Jumanne, 28 Novemba 2023

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI SIMIYU MBIONI KUFUNGA MASHAURI YA MIRATHI

Na Naumi Shekilindi-Mahakama-Simiyu

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga hivi karibuni aliongoza kikao cha Menejimenti Mkoa wa Simiyu kutathmini utendaji kazi na kuweka mikakati ya namna ya kufunga mashauri ya mirathi. 

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Gasto Kanyairita akiwa kama Katibu wa kikao, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya, Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala na Wahasibu wote wa Mahakama Mkoa wa Simiyu.

Akizungumza wakati anafungua kikao hicho, Mhe. Mahumbuga alisisitiza mambo makuu mawili, ikiwemo Mahakimu kuwa na tabia ya kusimamia, kufuatilia na kutathmini yale wanayoyapanga.

Jambo jingine ni kuwa na ubunifu na ushikiriano katika kazi ili kufikia lengo la Mahakama katika kutoa haki na huduma bora kwa wananchi 

“Kila mmoja aweze kujitathmini, tuchukue mawazo baina yetu na kushirikiana,” alisema Mhe. Mahumbuga.

Katika kikao hicho, Mahakimu Wafawidhi kutoka kila Mahakama ya Wilaya waliwasilisha taarifa ya hali ya mashauri, yakiwemo ya mirathi katika kipindi cha mwezi mmoja toka kufanyika kwa kikao cha menejimenti cha mwezi uliopita.

Taarifa hizo zinaonesha kuwa Mahakama za Mwanzo zilizopo ndani ya Mkoa wa Simiyu zimefanikiwa kufunga mashauri ya mirathi kwa silimia 50 kwa kipindi cha mwezi mmoja toka tarehe 27 Octoba, 203 hadi tarehe 24 Novemba, 2023. 

Mara baada ya kuweka mkakati wa namna ya kufunga mashauri ya mirathi, Mahakimu sasa wamejipanga kwenda kumaliza yaliyobaki kwa kutumia mbinu na uzoefu walioupata kutoka katika kikao hicho.

Naye Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu aliwasisitiza Mahakimu, Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala kuhakikisha wanathibiti na kufufua maeneo na mipaka ya Mahakama na kuwapa notisi Taasisi au watu wanaotumia majengo ya mahakama bila vibali.

Aliwaomba pia kufanya ukarabati wa majengo ya Mahakama yaliyochakaa na ujenzi wa vyoo katika Mahakama za Mwanzo zilizopo Mkoa wa Simiyu.

Mtendaji pia aliwaelekeza Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala kuwasisitiza watumishi kuwa na desturi ya kujua afya zao lakini pia kutoa elimu kwa watumishi ili kujua umuhimu wa kupima afya.

Kadhalika, Bw. Kanyairita aliwaasa watumishi wote wajiandae kwa ajili ya wiki ya sheria nchini kwa mwaka 2024 ambayo ina kauli mbiu inayosema, Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa taifa: Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai”.

Mwenyekiti wa kikao, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu Mhe. Martha Mahumbuga (kulia) akizungumza wakati anafungua kikao hicho. kushoto ni Katibu wa kakao ambaye ni Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita.

Wajumbe wa menejimenti wakiwa ukumbini wakati kakio kinaendelea.

Picha ya pamoja na wajumbe wa waliohudhuria kikao cha menejimenti.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni