Alhamisi, 16 Novemba 2023

WAZIRI KATIBA, SHERIA ATEMBELEA KITUO JUMUISHI CHA MASUALA YA FAMILIA –TEMEKE

 Na. Innocent Kansha - Mahakama

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameridhishwa na utendaji wa watumishi wa Mahakama kwa kushirikiana na wadau wa haki katika kuhakikisha dhana zima ya Kituo Jumuisha inakuwa suluhu ya kudumu kwa wananchi wanaotafuta haki zao hasa katika masuala ya kifamilia.

Mhe. Dkt. Chana jana tarehe 15 Novemba, 2023 alitembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kukagua shughuli mbalimbali za kiutendaji na kupokelewa na mwenyeji wake Jaji Mfawidhi, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.

Lengo lingine la ziara hiyo ya Waziri katika kituo Jumuishi hicho lilikuwa kujifunza kutoka kwa wataalamu wanaotoa huduma na kuona jinsi gani Kituo hicho kinavyofanya kazi katika kuwahudumia wananchi.

Waziri Chana alipata wasaa wa kupokea maelezo na ufafanuzi juu ya muundo wa uendeshaji wa shughuli za Mahakama na kufafanuliwa kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama namba 4 ya mwaka 2021. Vile vile alipata maelezo juu ya tarehe ya kuanza kufanya kazi na huduma zitolewazo na wadau waliopo katika kituo kituo hicho.

Akiwa Kituoni hapo Mhe. Dkt. Chana alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo chumba maalum cha kuratibu masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama vile mfumo mpya uliosimikwa wa (e -case management na record centre), mfumo wa kusajili wateja, PA system.

Aidha Dkt. Chana alikagua kumbi za wazi za kituo hicho na kujionea miundombinu ya kisasa iliyowekwa kwenye kumbi hizo kwa ajili ya kuendeshea mashauri na chumba maalumu ambacho kimetengwa kwa ajili ya akina mama kunyonyesha watoto wachanga wanapofika katika kituo hicho kupata huduma.

 Maeneo mengine aliyotembele Waziri Chana kabla ya kuzungumza na wadau ndani ya kituo hicho ni kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu (LHRC), Kituo cha msaada wa kisheria cha wanawake (WLAC), Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi, Mahakama ya watoto (Juvenile Court) na Ofisi ya Ustawi wa Jamii na kupokea maelezo ya taratibu mbalimbali za kuwahudumia wananchi.

Akizungumza na wadau baada ya kufanya ukaguzi huo, Waziri Chana aliupongeza Uongozi wa Mahakama kwa kubunifu mkubwa wa kuanzisha kituo hicho kinachowahudumia maelfu ya wananchi wenye shida za kisheria, hasa katika eneo la masuala ya familia.

“Sisi kama Wizara ya Katiba na Sheria tupo tayari, mlango wetu upo wazi muda wote kuendelea kutoa ushirkiano wa hali na mali kuendeleza jitihada za Mahakama katika kuboresha mazingira ya utoaji haki, ikizingatiwa haki inadumisha Amani na kuleta utulivu miongoni wa wanajamii”, alisema. 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (wa pili kulia) akipokea maelekezo ya namna wateja wanavyohudiwa mara wafikapo Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kutoka kwa Naibu Msajili wa Kituo hicho Mhe. Frank Moshi (aliyenyoosha mkono) wakati wa ziara hiyo iliyofanyika jana tarehe 15 Novemba, 2023.

 

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (kulia) akimpokea Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (kushoto) mara alipowasili Kituoni hapo kwa ajili ya kutembelea na kujifunza taratibu mbalimbali za uendeshaji wa mashauri ya kifamilia. 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (kushoto) akizungumza na sehemu ya wamama wanaonyonyesha kwenye chumba maalum kilichotengwa ndani ya Kituo hicho.


Afisa TEHAMA wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke (aliyenyoosha mkono) akimweleza Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (katikati) namna mifumo mbalimbali ya kuratibu uendeshaji wa mashauri inavyofanya kazi na kurahisisha shughuli za utoaji haki kituoni hapo.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke (aliyevalia kitenge kushoto) akimpa maelezo ya kina ya namna anavyotekeleza majukumu yake ndani ya kituo hicho Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (kulia)

Afisa kutoka kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu (LHRC) (kushoto) akifafaua jambo mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (kulia) alipotembelea Ofisi hiyo kujionea namna wanvyotekeleza majukumu yao.

  

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (kushoto) akitoa ufafanuzi wa jambo mbele ya Maafisa kutoka kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu (LHRC) alipowatembelea Ofisini hapo.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia - Temeke mara baada ya kuhitimisha ziara yake Kituoni hapo.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia - Temeke mara baada ya kuhitimisha ziara yake Kituoni hapo.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni