Alhamisi, 2 Novemba 2023

MANYARA IPO TAYARI KWA MATUMIZI YA MFUMO MPYA: JAJI KAHYOZA

Christopher Msagati – Mahakama, Manyara.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza amewasisitiza watumishi wa Mahakama, Kanda ya Manyara kutimiza majukumu yao kwa weledi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanayotokea kila wakati Mahakamani.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao leo tarehe 2 Novemba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama Kuu, Mhe. Kahyoza amesema, mfumo mpya wa usimamizi na uendeshaji wa mashauri ‘Advanced Case Management’ (e-CMS) utarahisisha kwa kiwango kikubwa shughuli za utoaji haki kwa wananchi.

“Ninawasihi watumishi wa Kanda ya Manyara tuwe mfano katika matumizi ya TEHAMA na hususani katika huu mfumo mpya ambao tunauanza. Halitakuwa jambo la busara kama wenzetu watayapokea mabadiliko haya na sisi tukabaki nyuma, ni wajibu wangu kuwakumbusha kujiandaa vema kutumia mfumo huo mpya wa uendeshaji mashauri utakao anza kutumi hivi karibuni” amesema Mhe. Kahyoza.

Akichangia wakati wa kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Hanang, Mhe. Arnold Kileo amemuhakikishi Jaji Mfawidhi Mhe. Kahyoza kuendelea kujitahidi kwa kadri ya uwezo wao kuutumia mfumo huu mpya na kusema hawatamwangusha kwa sababu wamejipanga vizuri kwa kujifunza tangu walipopokea maelekezo na kwamba wapo tayari kutekeleza.

Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kama zilivyo Kanda nyingine za Kimahakama Nchini ilipokea Maelekezo kutoka Ofisi ya Msajili Mkuu juu ya matumizi ya Mfumo wa Uendeshaji wa Mashauri ambao ni mbadala wa mfumo uliokuwa unatumika wa JSDS2.

Kikao hicho amabcho kimefanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao maarufu kama ‘Video Conference’ kimehudhuriwa na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya za Mkoa wa Manyara ambazo ni Babati, Hanang, Mbulu, Kiteto na Simanjiro pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Maafisa Utumishi, Maafisa Tawala wa Mahakama zote katika kanda hiyo.

Sehemu ya washiriki wa kikao kutoka Mahakama za Wilaya zilizopo Manyara wakionekana katika Video wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (aliyeketi kwenye kiti).

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Babati Mhe. Victor Kimario (kulia) akifuatilia kikao kilichoendeshwa kwa njia ya Mahakama Mtandao, kushoto ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Babati, Mhe. Juma Mwambago.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza akiendesha kikao kwa njia ya Mahakama Mtandao na watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara, kikao kilichohusu matumizi ya Mfumo Mpya wa Uendeshaji wa Mashauri.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni