·Mtendaji Mkuu, Wakandarasi wasaini mikataba
·Aonya ulipuaji, ataka kazi kukamilika kwa wakati
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama
Mahakama ya Tanzania leo tarehe 3 Novemba, 2023 imesaini mikataba yenye
thamani ya shilingi bilioni 49 na makampuni manne kwa ajili ya ujenzi wa Vituo Jumusihi
vya Utoaji Haki (IJCs) sita katika Mikoa ya Songea, Katavi, Geita, Njombe,
Simiyu na Songwe.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ndiye
aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo iliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke. Viongozi mbalimbali
wa Mahakama, wakiwemo Mkuu wa Kitengo cha Maboresho (JDU) na Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani,
Bw. Victor Kategele wameshuhudia utiaji saini huo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ametia saini mikataba hiyo sita kwa niaba ya
Mahakama, huku maofisa wa kampuni nne za ujenzi, za ndani na nje ya nchi,
wakisaini kwa makampuni zao na kushuhudiwa na Wakurugenzi na Wakuu wa Idara wa
Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza baada ya hafla
hiyo, Prof. Ole Gabriel amewataka wakandarasi na washauri elekezi kuzingatia
muda wa mkataba na mambo yote waliyokubaliana wakati wanapotekeleza ujenzi wa
majengo hayo na kuhakisha kazi inafanyika kwa ubora unaostahili.
“Muda ambao unaoneshwa katika mkataba ni miezi
tisa, hatutapenda izidi hata siku moja. Tusingependa nyongeza ya muda, mabadiliko
ya gharama, tungependa msisitize na kusimamia kazi zenu ninyi wakandarasi na
washauri elekezi juu ya muda huu.
“Muda huu ndiyo Watanzania
wanasubiri katika Mikoa hii sita wapate huduma kwenye majengo haya katika ngazi
ya Mahakama Kuu. Naamini Wakandarasi hamtaniangusha na mtafanya kazi yenu
vizuri na kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa,” amesema.
Amewakumbusha wakandarasi
hao kuwa utekelezaji wa mikataba hiyo inafuatiliwa kwa karibu na wadau na Viongozi
wengi, akiwemo Mkuu wa Nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan na Mahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma.
“Hatutasita kumchukulia
hatua mkandarasi yoyote au mshauri elekezi yoyote au mtumishi yoyote wa
Mahakama atakayekuwa kikwazo katika kufanikisha malengo haya. Benki ya Dunia
pia nao wanafuatilia ambao ndio wametoa mkopo nafuu kwa kazi hii,” Prof. Ole
Gabriel amesema.
Mtendaji Mkuu amewatahadhalisha
kutokuingia kwenye mikataba bila kuwasiliana na mteja, yaani Mahakama ya Tanzania
na kuridhia kwa maandishi. Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wale watakaotaka
kuingia mikataba ya ziada na wakandarasi hao kuwa makini ili kuepuka changamoto
ambazo zinaweza kujitokeza.
Ameishukuru Serikali,
hususan Wizara ya Fedha chini ya Waziri Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, kwa kuanzia na Katibu Mkuu wa zamani Emanuel Tutuba na baadaye Dkt.
Natu Mwamba kwa kukubali kuondoa kodi kwenye gharama ya miradi hiyo ambayo imesaidia
kuongeza idadi ya majengo.
Amewaomba wakandarasi
wote kujitambulisha kwa viongozi wa Mikoa watakayokwenda kufanya kazi ili
wasionekane wageni kwani kazi wanayofanya ni kusogeza huduma za utoaji haki kwa
wananchi.
Kadhalika, amewasihi
wananchi katika maeneo ya miradi hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha ili
kuwawezesha wakandarasi hao kutekeleza majukumu hayo kikamilifu na kujiepusha
na uharibifu wa aina yoyote wakati wa kutekeleza miradi hiyo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha
Maboresho, akizungumza katika hafla hiyo, ameeleza kuwa jumla ya Vituo Jumuishi
vya Utoaji Haki 14 vinatakiwa kujengwa katika kipindi hiki, lakini mikataba
iliyosainiwa ni ya vituo sita.
Amesema mchakato wa kuwapata
wakandarasi ulikuwa wa wazi kwani jumla ya zabuni 142 zilinunuliwa na walibaki
wakandarasi wanne baada ya mchucho kufanyika ambao ndio wameitwa kusaini
mikataba ya ujenzi wa majengo hayo mapya.
Wakandarasi hao na Mikoa
wanayojenga kwenye mabano ni M/S Azhar Construction Company Limited Songea na
Katavi), M/S Shandong Hi-Speed Dejian Group Co. Ltd (Geita na Njombe), M/S Riha
Company Limited (Simiyu) na M/S Home Africa Investment Company Limited
(Songwe).
“Mchakato huu haukuwa
mwepesi na ulihitaji umakini ili kujiridhisha ili Mahakama ipate watu wenye
uwezo na wanaostahili kwenda na kasi ya Mahakama,” amesema na kumshukuru
Mkurugenzi wa Ugavi na Manunuzi na timu yake kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Amesema kuwa kutiwa saini
kwa mikataba hiyo ni kilele cha kazi ambayo imefanyika kwa kipindi cha zaidi ya
miaka miwili iliyopita na kwa kuzingatia muda mchache uliokuwepo watumishi hao
walifanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kazi inafanikiwa.
Ametumia nafasi hiyo kuupongeza
Uongozi wa Mahakama chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel na wote kwa kuwaunga mkono
ili kufanikisha kazi hiyo.
Ujenzi wa Vituo hivyo
utafanya Mahakama ya Tanzania kuwa na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki 12. Kwa
sasa kuna vituo sita ambavyo vinafanya kazi katika Mikoa ya Dar es Salaam,
Mwanza, Dodoma, Arusha na Morogoro.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza baada ya utiaji saini mikataba hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni