Jumatatu, 27 Novemba 2023

SABABU JAJI RAIS MAHAKAMA KUU ZIMBABWE KUCHAGUA TANZANIA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube leo tarehe 27 Novemba, 2023 amekutana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na kuelezea namna anavyofurahishwa na uwepo wa ushirikiano mzuri kati ya nchi mbili na Mahakama.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi katika Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dube ambaye ameambatana na maofisa wengine wanne wa ngazi ya juu wa Mahakama kutoka Zimbabwe ameeleza kuwa nchi hizo mbili ni marafiki wa muda mrefu na wanathamini michango ambayo Tanzania inatoa kwa Zimbabwe.

“Kama ulivyoangazia hapo awali, Tanzania ni rafiki wa muda mrefu wa Zimbabwe, (……) Kuna nchi nyingine nyingi za Kiafrika katika Bara hili, ambazo ziko vizuri kwenye mfumo huu wa usimamizi wa mashauri, lakini tumekuchagua wewe (Tanzania) kwa sababu ya uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili,” amemweleza mwenyeji wake.

Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe amesema kuwa wamekuja Tanzania kujifunza shughuli mbalimbali za kimahakama kutokana na maboresho makubwa ambayo Mahakama ya Tanzania imeyafanya katika mnyororo wa utoaji haki, hasa katika maeneo ya mnenejimenti ya mashauri na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

"Tuko hapa kujifunza, tumeanza mfumo huo, lakini ni wazi tunataka kufanya maboresho (….) Kabla ya kuanza mfumo huo, tulikuwa tunasikiliza mashauri ana kwa ana, nyaraka zilikuwa zinawasilishwa kwa mkono. Tunatumaini tutajifunza mengi kutokana na uzoefu wenu, na sisi tutabadilishana kile kidogo tulichokusanya kwa miaka miwili iliyopita hadi sasa,” alisema.

Jaji Rais alielezea matazamio yao kujifunza pia jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyopitia mfumo wa kuifanya nchi kuunganishwa kimtandao kwani pindi mtu anapokwenda vijijini, anaweza kupata mtandao kwa urahisi, hivyo wangetamani kujua hilo lilivyowezekana kufanyika.

Mhe. Dube alirejea kwenye Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika na Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha, Tanzania, ambapo wajumbe walielezwa mafanikio kadhaa ambayo Mahakama ya Tanzania imeyapata, ikiwemo maendeleo katika kuchukua kumbukumbu, kunukuu na kutafsiri mwenendo wa mashauri.

“Hatuelewi hasa mnaendeshaje hili, hiyo ni sababu mojawapo ya sisi kuwa hapa, tunataka kujifunza ili tukirudi nyumbani tuweze kutekeleza mfumo huo. Pia tuko hapa kuangalia jinsi gani Tanzania imepata njia ya kuwafanya watu kutoka vijijini kuunganishwa kwa urahisi na mfumo huo,” amesema.

Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa mapokezi makubwa waliyoyapata kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo walipokelewa vizuri na kusindikizwa hadi hotelini. Alisema hiyo ni picha ya mtu rafiki mzuri, ambaye ni Tanzania.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania alimweleza Jaji Rais wa Mahakama Kuu Zimbabwe na ujumbe wake kuwa uamuzi wao wa kuichagua Tanzania kuwa sehemu ya kuja kujifunza ni fursa ya kipekee kwa sababu kuna mamlaka nyingine nyingi za Ulaya na Nchi za Afrika ambazo zina maendeleo makubwa katika mfumo wa menejiment ya mashauri.

Alieleza kuwa ziara ya Mhe. Dube ni muhimu kwani inaruhusu pande zote mbili kubadilishana maarifa na uzoefu ili kuendeleza malengo yao ya pamoja ya utoaji haki. "Tunafuraha kushiriki katika mijadala yenye kujenga na kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu," Mhe. Siyani alisema.

Jaji Kiongozi alieleza kuwa kubadilishana uzoefu ili kuonyesha uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili ni muhimu. 

Alisema kuwa nchi hizo mbili zilizoshiriki katika ukombozi wa Zimbabwe na ushirikiano wa mwendelezo, ikiwemo mipango ya maendeleo baada ya uhuru ambapo Tanzania ilipeleka Majaji kutumikia Mahakama Kuu Zimbabwe, inaonesha ushirikiano wa kudumu uliopo kati ya mataifa hayo.

"Kubadilishana huku kwa uzoefu wa kihistoria unaonyesha dhamira yetu ya kukuza ushirikiano wa muda mrefu ambao unavuka mipaka na kizazi," Mhe. Siyani alisema. 

Alimtaarifu mgeni wake kuwa wameandaa programu ya kina ili kuhakikisha ziara hiyo inakuwa yenye tija na walikuwa na shauku ya kupeana ufahamu na mijadala inayoimarisha ushirikiano wao wa kimahakama.

Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania walikuwepo kwenye mkutano huo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mhe. Dkt. Anjelo Rumisha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri, Mhe. Desdery Kamugisha, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Bw. Leonard Magacha na Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Aidan Mwilapwa.

 

Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe aliwasili Tanzania jana tarehe 26 Novemba, 2023 kwa ziara ya siku tatu. Ameambatana na maafisa wengine akiwemo Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana, Msajili wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Kudzai Maronga, Mkuu wa Fedha wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Milton Shadaya na Mkuu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Obey Mayenga.



Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (kushoto) akisalimiana na mwenyeji wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu.



Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (juu) akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na mwenyeji wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (picha chini).



Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.

Ujumbe wa Mahakama ya Tanzania ukichukua kumbukumbu wakati wa mkutano huo. Kutoka kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mhe. Dkt. Anjelo Rumisha na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel. Kushoto mwanzoni ni Mkuu wa Fedha wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Zimbabwe, Bw. Milton Shadaya.

Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (wa kwanza kushoto) akiuongoza ujumbe wake kwenye mkutano huo. Anayemfuatia ni  Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana, Msajili wa Mahakama Kuu Zimbabwe, Mhe. Kudzai Maronga na Mkuu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Obey Mayenga.



Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (juu na chini) akipata maelezo kutoka kwa wataalamu wa TEHAMA wa Mahakama ya  Tanzania namna kituo cha mtandao kinavyofanya kazi.



Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (kulia) na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kushoto).


Meza Kuu ikiongoozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati). Wengine ni Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (wa pili kushoto),  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (wa pili kulia), Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana (wa kwanza kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia).

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Zimbabwe.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wote waliohudhuria mkutano huo. 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni