Alhamisi, 2 Novemba 2023

WANANCHI WAIPONGEZA MAHAKAMA KUU MANYARA KWA KUBORESHA HUDUMA.

Christopher Msagati – Mahakama, Manyara

Wananchi mjini Babati mkoani Manyara wameipongeza Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara kwa kuboresha huduma zinazotolewa kila siku Mahakamani.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 2 Novemba, 2023 wakati Wananchi wakipokea Elimu inayotolewa kila siku ya Alhamisi kabla ya kuanza kwa shughuli za usikilizaji wa mashauri katika viwanja vya Mahakama Kuu Manyara.

“Kwa kweli siku hizi Mahakama imebadilika kwa namna ambavyo mnatoa huduma zenu tofauti na zamani, hata huu mfumo wa kutuelimisha kila tunapofika Mahakamani unaonesha kuwa kweli mna nia ya kurejesha imani kwa Wananchi kwa sababu pia mnatufundisha taratibu mbalimbali ambazo tulikuwa hatuzifahamu hapo awali kwa hili mnastahili pongezi”, amesema Bw. Beatha Temu ambaye ni mmoja wapo wa wananchi waliohudhuria Mahakamani.

Akitoa mada kwa wananchi hao Msaidi wa Sheria Mahakama Kuu Manyara, Mhe. Thobias John aliwafundisha wananchi juu ya ‘TARATIBU ZA UKATAJI WA RUFAA KATIKA MAHAKAMA’ huku akiwasisitiza kuwa taratibu hizi huwa zinatofautiana kulingana na ngazi ya Mahakama husika.

“Ni vema kuzingatia haya ninayowafundisha sasa hivi kwa sababu ukifika Mahakama ya Wilaya utakuta taratibu zake za kukata rufaa zinatofautiana kidogo na zile za Mahakama Kuu”, amesema Mhe. John.

Mahakama Kuu Kanda ya Manyara imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa Wananchi wanaofika Mahakamani kila ya siku ya Alhamisi kuanzia saa 2 asubuhi kabla ya shughuli ya usikilizaji wa Mashauri haijaanza.

 

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mhe. Thobias John akitoa Elimu kwa Wananchi waliohudhuria Mahakamani (hawapo picha) ikiwa ni utaratibu wa Mahakama Kuu Kanda ya Manya kila siku ya Alhamisi saa 2 asubuhi.

Sehemu ya Wananchi waliofika Mahakama Kuu Manyara wakisikiliza elimu iliyokuwa ikitolewa kabla ya kuanza kusikilizaji wa mashauri.

Sehemu ya Wananchi waliofika Mahakama Kuu Manyara wakisikiliza elimu iliyokuwa ikitolewa na Mhe. John (aliyesimama) kabla ya kuanza kusikilizaji wa mashauri.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni