Jumatano, 22 Novemba 2023

MAWAKILI DAR ES SALAAM KUTEMBELEA MAGEREZA KUSIKILIZA WATEJA WAO

  • Ni mpango ulioandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam

Na Eunice Lugiana, Mahakama Kuu-Dar es Salaam

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeandaa mpango wa kuwapeleka Mawakili wa Kujitegemea kutembelea wateja wao waliopo gerezani waliopangwa kuwatetea washtakiwa wa makosa makubwa ili wapate fursa ya kuonana na wateja wanaowawakilisha  Mahakamani kwenye mashauri ya Jinai hususani Mashauri ya Ugaidi, Mauaji na Mashauri ya Madawa ya kulevya.

Akizungumza na Mawakili waliopangiwa Mashauri hayo waliofika Mahakama Kuu Dar es Salaam tarehe 20 Novemba, 2023 ili kuelekea Gereza la Ukonga, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi alisema, hatua hiyo ilitokana na changamoto mbalimbali walizozitoa mahabusu wa makosa makubwa ikiwemo kukosa muda wa kutosha wa kuzungumza na Mawakili. 

Kwa mujibu wa Mhe. Maghimbi, mara nyingi mahabusu hao wamekuwa wakikutana na Mawakili kwa muda mchache wa kusikilizwa na pengine Wakili anaonana na mahabusu wakiwa mahakamani hiyo nayo imewafanya mahabusu hao kuona kama hawatendewi haki.

Katika kutatua changamoto hiyo Mahakama imeanza na hatua ya kuwakutanisha mahabusu na Mawakili wao katika Gereza la Ukonga kwa gharama za Mahakama ili kuhakikisha haki inafikiwa kwa wakati.

Mhe. Maghimbi alisema mpango huu ni matokeo ya ukaguzi unaofanya katika Magereza yaliyopo kanda ya Dar es Salaam ambapo Mahabusu  wamekuwa wakitoa changamoto zao, hivyo walikaa na kutafuta njia ya kutatua changamoto hizo.

Jaji Mfawidhi huyo ameahidi kusimamia na kuhakikisha changamoto  hii inaondolewa na pia ameahidi ataandaa mpango bora wa kusimamia changamoto hiyo. 

“Tumekubaliana na Magereza kuwa zoezi kama hili litakua endelevu wakati wote tunapokuwa tumeandaa vikao vya Mahakama Kuu kwa Mashauri kama haya.” alisema Jaji Mfawidhi.

Aliwakumbusha  pia Mawakili wote  wa Kujitegemea  ndani ya Kanda ya Dar es salaam kutimiza wajibu wao ipasavyo maana Mahakama inajitahidi kutekeleza jukumu hilo.

Naye, Mwenyekiti wa Timu ya Mawakili hao, Wakili Mohamed Tibanyendera alisema wamefarijika na utaratibu huo maana ni kwa mara ya kwanza kuona Mahakama inatumia rasilimali zake kwa Mawakili wa Kujitegemea waliochaguliwa kusikiliza mashauri na  Serikali na vilevile Mahakama kutoa ukumbi wenye huduma zote za mikutano katika Mahakama Kuu na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni. 

“Tunaipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa mpango huu ambao tumeupokea kwa mtazamo chanya,” alisema Wakili Tibanyendera.

Kitu kingine cha kitofauti ambacho Wakili huyo alifurahishwa nacho ni pamoja na kupewa usafiri, kuombewa kibali cha kuingia Magereza pamoja na kupewa Uongozi wa Mahakama ambapo Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe. Joseph Luambano aliambatana nao.

Kitu kingine ambacho Mawakili hao walifurahishwa nacho na kuipongeza Mahakama kuu Kanda ya Dar es Salaam ni kuombewa ruhusa Mawakili wanaoshughulikia kesi hizo katika Mahakama zote ili kuwapunguzia usumbufu Mawakili kusafiri kupeleka barua ya ahirisho la shauri katika Mahakama zingine kufuatia vikao hivyo.

Pia ameomba taarifa kuhusu vikao vya mashauri vinavyoendelea ziweze kutumwa na kuufikia umma kwa wakati.

 Naye, Mkaguzi Msaidizi wa Magereza Stima alieleza changamoto wanazokutana nazo ikifika wakati wa kuwasaidia wafungwa kufungua rufaa zao kutokana na kuwa Mahakama mtandao. Ameiomba Mahakama kufikiria namna ya kuwasaidia ikiwemo kuwapatia vifaa vya kuwawezesha kufungua mashauri ya rufaa.

Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Dkt. Mwaibako ameishukuru Mahakama kwa mpango huo maana utawaondolea msongo wa mawazo kama Maafisa wa Magereza maana malalamiko yamekuwa mengi kwa mahabusu hao, ameomba mpango huo uwe endelevu.

Mawakili wa Kujitegemea wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Gereza la Ukonga baada ya kumaliza kuzungumza na Wateja wao /Mahabusu (hawapo katika picha) tarehe 20 Novemba, 2023.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kushoto) akizungumza na Mawakili wa Kujitegemea (hawapo katika picha). Kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joseph Luambano.

 Mawakili Wakujitegemea Wakimsikiliza Jaji Mfawidhi, Mhe. Salma Maghimbi (hayupo katika picha) katika Ukumbi wa Mahakama Kuu kabla ya kuanza safari ya kuelekea Gereza la Ukonga tarehe 20 Novemba, 2023.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joseph Luambano (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Gereza la Ukonga Kamishna Msaidizi Wa Magereza Dkt.  Mwaibako Juma (aliyesimama kulia kwa Mhe. Luambano)

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni