Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amewataka Majaji Wafawidhi nchini kusimamia ipasavyo utekelezaji wa amri na tuzo za Mahakama.
Mhe. Siyani ameyasema hayo leo tarehe 28 Februari, 2024 wakati akifunga mkutano wa mwaka wa Majaji hao katika Hoteli ya ‘Mount’ Meru jijini Arusha.
"Changamoto ya ucheleweshwaji katika utekelezaji wa amri na tuzo za Mahakama kama ilivyo kwa usikilizaji wa mashauri ya kifamilia hususani mirathi ni maeneo ya kufanyia kazi,” amesema Jaji Kiongozi.
Amewataka Viongozi hao kukumbuka kuwa, wale wanaokuja mahakamani, hawaji kutafuta karatasi ya hukumu bali wanataka kupata kilichoamuliwa.
“Mathalani, kama mtu ametambuliwa kuwa mmiliki wa nyumba, anachotarajia ni kukabidhiwa nyumba yake. Vinginevyo tamko tu la kwamba yeye ni mmiliki wa nyumba na kisha asipewe nyumba yenyewe halina faida kwake,” amesema Mhe. Siyani.
Amewakumbusha kuzingatia msisitizo uliowekwa na Jaji Mkuu katika hotuba yake ya ufunguzi kwamba, kama Viongozi hawapaswi kuwa walalamikaji au watu wa kulaumu bali wajibu wao ni kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
“Na mimi nitumie fursa hii kuwakumbusha; kwa kuwa sisi ndio wasimamizi wa Mahakama katika maeneo yetu, ni wajibu wetu kuhakikisha kasi ya umalizaji na uondoshaji wa mashauri ya aina zote, inaendelea kuongezeka katika Mahakama zote ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” ameeleza Mhe. Siyani.
Akizungumzia matumizi ya TEHAMA, Jaji Kiongozi amewasihi Majaji hao kutorudi nyuma katika matumizi ya mtandao kwakuwa azma ya Mahakama ni kuwa Mahakama mtandao ‘e-Judiciary’.
“Ningependa kuwakumbusha juu umuhimu wenu kwa Taasisi yetu hasa wakati huu ambao Mahakama inafanya maboresho makubwa ya kimifumo katika utoaji wa huduma zake. Ningependa mfahamu, kwa kuwa ninyi ndio viongozi wa Mahakama katika Kanda na Divisheni zetu. Kufanikiwa au kutofanikiwa kwetu kutategemea sana utendaji wenu, nini mnafanya au nini hamfanyi katika kutimiza majukumu yenu, vitaamua hatma ya Mahakama na mchango wake katika kuwaletea maendeleo” amesema Jaji Kiongozi.
Amesisitiza kuwa, suala hilo halikwepeki kwa sababu katika karne hii, hakuna Taasisi yoyote, itakayofanikiwa kutoa huduma bora za viwango vya zama hizi bila TEHAMA hivyo, Mahakama haiwezi kuwa nyuma.
Kikao cha Majaji Wafawidhi cha siku tatu (3) kimehitimishwa leo na kutoka na maazimio mawili nayo ni pamoja na Miundombinu ya mifumo ya TEHAMA ikaguliwe katika Mahakama zote na kuboreshwa ili ikidhi mahitaji ya sasa ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA, hasa mfumo mama wa Usimamizi wa Mashauri e-CMS na 'MPBS' zitolewe kwa usawa kwa Mahakama zote au izingatie ngazi za Mahakama zenye mzigo mkubwa wa mashauri.
Ili kuboresha utendaji wa mfumo wa 'e-CMS' kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana kutoka kwa watumiaji, iundwe timu itakayojumuisha Majaji wafawidhi watatu, ipitie mfumo kwa kufanya mazoezi halisi ya utendaji wa mfumo kwa kila hatua ya kesi na itoe mapendekezo ya maboresho baada ya kuwashirikisha Majaji Wafawidhi.
Azimio lingine ni kuimarishwa kwa Mfumo wa malezi kitaaluma (mentorship) na uanze kutumika nchi nzima.
Mada zilizotolewa katika Mkutano huo ni pamoja na utekelezaji wa maboresho ya huduma za Mahakama, malezi ya kitaaluma, namna bora ya kukabiliana na mabadiliko (change management), majukumu ya Majaji Wafawidhi katika usimamizi wa shughuli za Mahakama na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo (stress management).
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. joachim Tiganga akitoa neno la shukrani kabla ya kumkaribisha Jaji Kiongozi kufunga mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu walioshiriki katika mkutano wa mwaka wa Majaji Wafawidhi wakimsikiliza kwa makini Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa neno wakati wa kufunga mkutano huo. Aliyeketi nyuma ya Majaji watatu ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni