Jumatatu, 19 Februari 2024

MAFUNZO KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA WANAOJIANDAA KUSTAAFU YAHITIMISHWA

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Mafunzo kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania wanaotarajiwa kustaafu utumishi wao hivi karibuni yaliyokuwa yanafanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro yamehitimishwa siku ya Jumamosi tarehe 17 Februari, 2024.

 

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa tarehe 12 Februari, 2024 yaliendeshwa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza lilihitimu tarehe 14 Februari, 2024. Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma ndiye aliyehitimisha mafunzo hayo.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Mruma alitoa pongezi kwa uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kubuni mafunzo hayo wezeshi na kuomba yawe endelevu na yasiishie kwa wastaafu pekee.

 

Alisema kuwa ni vyema mafunzo kama hayo yakawafika pia watumishi wengine ili waweze kujiandaa na kuwekeza kiuchumi pasipo kungojea fedha za mafao pindi atakapostaafu.

 

“Wengi wenu mnastaafu hivi karubuni lakini bado mnaonekana kuwa na nguvu nyingi, ni dhahiri kuwa mlezi wetu ambaye ni Mahakama alitulea vyema, rai yangu tukawe wana jamii wema. Naamini ni wakati muafaka mnaenda kuzalisha mali zaidi ya mlizonazo sasa, kwani kustaafu kazi ni mwanzo wa maisha mengine mapya,” alieleza Mhe. Mruma.

 

Aidha, Jaji Mruma aliwasihi watumishi hao kutumia vizuri muda waliobakiza kazini kuendelea kuwa na mahusiano mema na Viongozi wao na watumishi na kujiepusha kukwaruzana pasipokuwa na sababu za msingi.

 

“Hongereni kwa hatua hii muhimu katika maisha, siku tulizobakiza tuzitumie vizuri na muajiri wetu Mahakama, kustaafu sio kitu cha kukatisha tamaa bali tuwe na furaha mpya na tukikutana tuweze kusalimiana,” alisema.

 

Naye mratibu wa Mafunzo toka Mahakama ya Tanzania, Bw. Dornard Makawia alieleza kuwa jumla ya watumishi 121 wamepatiwa mafunzo hayo toka kwa wawezeshaji mbalimbali kutoka Mifuko ya Jamii ya PSSF na NSSF.

 

Pia alikuwepo Daktari wa Saikolojia toka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwezeshaji kutoa UTT, Wajasiliamali sambamba na watumishi wa Mungu.

Aliongeza kuwa jumla ya mada 11 zimefundishwa, hivyo ni imani ya waandaaji wa mafunzo hayo kuwa washiriki wameshiba madini ya kutosha.

 

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo walipata wasaa wa kutoa neno la shukurani kwa uongozi wa Mahakama kwa kuwapatia mafunzo hayo.

 

Hakimu Mkazi, Mhe. Hamis Makalala alisema, “Tunashukuru sana kwa mafunzo haya kwani yametutoa hofu tuliyokuja nayo, tulikuwa tunawaza sasa itakuwaje kuhusu maisha mapya tunayoenda kuyaanza, hofu ya kikokotoo,” alisema.

 

Alibainisha, hata hivyo, kuwa baada ya kupata mafunzo hayo wamekuwa wapya na wapo tayari kustaafu muda wowote.



Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir Mruma akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya watumishi wa Mahakama wanaojiandaa kustaafu hivi karibuni(hawapo pichani).

 


Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Asha Waziri akitoa neno la pongezi kwa washiriki wa mafunzo (hawapo pichani) muda mfupi kabla hajamkaribisha Kaimu Jaji Mfawidhi kufunga mafunzo hayo.


 


Mshiriki wa Mafunzo, Mhe. Hamis Makalala akitoa neo la shukurani kwa uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwapatia mafunzo hayo.

 


Meza Kuu ikiongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Amir. Mruma (aliyekaa katikati) kulia kwake ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Asha Waziri na kushoto kwake ni Mratibu wa Mafunzo toka Mahakama ya Tanzania, Bw. Dornard Makawia wakati wa kufunga mafunzo kwa watumishi wa Mahakama wanaojiandaa kustaafu.


 

Meza Kuu ikiongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Amir. Mruma (aliyekaa katikati) katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo (juu na picha mili chini).




(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni