Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Baada ya kundi la kwanza la watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuhitimu mafunzo ya kujiandaa kustaafu, kundi la pili limeanza mafunzo hayo leo tarehe 15 Februari, 2024.
Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Mahakama ya Tanzania yamelenga kuwaandaa watumishi hao kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya wao kustaafu, mbinu za kuweka hakiba, mipango na matumizi ya pensheni ya kustaafu pamoja na mbinu za ujasiliamali.
Akizungumza na kundi hili, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu alisema kuwa ni vyema watumishi hao watakapostaafu kazi wawe na maamuzi ya utulivu ili waweze kufanya vitu sahihi vitakavyowaleta matokeo chanya.
“Inasikitisha sana kusikia taarifa za mstaafu ameishia pabaya kana kwamba hakuwahi kuwa mtumishi wa umma,” alieleza Bi. Ngungulu na kutaadhalisha juu ya matapeli ambao kuanzia sasa wanawawinda ili waweze kunyakua mafao yao.
Alibainisha kuwa matapeli hao wengi hujifanya kuwa wanatokea ofisi za mifuko ya hifadhi ya jamii na pia hata wengine husingizia kuwa wanatokea katika taasisi ambazo mstaafu alikuwa anatumikia kabla ya kustaafu.
“Kama mtapokea simu yoyote yenye taarifa zinazohusu mafao yenu muwe makini, msipuuzie isipokuwa mfatilie kwa kina, ofisi mlizofanyia kazi zipo wazi, kama kuna mtu anawapigia simu kuhusu taarifa zozote tafadhali muwasiliane na ofisi zenu zitawasaidia,” alisisitiza.
Wakati wa mafunzo, kundi hili la pili lilianza na mada iliyogusia stahiki za mtumishi anapofikia ukomo wake kazini.
Mada hiyo ilitolewa na Afisa Utumishi, ambaye huwa anashughulika ma masuala ya mafao ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Sharifa Mbaraka. Katika mada yake, Bi. Sharifa alifundisha jinsi ambavyo mtumishi anapaswa kuwasilisha nyaraka zake mapema ili mafao na nauli ziweze kulipwa mapema.
Kundi hili la pili linategemewa kuhitimisha mafunzo hayo tarehe 17 Februari, 2024, wakati kundi lililopita lilihitimisha kwa kupata mawaidha kutoka kwa Viongozi wa dini ambao walifanya maombi maalumu kwa watarajiwa wa kustaafu hao na kuwaasa kutumia hekima waliyonayo kwenye nyumba za idaba.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu (juu na chini) akizungumza na kundi la pili la watumishi muda mfupi kabla ya kuanza kwa mafunzo ya kujiandaa kustaafu.
Mwezeshaji toka Mahakama ya Tanzania, Bi. Sharifa Mbaraka akitoa mada kwa washiriki hao (hawapo pichani).
Mwezeshaji toka Mahakama ya Tanzania, Bi. Sharifa Mbaraka (aliyesimama mbele) akisikiliza kwa makini madukuduku yaliyokuwa yanawasilishwa na washiriki.
Washiriki wa awamu ya pili wakifuatilia mada toka kwa muwezeshaji.
Watumishi wa Mungu (juu na chini) wakitoa mawaidha kwa washiriki wa mafunzo awamu ya kwanza waliohitimisha hapo jana tarehe 14 Februari, 2024.
Washiriki wa mafunzo awamu ya kwanza wakipokea maombi maalumu toka kwa mtumishi wa Mungu.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, DAR ES SALAAM)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni