Alhamisi, 16 Novemba 2023

MAHAKAMA KUU MANYARA YAADHIMISHA MWAKA MMOJA

Christopher Msagati-Mahakama, Manyara

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Manyara imeadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake mnamo tarehe 15 Novemba, 2022, imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mkoa huo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakipata changamoto ya kupata huduma za Mahakama Kuu hivyo kulazimika kuzifuata mkoani Arusha ikiwa ni umbali wa takribani kilomita 168.

Akifungua maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza aliwashukuru watumishi na wadau wote waliohudhuria na kusisitiza kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuwezesha shughuli mbalimbali za Mahakama kufanikiwa.

“Sisi sote tulioko hapa ni sehemu kubwa ya safari ambayo tulianza Mwaka jana, na ni jambo la kipekee sana kukutana tena leo katika kuadhimisha kumbukumbu ya safari hii. Tumefanya kazi kwa ushirikiano na sasa matunda ya Mahakama hii yanaonekana. Ninawaomba mshikamano huu uendelee ili tuweze kutoa haki kwa wakati”, alisema Mhe. Kahyoza.

Maadhimisho hayo, yaliambatana na kusoma taarifa ya tathimini ya utendaji kazi tangu kuanzishwa kwa Masjala ndogo hiyo ikiwa ni pamoja na mafanikio, changamoto na mipango ya baadaye. Vile vile kulikuwa na keki iliyoandaliwa kama ishara ya kumbukumbu ya maadhimisho hayo.

Akiongea kwa niaba ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Manyara Mwendesha Mashtaka Mfawidhi Mkoa Bi Chema Maswi aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ili malengo ya kitaasisi yatimie kwa wakati.

“Sisi nasi ni sehemu kubwa ya mabadiliko ambayo Mahakama inataka kuyatekeleza, hivyo ninaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ili tuwezeshe mabadiliko hayo yatekelezeke kwa vitendo”, aliongeza Bi Maswi.

Aidha, maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ambao ni Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Manyara, Jeshi la Polisi na Magereza Manyara, Mawakili wa Kujitegemea wa Mkoa wa Manyara pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (katikati walioketi) na sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya maadhimisho ya Mwaka Mmoja wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara yaliyofanyika tarehe 15 Novemba,2023 katika ukumbi wa Mahakama hiyo. Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Gladys Barthy (kushoto) na kulia ni Mwendesha Mashtaka Mfawidhi kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Manyara Bi Chema Maswi. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe John Kahyoza akikata keki kuashiria maadhimisho ya Mwaka mmoja wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, akisaidiwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Gladys Barthy (kushoto) na kulia ni Mwendesha Mashtaka Mfawidhi kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Manyara Bi Chema Maswi.

Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara pamoja na wageni waalikwa  wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho hayo, katikati mstari wa mbele ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe. Bernard Mpepo.

(Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni