Na. Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya
Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA),
wametoa mafunzo ya namna ya kushughulikia kesi za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia
kwa wanawake na watoto. Mafunzo hayo yamefanyika hivi karibuni mkoani Mbeya
yakihusisha waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu Mbeya, Mahakimu kwa mkoa wa
Mbeya na Songwe.
Akifungua mafunzo hayo, Afisa Tawala wa Mkoa wa Mbeya
Bw. Lodric Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Juma Homera alisema Uongozi
wa Mkoa umefurahishwa sana kwa mafunzo hayo kufanyika mkoani hapo kwani Mbeya
ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza katika vitendo vya ukatili wa kijinsia
kwa Tanzania Bara, na pia Tanzania ikiwa inaelekea kuadhimisha siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia. Hivyo mafunzo hayo yanaweza kuiwezesha jamii kujua haki na
sheria na mtiririko wa hatua za kuchukua mtu anapokuwa na matatizo kama hayo
mahakamani.
“Nimefurahi kuona kuwa mafunzo haya yamejumuisha
Majaji na Mahakimu wa ngazi zote za Mahakama na wa jinsia zote mbili, kike na
kiume. Hivyo nina matumaini kuwa washiriki watapata fursa ya kuchangia
kubadilishana Mawazo ya namna bora ya kushughulikia kesi au migogoro
inayohusiana na ukatili wa kijinsia”, alisema Bw. Mpogolo
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania
(TAWJA) Mhe. Barke Sehel alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu na ya kipekee
yanayohusiana na namna ya kushughulikia kesi au matatizo ya ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto hivyo yanahitaji umakini mkubwa.
Aidha, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mbeya na Makamu Mwenyekiti wa TAWJA Mhe. Victoria Nongwa alimpongeza mgeni
rasmi kwa kutumia muda wake kuja kuwaunga mkono Majaji na Mahakimu pamoja na
washiriki wote wa mafunzo hayo.
Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni