Ijumaa, 3 Novemba 2023

MAJAJI MAHAKAMA YA RUFANI WAKUNWA UTUNZAJI MAZINGIRA MAHAKAMA KUU MUSOMA

Na Francisca Swai, Mahakama – Musoma

Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania wapo mjini hapa kusikiliza jumla ya mashauri 32 ya rufaa katika kikao kinachofanyika Mahakama Kuu Musoma kwa muda wa siku 19 kuanzia tarehe 30 Octoba, 2023 hadi tarehe 19 Novemba, 2023.

Jopo hilo linajumuisha Mhe. Mwanaisha Kwariko (Mwenyekiti) na wajumbe wengine, Mhe. Zephrine Galeba na Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rashid Chaungu, katika mashauri 32 yanayoendelea kusikilizwa, 24 ni ya jinai na mashauri nane ya madai.

Pamoja na kuendelea na usikilizaji wa mashauri hayo, Majaji hao wamevutiwa na mandhari ya bustani nzuri iliyopo katika maeneo ya Mahakama Kuu Musoma, jambo lililopelekea kufanya ukaguzi na kujionea mazingira hayo.

Majaji hao wamepongeza juhudi zinazofanywa na Uongozi wa Mahakama Kuu Musoma kuhakikisha mazingira ya ndani na nje ya jengo yanakuwa katika hali ya usafi na ya kuvutia muda wote.

Wakipokea pongezi hizo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Festo Chonya na Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Erick Marley walisema utunzaji wa mazingira ni moja ya kipaumbele muhimu kwao.

Viongozi hao wameeleza kuwa licha ya uwepo wa changamoto za hali ya hewa bado jitihada kubwa na usimamizi wa karibu unafanywa kuhakikisha mandhari nzuri ya maeneo ya Mahakama yanakuwa hayapotei.

Katika ukaguzi huo Majaji hao walifanikiwa kuona miti iliyopandwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Mhe. Ferdinand Wambali, Mhe. Ignas Kitusi, Mhe. Zephrine Galeba, Mhe. Lilian Mashaka, Mhe. John Kahyoza, Mhe. Ephery Kisanya na Naibu Msajili, Mh. Mary Moyo.


Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mwanaisha Kwariko akifurahia matunda ya mti wa mwembe ulioko katika bustani ya Mahakama Kuu Musoma. Picha chini akiangalia mti wa mpera uliopandwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Ibrahim Juma katika bustani hiyo.

Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mwanaisha Kwariko (kushoto), Mhe.  Dkt. Paul Kihwelo (katikati) pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kulia) wakifurahia madhari na hewa safi katika bustani ya Mahakama Kuu Musoma.
Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Mwanaisha Kwariko (katikati) na Mhe.  Dtk. Paul Kihwelo (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kulia) kwenye picha ya juu. Picha chini wapo pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (wa kwanza kulia) na Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Erick Marley (wa kwanza kushoto) baada ya ukaguzi wa jengo na mazingira ya bustani Mahakama Kuu Musoma.



Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Festo Chonya (aliyenyoosha mkono) akiwa anawaelezea Majaji wa Mahakama ya Rufani namna shughuli za utunzaji wa jengo na bustani unavyofanywa. Picha chini wakiondoka kwenye bustani hiyo baada ya kujionea mazingira mazuri katika Mahakama hiyo.

Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Mwanaisha Kwariko (katikati) na Mhe.  Dtk. Paul Kihwelo (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Festo Chonya (wa kwanza kulia) na Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Erick Marley (wa kwanza kushoto) mbele ya jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Musoma.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni