Jumatano, 28 Februari 2024

MABORESHO MAHAKAMANI YATAMALAKI

Na Seth Kazimoto – Mahakama Arusha

Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, Mhe. Jaji Dkt. Angelo Rumisha amesema kuwa Mhimili huo umefanya maboresho makubwa katika suala zima la utoaji haki ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. 

Mhe. Rumisha aliyasema hayo jana tarehe 27 Februari, 2024 ikiwa ni siku ya pili ya mkutano wa Majaji Wafawidhi unaoendelea katika Hoteli ya ‘Mount Meru’ jijini Arusha.

Akiwasilisha mada inayohusu maboresho yaliyofanyika mahakamani, Mhe. Rumisha amegusia maeneo mbalimbali ambayo ufanisi mkubwa umeonekana ikiwa ni pamoja na muda unaotumika kumaliza shauri kiwango cha mashauri kinachosikilizwa na kuisha mahakamani, imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa na Mahakama, mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau wake na suala la uwazi kwa huduma za Mahakama.

Akizungumzia suala la muda unaotumika kuanzia kusajili hadi kumaliza shauri, Mhe. Dkt. Rumisha amesema Mahakama imefanikiwa kupunguza siku za kumaliza shauri kutoka wastani wa siku 827 mwaka 2020 hadi kufikia siku 231 mwaka 2023.

Dkt. Rumisha ameeleza kuwa matokeo yatokanayo na kupungua muda wa kusikiliza mashauri ni pamoja na ongezeko kubwa la mashauri yanayomalizika mahakamani kutoka asilimia 60 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 83 kwa mwaka 2023.

Vilevile, Jaji Rumisha amesema kuwa kupungua kwa muda wa mashauri mahakamani kumeongeza imani ya wananchi kwa Mahakama kutoka asilimia 78 kwa mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 88 kwa mwaka 2023. 

“Kumekuwa pia na ongezeko kubwa la mafunzo kwa watumishi na wadau wa Mahakama ili kuwaongezea ujuzi na maarifa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi. Kwa mfano, kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2023, jumla ya watumishi na wadau 2,317 wamepatiwa mafunzo,” alieleza Mhe. Dkt. Rumisha.

Ameongeza kwamba, uwazi katika utendaji kazi wa Mahakama umeboreshwa, upandishwaji wa maamuzi katika mfumo wa Tanzlii nao umevuka lengo ambapo ameeleza kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2023, asilimia 54 ya maamuzi yalipandishwa katika mfumo wa kielektroniki wa Tanzlii na idadi ya watu wanaotembelea mfumo huo imeongezeka. Amebainisha kuwa, kati ya watu 153,901 waliotembelea mtandao wa Mahakama, 122,276 walikuwa watumiaji wa mfumo wa TanzLII.

Kadhalika, amebainisha kuwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi wanaopata huduma za Mahakama Kuu kutoka asilimia 52 kwa mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 84 kwa mwaka 2023. 

Kadhalika, Mhe. Dkt. Rumisha amesema kuwa Mahakama inalenga kuimarisha ushirikiano na Wadau na mikakati ya kuzuia mashauri mlundikano pamoja na kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa Mahakama.


 Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akiwasilisha mada ya Maboresho mahakamani katika Mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akiongoza majadiliano katika Mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania unaoendelea jijini Arusha.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akichangia mada katika Mkutano wa Majaji Wafawidhi unaoendelea jijini Arusha.

 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim akichangia mada.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza jambo katika mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda akichangia mada.
 
Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akichangia jambo wakati wa Mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha akichangia mada katika mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania unaoendelea jijini Arusha. Kulia ni Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji, Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso.
Mtendaji Mahakama Kuu-Divisheni, Bi. Mary Shirima akichangia jambo wakati wa mkutano wa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Mahakma ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni