• Wasema Mradi wa Mahakama ni miongoni mwa Miradi inayofanya vizuri
Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) leo tarehe 19 Februari, 2024 umeanza ziara ya kufanya tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki hiyo.
Akizungumza leo wakati akifungua kikao kati ya Ujumbe huo na wa Mahakama ya Tanzania katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa, lengo la ziara hiyo ni pamoja na kutembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wa Mahakama inayogharamiwa fedha za mkopo za Benki hiyo.
“Leo tarehe 19 Februari, 2024 tumepata bahati ya kutembelewa na ujumbe wa Benki ya Dunia na miongoni mwa mambo watakayofanya ni pamoja kutembelea miradi ya ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Mahakama ambavyo ujenzi wake unatokana na mkopo wa awamu ya pili kutoka Benki hiyo,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Mtendaji Mkuu ametumia fursa hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Fedha kwa kuiwezesha Mahakama kupata mkopo wa Dola milioni 90 kutoka Benki ya Dunia unaowezesha Mahakama kufanya maboresho mbalimbali ya huduma zake. Amepongeza pia Uongozi wa Jaji Mkuu wa Tanzania unaosimamia kwa dhati utekelezaji wa maboresho mbalimbali ya Mahakama.
Kadhalika, Mtendaji Mkuu amesema kuwa kupitia mradi huo, Mahakama imepanga kuwa na Vituo Jumuishi nchi nzima ambapo kwa sasa amesema ujenzi wa Vituo Jumuishi tisa unaendelea na mpango uliopo ni kujenga Kituo hicho visiwani Pemba.
Naye, Kiongozi Mwenza wa Ujumbe wa Benki ya Dunia ambaye pia ni Afisa Mwandamizi kutoka Benki hiyo, Bw. Benjamin Mtesigwa amepongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania na kukiri kuwa, Mradi unaotekelezwa na Mhimili huo ni moja ya Miradi inayofanya vizuri.
“Niseme tu kwa kumbukumbu tulizo nazo Benki ya Dunia, Mradi huu ni moja kati ya Miradi inayofanya vizuri sana, kama Benki ya Dunia tunaridhishwa na utekelezaji wa huu Mradi kwa hivyo tunaamini kuwa katika ziara hii tutakutana na mafanikio mengi zaidi ambayo yataendelea kudhihirisha hili,” amesema Bw. Mtesigwa.
Amesema kuwa, Benki ya Dunia itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa Mradi huo unaendelea kuwa Mradi bora.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour amesema kuwa lengo la ziara yao ni kufahamu maendeleo ya Mradi pamoja na kuona kama makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ujumbe uliopita kama yametekelezwa.
“Tunafanya ziara kama hii mara kwa mara lengo ni kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa kazi mbalimbali za Mradi pamoja na utekelezaji wa makubaliano ya ziara iliyopita,” amesema Bi. Christine.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amesema maboresho ya huduma za Mahakama yanamlenga mwananchi kwa asilimia kubwa.
“Katika utekelezaji wa mradi hii tumejikitika katika kuboresha maeneo makuu nane (8) ambayo ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, kuboresha ushirikishwaji wa wadau kuongeza miundombinu ya majengo ya Mahakama na mengine,” amesema Mhe. Dkt. Rumisha.
Akitoa mfano kuhusu ushirikishwaji wa wananchi, Mkuu huyo amesema kuwa kwa mujibu wa Ripoti iliyofanywa na 'REPOA' mwaka 2023 asimilia 88 ya wananchi wanaridhishwa na huduma zinazolewa na Mahakama, kiwango hicho kimepanda kutoka asilimia 78 kwa mwaka 2019.
“Malengo yetu Mahakama ilikuwa ni kuwaridhisha wananchi kwa asilimia 82 lakini ukiangalia kiwango cha kuridhika kimepanda nah ii inatokana na uboreshaji wa huduma za Mahakama unaoendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupunguza hatua/vituo vya shauri mahakamani, kupungua idadi ya siku za shauri kukaa mahakamani na kadhalika,” amesisitiza.
Akizungumzia kuhusu miradi ya ujenzi amesema, lengo la Mahakama ni kuwa na huduma za Mahakama Kuu nchi nzima ili kumpunguzia mwananchi aza za kutafuta haki kwa umbali mrefu. Amesema kwa sasa Vituo Jumuishi vinajengwa katika mikoa tisa ambayo ni Geita, Simiyu, Njombe, Katavi, Songwe, Lindi, Singida, Songea na Pemba.
Katika ziara yao ya wiki moja miongoni mwa shughuli zitakazofanywa na Ujumbe huo ni pamoja na kutembelea baadhi miradi ya ujenzi wa Vituo Jumuishi ikiwemo Geita na Simiyu na mwisho tarehe 24 Februari, 2024 watahitimisha kwa kufanya majumuisho katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni