoezi la kufungua Vilabu hizo lilifanyika jana tarehe 01 Novemba, 2023 na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Utoaji elimu kwa umma, Mhe. Victor Kagina pamoja na Afisa utumishi wa Kanda hiyo, Bw. Festo Sanga.

Akizungumza wakati akiwafundisha Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole, Mhe. Kagina alisema kuwa, Mahakama ya Tanzania imechukua hatua ya kufungua klabu hizi katika shule mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuandaa jamiii na watumishi wa baadae katika Serikali yetu na Taasisi mbalimbali ikiwemo Mahakama na hivyo kuwa na uelewa wa jumla.

“Mahakama inadhamiria kuwalea nyie katika maadili tukishirikiana na wazazi, pamoja na walimu ili kuhakikisha mtakapofikia elimu ya juu mpende kusomea hii  tasnia ya Sheria ili mkawe watumishi bora katika Taasisi za Sheria na kusaidia jamii zetu na Taifa letu la Tanzania katika utoaji wa haki,” alisema Mhe. Kagina.

Kwa upande wake Bw. Sanga, aliwasihi wanafunzi hao kuzingatia elimu maana ndio ufunguo halali wa Maisha na kuongeza kuwa, juhudi zao ndio zitakazofikisha katika hatua ya kuitwa Hakimu au Jaji wa Mahakama.

 “Hao Waheshimiwa Majaji au Mahakimu mnaowaona wote walikuwa kama ninyi wakati wanasoma shule za sekondari, na wakachagua kusomea Sheria na hatimaye wakafikia hatua ya kuwa Hakimu au Jaji wa Mahakama, hivyo nawasihi kuzingatia masomo ili kufikia malengo yenu,” alisema Bw.Sanga.

Aidha, aliwataka wanafunzi hao kuzingatia na kuhudhuria elimu hiyo ya Mahakama/Sheria itakayokuwa ikitolewa kila mwisho wa mwezi ambapo mada na watoa mada watabadilika kutokana na ratiba iliyowekwa na Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Philipo Gabriel aliwashukuru Viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kuchagua shule yao kuwa sehemu ya wanufaika na elimu ya huduma zitolewazo na Mahakama.

“Tunaishukuru Mahakama Kanda ya Kigoma kwa kuichagua shule yetu kuwa miongoni mwa wanufaika wa elimu ya Mahakama itakayokuwa ikitolewa kwa wanafunzi wetu kwa kipindi chote mlichopanga tunatarajia makubwa kwenu na sisi tutawapa ushirikiano mkubwa kuhakikisha tunajenga Taifa lenye uelewa juu ya masuala ya sheria na taratibu za Mahakama katika upatikanaji wa haki kwa wakati,” alisema Mwalimu Gabriel.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina (aliyeketi kulia) pamoja na Afisa Utumishi  Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Mlole, Bw. Kandidus Kamaze (katikati) na sehemu ya Wanafunzi wanaosoma katika Shule hiyo.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina akifurahia jambo na wanafunzi wakati akifundisha kuhusu  ya huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania.

Afisa Utumishi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga akitoa neno la utangulizi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole.

Mtaaluma Mkuu wa Shule ya Sekondari Mlole, Mwl. Philipo Gabriel akifuatilia kwa karibu mada iliyokuwa ikifundishwa na Mhe. Kagina (hayupo katika picha).

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mlole, Bi. Abigaeli Philipo akiuliza swali kwa Mhe. Kagina, akiomba kufahamu muundo wa Mahakama ya Tanzania.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni