Alhamisi, 2 Novemba 2023

MAZOEZI NI MWAROBAINI WA AFYA: JAJI KARAYEMAHA

Na Hasani Haufi- Mahakama, Songea

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha jana tarehe 1 Novemba, 2023 amewahimiza watumishi wote wa Mahakama katika Kanda hiyo kushiriki katika mazoezi kwani ndiyo mwarobaini wa kuimarisha afya.

Mhe. Karayemaha ametoa wito huo jana tarehe 1 Novemba, 2023 wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu katika hafla ya uzinduzi wa mazoezi kwa watumishi wa Mahakama Kanda ya Songea.

“Afya bora na imara hujengwa na kuboreshwa kwa mambo mbalimbali, lakini mazoezi kwa binadamu yamekuwa ni tiba na mwarobaini wa kuboresha na kujenga afya ya mwanadamu,’’ alimesema.

Jaji Mfawidhi alisema kuwa afya ni mtaji na utajiri mkubwa kwa binadamu, hivyo watumishi wote wanapaswa kulinda tunu waliyopewa na Mungu na njia pekee ya kufanikisha jambo hilo ni kufanya mazoezi ya mara kwa mara.

“Muda mwingi tunautumia kukaa sehemu moja, hivyo ni rahisi kupata tatizo la afya na ili kuepukana na changamoto hiyo tunapaswa kufanya mazoezi kila siku,” alisema.

Aliwakumbusha pia matumizi ya vyakula, ikiwemo vya wanga wanavyotumia kila siku ambavyo baada ya mfumo wa umeng’enywaji hutengeneza sukari na mafuta, hivyo ili kulinda afya kutokana na tatizo la magonjwa kama sukari na shinikizo la damu (pressure) wanapaswa kufanya mazoezi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akizungumza na watumishi wakati wa kuzindua mazoezi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (katikati mwenye fulana nyeupe) akishiriki kwenye mazoezi pamoja na watumishi wa Mahakama.
Mazoezi yakiwa yamepamba moto.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni