Na Lydia Churi na Seth Kazimoto- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Arusha
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wadau wote kwenye mnyororo
wa utoaji haki kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao ili kutenda haki kwa
wananchi.
Akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo watakaokuwa Wakufunzi wa
Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ambayo yanawalenga
Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu zikiwemo Divisheni za Mahakama Kuu na Kituo
cha Usuluhishi, Jaji Mkuu amesema wadau wa utoaji haki wakikosa uadilifu,
Mahakama ndiyo hulaumiwa kwa kutokutenda haki.
”Kama walivyo Majaji, Wasajili, Mahakimu na watumishi
wengine wa Mahakama; Wapelelezi, Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Serikali na wa
Kujitegemea, Madalali wa Mahakama, na Wasambaza Nyaraka, wanatakiwa kuwa na
sifa ya uadilifu, weledi, uwajibikaji, kuaminika, na kutegemewa kuwa watatenda haki”
alisema Jaji Mkuu.
Aliwataka wadau katika mnyororo wa utoaji haki kusimamia
kanuni zao za maadili na kuchukuliana hatua wao wenyewe wanapokiuka maadili
yao. Aidha Jaji Mkuu pia aliwataka wananchi kuwa waadilifu.
”Kwa mfano Mwananchi ana kesi inayoendelea mahakamani, au
anayo nafasi ya kukata rufani- lakini ataandika barua kwa Mhe. Rais, Jaji Mkuu
au Jaji Kiongozi kuwaomba “waingilie kati”. Maombi ya aina hii ni uvunjifu wa
maadili” alisema.
Aidha, Jaji Mkuu
amewataka Wanahabari nchini kutoa kwa usahihi taarifa zinazohusu Mhimili wa Mahakama
kwa kuhusisha pande zote mbili ili kutenda haki badala ya kutoa taarifa
zinazoegemea upande mmoja. Alisema ni muhimu jamii ikaelimishwa kuwa wao ni
sehemu ya kujenga maadili kwa Maafisa Mahakama kwa kuepuka kuwashawishi kuvunja
maadili kwa kutoa uamuzi kwa upendeleo.
Akizungumzia mafunzo hayo, Jaji Mkuu alisema jitihada za
Tume kutoa mafunzo hayo ni kielelezo dhahiri na dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa suala la maadili, uadilifu
na uwajibikaji linaeleweka katika ngazi zote za Mahakama na Kamati za Maadili
za Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ili uelewa huo ukatumike kuendelea kulinda heshima ya Mahakama.
Alisema
Majaji Wafawidhi ni kiungo muhimu kinachowakilisha uongozi wa Mahakama, na pia
Tume katika usimamizi imara wa maadili ya watumishi na Maafisa-Mahakama katika
Kanda.
Alifafanua
kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011, Majaji
Wafawidhi ndio wenye jukumu la kuwasilisha Tume ya Utumishi wa Mahakama, taarifa
ya uchunguzi wa mashauri ya kinidhamu kutoka kwenye Kamati ya Maadili ya
Maafisa Mahakama ya Mkoa au Wilaya. Aliongeza kuwa, taarifa ya Kamati inayowasilishwa
Tume inatakiwa pia kuwa na taarifa ya Jaji Mfawidhi kuhusu mwenendo wa Afisa
Mahakama mwenye shauri husika.
“Hivyo,
mafunzo haya ya siku tatu ni muhimu kwenu sio tu kwa ajili ya kutekeleza jukumu
la kuwafundisha Wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na Wilaya bali kwa
kuwa ninyi pia walezi katika masuala ya nidhamu na maadili kwa watumishi wa
Mahakama na wadau wa Mahakama katika mnyororo wa utoaji haki”, alisema.
Mwenyekiti
huyo wa Tume alisema Kamati za maadili ni jicho la Tume katika kusimamia,
kuendeleza na kudumisha maadili ya Utumishi wa Mahakama ili kuufanya utumishi
wa Mahakama kuwa wenye heshima, uadilifu, weledi, na uwajibikaji.
Prof.
Juma alisema kamati za Maadili zimepewa wajibu wa kisheria, wa kuishauri Tume
kuhusu uzingatiaji wa Maadili ya Utumishi wa Mahakama ili watoe huduma bora kwa
jamii ya Watanzania.
Kwa
upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume
ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel
amesema maadili ni moja kati ya nguzo muhimu za Mahakama ya Tanzania katika
kuboresha huduma na kuimarisha taswira chanya ya Mhimili huo.
Aliwataka
watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia
maadili ili wananchi wapate huduma bora na kujenga imani na Mhimili huo wenye
jukumu la msingi na la kikatiba la kutoa haki.
Mafunzo
ya siku mbili kwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu kutoka maeneo mbalimbali
nchini yanalenga kuwajengea uwezo Majaji hao wa kutoa mafunzo yanayofanana
(equal standard) kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa
na Wilaya katika mikoa yote nchini.
Tume ya Utumishi wa Mahakama
ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama
ya Tanzania. Moja ya
jukumu lake ni kusimamia Maadili ya
Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la
msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu
la kusimamia maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume,
yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kifungu 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Na.4 ya mwaka 2011.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni