Na Eva Leshange, Mahakama-Singida
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imepanga kushughulikia jumla ya mashauri tisa (9) yanayohusu mauaji katika kikao chake kinachofanyika mkoani Singida kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Akisoma taarifa ya ufunguzi wa kikao cha maandalizi ya vikao maalumu vya kusikiliza mashauri ya jinai ‘criminal session’ leo tarehe 13 Novemba, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi amesema jumla ya mashauri tisa ya jinai yanategemewa kushughulikiwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo hadi tarehe 11 Desemba, 2023.
Kwa mujibu wa Mhe. Lushashi, kikao hiki ni cha tano kufanyika katika Mkoa wa Singida kwa mwaka huu, aidha, amewaeleza wajumbe kuwa, kikao hicho kitaongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt.Adam Mambi.
“Jumla ya mashauri tisa yamepangwa kusikilizwa katika kikao hiki ambapo Singida ina mashauri manne (4), Iramba manne (4) na Manyoni 1. Hata hivyo Mkoa wa Singida una mashauri 21 ambayo yanasubiri kusikilizwa (uncauselisted) ambapo Singida ina mashauri 14, Iramba 04 na Manyoni 3,” amesema Mhe. Lushashi.
Amebainisha kuwa, mashauri tajwa hayahusishi mashauri yanayosubiri washtakiwa kusomewa kwa mara ya kwanza (plea taking).
Naye, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Mambi amewapongeza wadau kwa ushirikiano ambao wanauonesha katika kufanikisha usikilizwaji wa mashauri haya na kusisitiza Mawakili kunyumbulika (kuwa flexible), kusoma majalada vizuri na kuzungumza na wateja wao vizuri.
Nao wajumbe wameeleza kwamba, wamejipanga vizuri maandalizi yote yameshafanyika na kwa upande wa Mawakili wa Kujitegemea wameisifia Ofisi ya Mtendaji kwa kuwafanyia malipo yao kwa wakati na hivyo kuwa na ari ya kazi.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni