Na. FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Mary Dube leo tarehe 28 Novemba, 2023 amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kupongeza kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Famili Temeke ambacho kipo mahususi kushughulikia mashauri yanazohusiana na familia.
Mhe. Dube alimweleza Jaji Mkuu katika siku ya pili ya ziara yake jinsi alivyofurahishwa na jengo kubwa la Kituo cha Haki Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke aliloliona jana tarehe 27 Novemba 2023 pamoja na mipangilio yake ya kujumuisha wadau wote wa masuala ya utoaji haki, hususan Maafisa Ustawi wa Jamii.
"Nimefurahishwa sana na kile kinachoendelea katika kituo hicho. Tuna divisheni ya masuala ya kifamilia katika Mahakama Kuu, lakini ni ndogo sana ikiwa na majaji wanne na ni sehemu ya Mahakama Kuu kama vile ile Mahakama Kuu huko Harare, hatuna divisheni ya masuala ya familia inayojitegemea...
"Ukiwa nayo unabobea, unafanya vizuri zaidi, unaangalia mambo mengine ya sheria ya familia ambayo unaweza kuweka. Niliona maafisa ustawi wa jamii. Hatuna mfumo ambao tuna maafisa ustawi wa jamii wanaosaidia watoto na wanawake," alisema.
Jaji Rais amemshukuru Jaji Mkuu kwa kukubali wito wao na kwa mapokezi mazuri waliyoyapata tangu siku ya kwanza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kwamba ziara yao imekuwa ya mafanikio zaidi.
“Unajua kwa nini tuko hapa, tumekuja hapa kujifunza, tumekuja hapa kubadilishana uzoefu na kuungana na Majaji wenzetu. Ni muhimu tufahamiane katika kiwango hiki na mimi na wenzangu kabla hatujafika hapa, tayari tuna uhusiano. Ninaamini uhusiano huu utaendelea katika siku zijazo,” amesema.
Mhe. Dube pia alishukuru kwa mpango mahsusi ambao umewawezesha kujifunza mengi na kupata fursa ya kusikiliza mawasilisho ya mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri, ambapo wamegundua upo sawa na ule walionao, lakini una mapungufu yaliyowasababisha kuja Tanzania.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania alimshukuru Jaji Rais na timu yake kutoka Zimbabwe kwa ziara hiyo na kwa mara nyingine akamkaribisha nchini Tanzania, akitarajia kuwa mawasiliano hayo yataendelea.
Prof Juma alimueleza Mhe. Dube kwamba wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika na Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha alikutana na Jaji Mkuu wa Zimbabwe, ambaye alisisitiza kuwa atatuma ujumbe hivi karibuni nchini Tanzania.
“Sikujua kuwa itakuwa ni hivi karibuni, nimefurahi sana kwa sababu sisi Majaji Wakuu tumekuwa tukijadili mambo mengi, lakini pia katika ngazi za chini ni muhimu kujifunza na kujadiliana uzoefu. Mimi nimefurahi sana kwamba umetutembelea, nina hakika umeona tunachofanya," alisema.
Jaji Rais wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe aliwasili Tanzania tarehe 26 Novemba, 2023 kwa ziara ya siku tatu. Ameambatana na maafisa wengine akiwemo Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Walter Chikwana, Msajili wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe, Mhe. Kudzai Maronga, Mkuu wa Fedha wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Milton Shadaya na Mkuu wa Teknolojia ya Habari (IT) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Obey Mayenga.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akisalimiana na Jaji Rais wa Mahakama Kuu nchini Zimbabwe, Mhe. Mary Dube (kushoto) alipowasili Ofisini kwake jijini Dar es salaam leo tarehe 28 Novemba, 2023 kwa ajili ya kumtembelea ili
kumfahamisha mafanikio ya ziara yake ya kujifunza nchini Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na ujumbe kutoka nchini Zimbabwe ulioambatana na viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania ulipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni