Jumatano, 14 Februari 2024

MAHAKAMA NJOMBE YAMALIZA MASHAURI YA MUDA MREFU

Na Abdallah Salum, Mahakama-Njombe

Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemaliza jumla ya mashauri mawili (2) ya muda mrefu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe katika kikao maalum kilichofanyika mkoani humo.

Kikao cha kusikiliza mashauri hayo kiliongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta ambapo zoezi la usikilizwaji wa mashauri hayo lilihitimishwa jana tarehe 13 Februari, 2024. Moja ya mashauri hayo lilikuwa la mwaka 2019 na lingine la mwaka 2021.

Baada ya kikao hicho, Mhe. Mugeta akiongozwa na Kaimu Hakimu Mkazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe alipata wasaa wa kukutana na kuzungumza na watumishi wa Mahakama hiyo kwa lengo la kufahamu changamoto zinazowakabili na kuwaaga baada ya kumaliza kikao cha usikilizwaji wa mashauri.

Katika kikao hicho, watumishi walimueleza Jaji Mfawidhi kuwa wanakabiliwa na uchache wa watumishi haswa kwenye Kada ya Usaidizi wa Ofisi hivyo wameomba kuongezewa watumishi hao kutokana na uchache wao.

Mhe. Mugeta amewasihi watumishi wa Mahakama Mkoa wa Njombe kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu na kuwatakia heri katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amewashukuru watumishi wa Mahakama hiyo katika kipindi chote alichokuwa hapo na kusema kuwa, tangu amefika Njombe ambapo amekaa kwa takribani wiki mbili hakusikia wala kupata changamoto au malalamiko yoyote katika utendaji kazi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta (aliyeketi) akiwasikiliza watumishi ambao (hawapo katika picha). Kushoto aliyesimama ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Matilda Kayombo.

Mtumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Siza Nambasi akiwasilisha jambo mbele ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta (hayupo katika picha).

Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Njombe wakiwa kwenye kikao pamoja na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta (hayupo katika picha).

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni