Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Ikiwa ni siku ya pili tangu kufunguliwa kwa mafunzo wezeshi kwa watumishi wa Mahakama wanaotarajia kustaafu kazi hivi karibuni, leo tarehe 13 Februari, 2024 watumishi hao wamepewa elimu juu ya umuhimu wa mifuko ya hifadhi za jamii.
Elimu hiyo imetolewa na wawezeshaji toka Mifuko ya PSSF na NSSF ambao walipata wasaa wa kuwaelimisha washiriki wa mafunzo mambo mbalimbali ya kuzingatia na namna inavyofanya kazi kabla na baada ya kustaafu kwa mtumishi.
Akitoa elimu, Meneja Mafao toka NSSF, Bw. James Oigo alihimiza kuwa ni vyema watumishi kuwa na mipango bora ya uwekezaji itakayowasaidi kuzalisha kipato mara baada ya kustaafu kwa kuwa mipango mibovu hupelekea mstaafu kuwa na msogo wa mawazo ambao ni chanzo cha magonjwa.
Naye Mwezeshaji toka PSSF, Bw. Charles Mahanga alieleza umuhimu wa maandalizi kabla ya kustaafu kazi ambapo aligusia kuwa kila mtumishi anapaswa kujiandaa kiuchumi, kisaikolojia, kijamii na kiafya.
Akaendelea kusisitiza kuwa maandalizi hayo yatawasaidia mara baada ya ukomo wao katika utumishi wa umma.
Sanjari na hilo, watumishi hao pia walipata nafasi ya kujifunza kuhusu kikokotoo kipya na namna kinavyofanya kazi yake, huku wakielekezwa kwa mifano juu ya sababu zinazopelekea watumishi wanapostaafu kuwa na kiwango tofauti cha mafao licha ya kuwa wote wamestaafu katika cheo na ngazi ya mshahara mmoja.
Mwezeshaji alitaja miongoni mwa sababu kubwa ni umri wa mtumishi ndani ya ajira. Upande huo wa kikokotoo uliibua maswali kadhaa ambayo yalitolewa ufafanuzi yakinifu na wawezeshaji.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwenda kwa watumishi wake wanaotarajiwa kustaafu kuanzia mwezi Februari hadi Juni 2024. Kundi la kwanza la washiriki linategemewa kuhitimisha hapo kesho tarehe 14 Februari, 2024 kupisha kundi la pili ambalo litaenda mapaka tarehe 17 Februari, 2024.
Meneja Mafao toka NSSF, Bw. James Oigo akitoa somo la uwekezaji kwa washiriki (hawapo pichani).
Mwezeshaji toka PSSF, Bw. Charles Mahanga akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo ya kujiandaa kustaafu kwa watumishi wa Mahakama wanaotarajia kustaafu hivi karibuni (hawapo pichani).
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mafunzo (juu na picha mili chini).
Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo toka Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu (kushoto) na Afisa Utumishi toka Mahakama ya Tanzania, Bi. Sharifa Mbaraka (kulia) wakifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa wakati wa mafunzo ya watumishi wa Mahakama wanaotogemea kustaafu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo toka Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu akisalimiana na wawezeshaji.
Picha ya pamoja ya wawezeshaji kutoka mifuko ya hifadhi za jamii walioshiriki kutoa mada katika mafunzo ya watumishi wanaojiandaa kustaafu.
Bw. Dornard Makawia toka Mahakama ya Tanzania ambaye ni sehemu ya sekretarieti ya mafunzo akinakili pointi muhimu wakati mada ya mafao ikiwasilishwa.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni