Emmanuel Oguda, Mahakama Kuu-Shinyanga
Jumla ya Mashauri 60 yaliyokuwa yakisikilizwa na Majaji watatu wapya Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga yamesikilizwa na kumalizika ndani ya siku 30 pekee huku yakitajwa kupunguza mzigo wa mashauri ndani ya Kanda hiyo.
Hayo yalibainishwa tarehe 20 Novemba, 2023 na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali wakati akitoa tathmini ya utendaji kazi kwa kipindi cha siku 30 kwa Majaji hao wakati wa kikao kazi cha watumishi wa Mahakama Kuu kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano Mahakama Kuu Shinyanga.
Jaji Mahimbali alisema kuwa, Majaji hao walipangiwa mashauri 20 kila mmoja na kufanikiwa kusikiliza na kumaliza mashauri yote ndani ya siku 30 pekee kuanzia tarehe 23 Oktoba hadi 23 Novemba mwaka huu.
Akitoa salamu za pongezi kwa Majaji hao, Jaji Mahimbali alieleza kwamba, idadi ya mashauri 60 kwa kupindi cha siku 30 pekee ni kubwa na kuongeza kuwa, Majaji hao wamefanya kazi kubwa kwa kipindi hicho na kuifanya Kanda ya Shinyanga kupunguza mzigo wa mashauri ambayo kimsingi ingewawia vigumu Majaji watatu wa Kanda hiyo ambao nao wapo Katika vikao vya Mahakama Kuu katika vituo vya Kahama na Bariadi.
“Kila Jaji alipangiwa jumla ya mashauri 20, ninayo furaha kwa niaba ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kuwashukuru sana kwa kazi kubwa, mmetupa hamasa kubwa sana kumaliza mashauri 60 ndani ya kipindi cha siku 30 pekee, hongereni sana na tunawatakia kila la kheri katika vituo mlivyopangiwa’’ alisema Jaji Mahimbali.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Ntuli Mwakahesya miongoni mwa Majaji watatu waliosikiliza na kumaliza mashauri hayo na kupata bahati ya kusalia katika Kanda hiyo, ametoa pongezi kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa watumishi.
Aliongeza kuwa, ni furaha kwake kupangwa kuendelea kuitumikia Kanda ya Shinyanga katika kazi ya Ujaji wa Mahakama Kuu.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Emmanuel Kawishe miongoni mwa Majaji waliosikiliza mashauri hayo aliwashukuru watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga kwa ushirikiano katika kazi na kuongeza kuwa, amejifunza vitu vingi kwani watumishi aliofanya nao kazi katika kipindi hicho wamekuwa Walimu wazuri kwake kuhakikisha anafanya kazi vizuri na kuwezesha kumaliza mashauri yote 20 aliyopangiwa.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Frank Mirindo pia alitoa shukrani zake kwa watumishi wa Kanda ya Shinyanga na kufurahi kuona baadhi ya Watumishi waliwahi kuwa wanafunzi wake wakati akifunda Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Majaji hao ni miongoni mwa Majaji 20 wapya walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo baada ya kupata mafunzo (induction) kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), walipangiwa kusikiliza mashauri 60 ambapo kila mmoja akisikiliza na kumaliza mashauri 20 ndani ya siku 30 pekee.
Mashauri hayo yamesikilizwa na kumalizwa na Majaji watatu ambao ni Mhe. Ntuli Mwakahesya, Mhe. Emmanuel Kawishe na Mhe. Frank Mirindo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (katikati) akizungumza na watumishi wa Kanda hiyo (hawapo katika picha) tarehe 20 Novemba, 2023 wakati wa kikao cha tathmini ya utendaji kazi kilichofanyika Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, wengine kutoka kushoto ni Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita na kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti.
Jaji wa Mahakama Kuu miongoni mwa Majaji waliosikiliza mashauri aliyepangiwa kituo cha kazi Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Emmanuel Kawishe akiwashukuru watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga kwa ushirikiano.
Jaji wa Mahakama Kuu aliyepangiwa kituo Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara na miongoni mwa Majaji waliosikiliza mashauri 60, Mhe. Frank Mirindo akitoa neno la shukrani kwa kuhudumu Kanda ya Shinyanga kwa kipindi cha mwezi mmoja.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni