Na. Amina Said – Kituo Jumuishi Temeke
Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Temeke kilichopo TAZARA, Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni kiliendesha mafunzo kwa watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke ya usalama na utayari dhidi ya majanga ya moto.
Kabla ya kuendesha mafunzo hayo, Askali kutoka Kituo hicho cha Zimamoto na Uokoaji, Staff Seargent (S/SGT) Prosper David alifanya ukaguzi na tathmini ya miundombinu ya kujikinga na kupambana na majanga ya moto ambapo alionesha kuridhwa na ubora wake katika jengo hilo la Mahakama.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, S/SGT David alisema baada ya kuthibitisha vifaa vilivyopo ni vingi, vya kisasa na vinaendana na mahitaji ya jingo kuwa maboresho miundombinu fursa mpya ya usalama dhidi ya majanga ya moto mahakamani.
“Vifaa ni vingi, jukumu lililopo ni kujenga uwezo wa watumishi kuvitumia. Semina za mara kwa mara ni muhimu ili kujenga utimamu na kuwa tayari kutoa msaada kwa wananchi wanaopata huduma majanga yanapotokea,” alisema.
Katika mafunzo hayo, mkufunzi alizungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo aina za moto na njia za kudhibiti, jinsi ya kujiokoa na kuokoa wengine mara janga la moto linapotokea, kufahamu aina ya vifaa vya kuzima moto na jinsi ya kuvitumia, jinsi ya kutumia mifumo iliyopo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kawaida kwenye kudhibiti moto na njia za utoaji wa taarifa za majanga ya moto kwa mamlaka husika.
Naye Mtendaji wa Mahakama wa Kituo cha Temeke, Bw. Samson Mashalla, akizungumza kuhusu mafunzo hayo alisema, “Mafunzo haya yameandaliwa ili kuwaweka sawa watumishi wa Mahakama na wadau wetu kutumia kwa ufanisi miundombinu ya kuzuia na kupambana na majanga ya moto.
“Mafunzo haya ni awamu ya kwanza kujenga ufahamu na hatua itakayofuata itakuwa mazoezi ya utayari wa kukabiliana na majanga ya moto kwa vitendo. Malengo yetu kila mtumishi na mdau ndani ya jengo awe tayari kupambana na kuondoa tatizo linapotokea,” alisema.
Maboresho ya miundombinu ya majengo ya Mahakama yanaenda sambamba na usimikaji wa mifumo bora ya kisasa ya kujikinga na kukabiliana na majanga ya moto. Usalama wa watumishi, wadau na wananchi wanaopata huduma katika Kituo umezingatiwa kwenye ujenzi wa jengo na usimikaji wa miundombinu yake.
Kufanyika kwa mafunzo hayo ni utaratibu wa kawaida wa elimu kwa watumishi wa Kituo Jumuishi Temeke wa kila siku ya Ijumaa asubuhi baada ya kikao cha tathmini ya wiki iliyopita na kuweka mikakati ya wiki inayofuata.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, Jaji wa Mahakama Kuu katika Kituo hicho, Mhe. Gladys Barthy, Naibu Msajili, Mhe. Frank Lenard Moshi, Bw. Mashalla Viongozi wengine.
Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (wa pili kushoto mstari wa ebele) akiwa patika picha ya pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama, akiwemo Jaji Gladys Barthy (wa pili dulia), Naibu Msajili, Mhe. Frank Moshi (wa kwanza kulia) na Mtendaji, Bw. Samson Mashalla (wa kwanza kushoto). Katikati ni S/SGT Prosper David kutokaKituo cha Zimamoto na Uokoaji Temeke.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni