· Atoa wito kuimarisha ushirikiano katika haki za kimazingira
Na
Faustine Kapama, Innocent Kansha- Mahakama, Dar es Salaam
Naibu Jaji Mkuu na Makamu wa Rais wa Mahakama ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa
China, Mhe. Yang Linping leo tarehe 1
Novemba, 2023 amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
na kufanya naye mazungumzo mafupi yenye lengo la kuimarisha ushirikiano na
kujifunza kuhusu masuala ya haki za kimazingira Tanzania.
Mhe. Linping aliwasili
katika ofisi ya Jaji Mkuu wa Tanzania iliyopo katika jengo la Mahakama ya
Rufani jijini Dar es Salaam na kupokelewa na mwenyeji wake majira ya saa 4.00
asubuhi. Baada ya kupata utambulisho wa Viongozi mbalimbali wa Mahakama kutoka
pande zote mbili, wageni hao walipitishwa kwenye andiko maalumu linalohusu haki
za kimazingira Tanzania ambalo liliwasilishwa na Mkurugenzi wa Menejimenti ya
Mashauri, Mhe. Desdery Kamugisha.
Pamoja na mambo mengine,
Mhe. Kamugisha aliueleza ujumbe ulioongozwa na Naibu Jaji Mkuu na Makamu wa Rais wa Mahakama ya Upeo ya Jamhuri
ya Watu wa China kuhusu muundo wa Mahakama ya Tanzania, Mahakama zenye mamlaka
ya kusikiliza mashauri ya haki za kimazingira, sheria zinazotumika na mikataba
mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini ili kulinda mazingira.
Alieleza pia mamlaka za kiserikali zilizoundwa kusimamia mazingira na
alitoa uzoefu wa mashauri mbalimbali ambayo yameshatolewa maamuzi na Mahakama
kuhusu utunzaji wa mazingira. Baada ya wasilisho hilo, Kiongozi huyo kutoka Jamhuri
ya Watu wa China alitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya
Tanzania na China kuhusu utawala wa sheria katika haki za kimazingira ili yasiendelee
kuharibiwa zaidi.
"Kuna haja ya sisi kuimarisha ushirikiano wetu kuhusu utawala wa
sheria katika haki za kimazingira kati ya China na Afrika na kati ya China na
Tanzania kwa sababu haki za kimazingira ni za pamoja kwa kila binadamu," alisema.
Mhe. Linping alieleza kuwa China na Tanzania tayari ni washirika wa
ushirikiano wa kimkakati, kwani Rais Xi Jinping ana uhusiano wa karibu na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan.
“China na Tanzania ni marafiki wazuri na pia Tanzania ilichukua jukumu
muhimu sana katika ulinzi wa mazingira duniani. Ninaamini kwamba tunapaswa pia
kuimarisha ushirikiano wetu katika haki hasa haki za kimazingira kati ya Mahakama
zetu, tunaamini kuna maeneo ambayo nyinyi mmepiga hatua katika haki za kimazingira,
hivyo na sisi tungependa kujifunza,” alisema.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania alimueleza mgeni wake kuwa eneo la
haki za kimazingira linahusishwa na sheria nyingi na kazi kubwa ya Mahakama ni
kutafsiri sheria hizo.
“Kwa mfano, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2002, Sheria ya
Uhifadhi wa Wanyamapori, Sheria ya Misitu, Sheria ya Hifadhi za Bahari, Sheria
ya Uvuvi, pamoja na nyinginezo. Ukisoma sheria hizi zote, unaweza kutambua jinsi
zinavyolinda baadhi ya vipengele vya mazingira,” alisema.
Mhe. Prof.Juma alibainisha baadhi ya maeneo ya ushirikiano kati ya Mahakama
ya China na Mahakama ya Tanzania, ikiwemo teknolojia na pia uwepo wa vyama ndani
ya Mahakama ambapo watu kwa watu wanaweza kushirikiana.
“Nimebaini kuwa mna Chama cha Majaji Wanawake wa China, pia na sisi tuna
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania. Kwa hiyo, haya ndio maeneo
ambayo watu kwa watu wanaweza kushirikiana....
“Katika eneo la teknolojia, China iko mbele sana kuliko Tanzania na katika
baadhi ya mageuzi yetu tumechunguza China imefanya nini, katika masuala ya
uandishi na tafsiri ili kurahisisha upatikanaji wa haki. Kwa hivyo, hili ni
eneo lingine ambalo tuna mengi ya kushirikiana,” Jaji Mkuu aliwaambia wageni
wake.
Alimshukuru mgeni wake kwa kufika Tanzania na kutembelea Mahakama ya
Tanzania, kwani wameshughulikia maeneo kadhaa ambayo ni muhimu, si tu kwa
urafiki wa nchi hizo mbili bali pia ushirikiano kati ya Mahakama.
Viongozi wengine wa Mahakama
waliofuatana na Jaji Linping katika ziara yake ni Jaji Mkuu na Rais wa
Divisheni ya Mazingira na Rasilimali ya Mahakama ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa
China, Jaji Liu Zhumei na Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Mahakama
ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa China, Bi. Li Wenwen.
Wengine ni Jaji
Mwandamizi wa Divisheni ya Mazingira na Rasilimali katika Mahakama ya Upeo ya Jamhuri
ya Watu wa China, Jaji Zhu Jing, Jaji Msaidizi, Divisheni ya Mazingira na
Rasilimali katika Mahakama ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa China Qiu Yanjun, Ofisa
kutoka Mahakama ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa China Huang Zheya, Meneja Mkuu wa
Programu au Mkalimani, ClientEarth Liu Mengxing na Mwanasheria ClientEarth
Jiang Boya.
Kwa upande wa
Mahakama ya Tanzania, Viongozi waliohudhuria ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mhe. Angelo Rumisha na Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Wengine Kaimu Msajili
Mkuu na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylvester Kainda, Mkurugenzi wa Menejimenti
ya Mashauri, Mhe. Desdery Kamugisha, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano, Bw. Kalege Enock, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi na Katibu
wa Jaji Kiongozi, Mhe. Idan Mwilapwa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiagana na Naibu Jaji Mkuu na Makamu wa Rais wa Mahakama ya Upeo ya Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Yang Linping baada ya kukutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni