Jumatano, 29 Novemba 2023

TAWJA YATOA ELIMU KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA

Na Arapha Rusheke-Mahakama Kuu, Dodoma 


Chama cha Majaji na Mahakimiu Wanawake Tanzania (TAWJA) katika Mkoa wa Dodoma hivi karibuni kilitoa elimu kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia juu ya udhalilishaji wa kimtandao dhidi ya watoto.

Elimu hiyo ilitolewa kwenye semina iliyoandaliwa na chama hicho katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Akifungua semina hiyo na kutoa salaam za ufunguzi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma na mlezi wa TAWJA Tawi la Dodoma, Mhe.  Dkt. Juliana Masabo alisema imekuwa ni nafasi ya kipekee kukutana kwa ajili ya kujifunza na kukumbushana kuhusu makosa ya kimtandao, sheria zinazotumika, uendeshaji wake wa kesi za aina hii na adhabu zake.

“Nichukue fursa hii kushukuru uongozi mzima wa Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuiwezesha TAWJA kushiriki katika jambo hili muhimu na kipekee sana,” alisema.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi aliishukuru Wizara ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Balozi, Mhe Dkt. Pindi Chana kuweza kushirikiana na Mahakama ya Tanzania na TAWJA bega kwa bega ili kufanikisha shughuli zao za kila siku.

Alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inayosema, “Ungana, wekeza kuzuia ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto” ni muhimu kwani inawahamasisha wote bila kujali tofauti zao kusimama pamoja na kuwa sehemu ya mabadiliko katika kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.

Naye Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Nkasori Sarakikya ameishukuru TAWJA kwa kumpa nafasi adhimu ya kuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo.

 

“TAWJA mmeamua kuja na uelimishaji kwa njia ya vitendo, elimu imeandaliwa kwa lengo la kuwalinda watoto, mwanamke na vijana na hatimaye jamii nzima itakuwa salama kwani hawa ndio waathirika wakuu wa masuala ya ukatili wa kijinsia,” alisema.

 

Semina hiyo ililenga kuwaelimisha wanawake kuhusu ukatili ambapo mwanamke ana nafasi kubwa kuupunguza kama akikaa vizuri kwenye nafasi yake mahali popote anapokuwa.


Meza Kuu ikiongozwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Nkasori Sarakikya ambae ni mgeni rasmi akizungumza na sehemu ya wanachama wa TAWJA pamoja na wadau.


Sehemu ya wanachama wa TAWJA Mkoa wa Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Meza kuu ikiongozwa na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Nkasori Sarakikya (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja.


Meza kuu ikiongozwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Nkasori Sarakikya katikati wakiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni