Jumatano, 31 Januari 2024

JAJI MFAWIDHI TABORA AONGOZA WADAU KUTEMBELEA KITUO CHA WATOTO YATIMA IGAMBILO

Na Amani Mtinangi-Mahakama Kuu, Tabora

Baada ya kukamilika maonesho ya Wiki ya Sheria nchini,Wadau na watumishi wa Mahakama waliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi kutembelea kituo cha watoto yatima Igambilo kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Tabora. 

Baadhi ya wadau walioshiriki ni wawakilishi wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Jeshi la Polisi, Baraza la Usuluhishi na Uamuzi.

Wakati wa tukio hilo, Jaji Mambi alitoa pongezi kwa walezi wa kituo hicho na kuwashukuru  kwa juhudi alizofanya  kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao na malezi bora yanayotolewa kwa ujumla, huku akiwapa moyo watoto hao na kuwaasa kutokata tamaa katika kufikia ndoto zao.

“Ninawashukuru walezi kwa kwa juhudi mnazofanya za kuhakikisha watoto hawa wanapata mahitaji yao na kwa malezi bora mnayowapatia katika kituo hiki. Ninawaasa wanangu mfanye bidii kutimiza ndoto zenu bila kukata tamaa,” alisema Jaji Mfawidhi.

Aidha, watoto hao walikabidhiwa vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi yao ya kiafya na kielimu ambavyo vitawasaidia kwa sehemu kikidhi mahitaji yao. 

Naye mlezi wa watoto hao, Bi. Halima Malaswai aliwashukuru wadau wa Mahakama kwa ujio wao, faraja, kuwatia moyo na kwa vitu vwalivyokabidhi.

Aliwakaribisha kutembelea kituo hicho mara kwa mara ili kuona maendeleo ya watoto hao huku akitaja changamoto ya chombo cha usafiri kuwa ndiyo kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa.

“Hakika tunawashukuru kwa msaada wa vitu mlivyokuja navyo, ni faraja kwetu na kwa watoto hawa. Watoto hawa wanahitaji kufarijiwa, hivyo ninawaomba kututembelea mara kwa mara ili muone maendeleo ya watoto hawa…

“Pamoja shukrani hizi, changamoto yetu kubwa ni kukosekana kwa gari kwa ajili ya shughuli za kituo. Ninaomba kama atajitokeza mdau yeyote atayeweza kutusaidia gari ajitokeze ili kutusaidia,” alisema Bi. Halima Malaswai.

Ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2024.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, akisaini kitabu cha wageni cha kituo cha kulelea watoto Igambilo.


Mlezi wa watoto katika kituo cha Igambilo, Bi. Halima Malaswai akisema neno wakati wa ziara hiyo.

Mwenyekiti wa Baraza Usuluhishi na Uamuzi, Bi. Asnath Msaky (aliyesimama) ambaye ni mmojawapo wa wadau walioshiriki kutembelea kituo cha watoto yatima Igambilo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni