Alhamisi, 2 Novemba 2023

KESI YA SABAYA YAVUTA WENGI MAHAKAMANI

Na Seth Kazimoto – Mahakama Kuu, Arusha

Jumla ya mashauri 87 yanatarajiwa kusikilizwa na kuamuliwa na Mahakama ya Rufani ya Tanzania kwenye vikao maalum viwili vinavyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini hapa.

Vikao hivi vilianza tarehe 30 Octoba, 2023 na vinatarajiwa kumalizika tarehe 17 Novemba, 2023. Miongoni mwa mashauri yanayosikilizwa ni rufaa ya jinai namba 231/2022 iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye anapinga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili kuachiwa huru na Mahakama Kuu Arusha.

Rufaa hiyo imesikilzwa jana tarehe 1 Novemba, 2023 na jopo la Majaji watatu linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Jacobs Mwambegele. Majaji wengine ni Mhe. Ignas Kitusi na Mhe. Leila Mgonya.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa kuanzia saa 4.00 asubuhi mpaka saa 10.00 alasiri na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu kiasi kwamba ukumbi namba nne uliokuwa umeandaliwa kutumika katika kusikiliza kesi hiyo ulionekana kuwa mdogo.

Kufuatia hali hiyo, iliamuliwa na Majaji hao kutumia ukumbi namba tatu ambao ni mkubwa zaidi japokuwa watu wengi hawakupata nafasi za kukaa ikawabidi kusimama sehemu ya nyuma ya ukumbi.

Jopo hilo la Majaji limesikiliza sababu tatu za rufaa zilizowasilishwa na upande wa mrufani, ambazo ni kama Jaji wa Mahakama Kuu alikosea kusema usikilizaji wa awali ulikuwa kinyume cha sheria.

Sababu zingine ni kama shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha lilithibitishwa bila kuacha shaka na kama kushindwa kumuuliza maswali shahidi wa pili wa upande wa mashtaka ilikuwa ni batili.

Uamuzi unatarajiwa kutolewa kabla ya Novemba 17, 2023 katika kipindi ambacho Mahakama ya Rufani itakitumia kusikiliza mashauri mbalimbali ambayo yameletwa mbele yake na kupangiwa kusikilizwa. Jumla ya mashauri 47 yanatarajiwa kusikilizwa katika kikao hicho.

Uamuzi wa Mahakama Kuu unaolalamikiwa ulitolewa na Jaji Ephery Kisanya ambaye aliwaachia huru wajibu rufaa katika shauri la jinai rufaa namba 129/2021 baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwatia hatiani katika kesi ya jinai namba 105/2021. 

Mbali na jopo hilo, kuna kikao kingine cha Mahakama ya Rufani kinachoendelea hapa Arusha ambacho Mwenyekiti wake ni Mhe. Stella Mugasha ambaye anaketi pamoja na Mhe. Patricia Fikirini na Mhe. Lilian Mashaka. Kikao hiki kinatarajia kusikiliza na kuamua mashauri 40 yaliyo mbele ya jopo hilo.

Jopo la Mawakili wa Jamhuri muda mfupi kabla ya kesi kuanza kusikilizwa.
Jopo la Mawakili wa Kujitegemea wakiwa tayari kwa kazi iliyowaleta.

Bw. Lengai Ole Sabaya (katikati mwenye shati la bluu bahari) akiwa nje ya jengo la Mahakama Kuu Arusha baada ya kesi yake kusikilizwa.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni