Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Mahakama ya Tanzania inaendesha mafunzo mkoani hapa kwa watumishi wake wanaotarajia kustaafu utumishi wao hivi karibuni.
Mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi ulioko ndani ya Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro yamefunguliwa leo tarehe 12 Februari, 2024 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kandaa ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wamafunzo hayo, Mhe. Mansoor alisema kuwa ni vyema washiriki wakazingatia kikamilifu mada zitakazotolewa na wawezeshaji.
Amewaomba kuwa na moyo wa kujifunza na kukubali kubadilika ili kuyakabili maisha mapya kwa kuwa hatua hiyo ni muhimu katika safari maishani.
“Mnapojitayarisha kuingia katika mazingira mapya ya maisha ni vyema kutafakari na kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza, hivyo ni imani yangu kuwa mafunzo haya yatawajenga na kuwasaidia kupata mbinu za kukabiliana na changamoto hizo,” alisema Mhe. Mansoor.
Aidha, Jaji Mansoor alitoa pongezi zake kwa watumishi hao ambao kupitia michango yao mikubwa wameiwezesha Mahakama ya Tanzania kuendelea kutoa haki kwa wananchi kwa ubora, jambo lililopelekea kuendelea kujenga imani ya wananchi kwa Muhimili wa Mahakama.
“Kwa kutambua mchango wenu mkubwa Mahakama imeona umuhimu wa kuandaa mafunzo haya ili kujiandaa kutoka kwenye ajira rasmi na kwenda kwenye sekta isiyo rasmi, pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwezesha jambo hili,” alisema.
Awali wakati akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu alisema kuwa miongoni mwa mada zitakazofundishwa ni pamoja na Bima ya Afya baada ya kustaafu kazi, Mbinu za Ujasiliamali, Biashara na Kujikimu kabla, wakati na baada ya kustaafu kazi, Uwezekaji katika mifumo mbalimbali, Menejimenti ya mafao ya hitimisho la ajira na ushughulikiaji sahihi wa mirathi ya watumishi.
Mafunzo haya ambayo yatatolewa kwa siku sita kuanzia hadi tarehe 17 Februari, 2024 yamelengwa kuwafikia jumla ya washiriki 119 ambao kati yao kundi la kwanza lililoanza mafunzo lina jumla ya washiriki 62 ambao watahitimu tarehe 14 Februari, 2024 kupisha kundi la pili lenye washiriki 59 ambao wataanza tarehe 15 hadi tarehe 17 Februari,2024.
Washiriki wote wanatoka sehemu mbalimbali za Mahakama ya Tanzania na wanategemea kustaafu utumishi wao wa umma kuanzia mwezi Februari hadi mwezi Julai 2024.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu akizungumza wakati akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo ya kujiandaa kustaafu kwa watumishi wa Mahakama.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Fadhili Mbelwa akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Sehemu ya washiri wa mafunzo ya kujianda kustaafu utumishi wa Mahakama (juu na chini) wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.
Meza Kuu wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, ikiongozwa na mgeni rasmi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor (katikati), kushoto kwake ni Naibu Msajili, Mhe. Fadhili Mbelwa kutoka Kanda ya Morogoro na kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu katika picha ya pamoja.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya mafunzo ya kujiandaa kustaafu utumishi wa Mahakama.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mafunzo ya kujianzaa kustaafu utumishi wa Mahakama (juu na chini).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni