Jumatatu, 26 Februari 2024

JAJI MKUU ASISITIZA UTOAJI HAKI BILA KUYUMBISHWA

Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wote nchini kutoa haki kwa kuzingatia mizani ya haki bila kuyumbishwa na mitazamo inayotolewa na watu baada ya hukumu kusomwa.

Mhe. Prof. Juma ameyasema hayo leo tarehe 26 Februari, 2024 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo pia ametoa rai kwa watu wasioridhishwa na maamuzi yanayotolewa kukata rufaa kwa kuwa ni haki yao.

“Moja ya kazi za Majaji Wafawidhi ni kusimamia eneo la utoaji haki, na haki sio ushindi bali ni ushahidi unaotolewa kwa kuangalia mizani ya haki hivyo msikatishwe tamaa na wanaopinga maamuzi yanayotolewa,” amesema Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Prof. Juma amewakumbusha Majaji hao kusimamia haki kwa kuhakikisha kuwa wanasoma taarifa mbalimbali zinazowasilishwa kwao ili kutatua changamoto zinazojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi.

“Mnatakiwa kusimamia utoaji haki sio kuwa sehemu ya malalamiko au kukaa na kusubiri taarifa za viongozi wanaowasaidia, mfano Wasajili, Watendaji na Mahakimu Wafawidhi, lazima unapopokea taarifa, ni muhimu utafute changamoto zilizojificha ambazo wewe kiongozi mkuu wa Kanda au Divisheni unatakiwa kuzifahamu na kuzitafutia ufumbuzi,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Pamoja na hayo, Mhe. Prof. Juma hakusita kuwakumbusha Majaji Wafawidhi kuhusu matumizi ya TEHAMA hususani katika kipindi hiki ambacho Mahakama ipo kwenye safari ya kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.

“Matumizi ya Teknolojia ni eneo la msisitizo ambalo uwekezaji mkubwa umefanywa. Ni wajibu wetu Viongozi kuhakikisha kuwa, miundombinu yote ya TEHAMA na vifaa vilivyofungwa vinatumika kuleta manufaa makubwa na kutusaidia kuifikisha Mahakama katika hadhi ya Mahakama Mtandao,” ameeleza Mhe. Prof. Juma.

Ameongeza kwamba, matumizi ya Teknolojia ndio nyenzo ya karne ya 21 ya kuleta matokeo makubwa ya kusogeza huduma za haki zilizo bora, hivyo Taaluma ya Sheria na Mifumo ya utoaji haki haiwezi kukwepa mapinduzi makubwa yanayotokana na Teknolojia kukua kwa kasi.

Amewasihi Majaji hao kuwa sehemu ya safari ya Mahakama ya Tanzania inayolenga kutumia mifumo ya teknolojia kudijiti nyaraka zote za Mahakama ili kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji huduma.

Ametaja faida kadhaa zitakazopatikana endapo Mahakama itadijiti nyaraka zake, ambazo ni pamoja na kuondoa changamoto za nyaraka kutoonekana kwa kuhakikisha kuwa nyaraka zote zinatunzwa katika mifumo ya kielektroniki, kuimarisha ufanisi katika hatua za kimahakama zinazopitiwa hadi haki kupatikana.

Faida nyingine ni kuimarisha upatikanaji wa taarifa muhimu za mashauri ya wadau, Majaji, Mahakimu, Wanasheria, Wadaawa na wananchi kwa ujumla, kuongeza uwazi kwa kuweka kumbukumbu kuhusu usajili wa mashauri, amri na maamuzi mbalimbali yanayotolewa, kuongeza uwajibikaji pamoja na kuiwezesha Mahakama kukusanya na kuchambua takwimu kuhusu mashauri.

Kadhalika amewataka, Majaji hao kuwatumia Maafisa TEHAMA kikamilifu ili kutoa suluhisho ya changamoto mbalimbali za Mifumo ya Kieletroniki inayotumika mahakamani ikiwemo Mfumo wa Kieletroniki ya Usimamizi wa Mashauri (e-CMS), Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) na mingine.

Akizungumzia kuhusu Mfumo wa ‘e-CMS’ Jaji Mkuu amewataka Majaji hao kuendelea kuutumia na kubaini changamoto zinazohusiana na Mfumo huo. Hata hivyo amesema amepata changamoto na mapendekezo kuhusu Mfumo huo kutoka kwa Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza. 

“Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza, alipendekeza suluhisho katika changamoto za Mfumo wa ‘e-CMS’, ambapo amependekeza Wataalamu wa Mahakama wafuatilie kwa karibu na kwa haraka uwezekano wa kuongezewa uwezo wa kuhifadhi ‘data’,” ameeleza Jaji Mkuu.

Mkutano huo wa siku tatu (3) ambao umeshirikisha Majaji Wafawidhi wote nchini pamoja na Majaji kadhaa wa Mahakama Kuu ya Tanzania unalenga kukumbushana na kubadilishana uzoefu kuhusu majukumu ya Majaji hao na nafasi zao katika maboresho ya Mahakama na kupitia maboresho ya Mhimili huo ili kufanikisha ustawi wa wananchi kwa ujumla.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji kadhaa wa Mahakama hiyo (hawapo katika picha) wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Majaji hao leo tarehe 26 Februari, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.


Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Majaji Wafawidhi ulioanza leo tarehe 26 Februari, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.


Picha mbalimbali zikiwaonesha Majaji Wafawidhi na washiriki wengine wa Mkutano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi iliyokuwa ikitolewa na Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Majaji hao unaofanyika katika Ukumbi wa hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi unaofanyika jijini Arusha. Kushoto ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga.
Meza kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji Wafawidhi kutoka Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania. Aliyeketi katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kushoto ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga.
Meza kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaoshiriki katika mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi. 
 
Meza kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama wa sita kushoto). Walioketi katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kushoto ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga.

(Picha na Seth Kazimoto, Mahakama-Arusha)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni