Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaagiza Mawaziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria kushirikiana katika kutekeleza mapendezekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania aliyoyatoa kuhusu kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya Taasisi za Haki jinai iweze kusomana.
Mhe. Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo tarehe 01 Februari, 2024 wakati akihutubia kwenye hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini iliyofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
“Katika hotuba ya Jaji Mkuu ya maadhimisho ya Siku ya Sheria amebainisha maboresho makubwa ya Mahakama ambayo yametokana na TEHAMA, na hivyo kuzishauri pia Taasisi za Haki Jinai ziwe na Mifumo ya TEHAMA inayosomana ili kuongeza ufanisi na kupunguza hali ya mifumo kutosomana,” amesema Rais Samia.
Mhe. Dkt. Samia amesema kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana kuchukua mapendekezo yaliyotolewa na Jaji Mkuu na kuyatekeleza na hatimaye kuboresha Mfumo wa Haki Jinai nchini.
Katika hotuba yake kabla ya kumkaribisha Rais Samia, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alitoa rai kwa Wadau wa Haki Jinai kuwa na mifumo inayosomana ambapo amewashauri kuunda kamati itakayopitia na kuandaa taratibu/hatua mbalimbali za utendaji kazi (business process), kuunda matumizi TEHAMA na kuwa na mifumo inayosomana ya Taasisi za Haki Jinai.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Samia pia amewakumbusha Majaji na Mahakimu kuendelea kutumia njia ya Usuluhishi katika utatuzi wa migogoro mbalimbali inayowasilishwa mahakamani kwa kuwa njia hiyo ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda.
Amewaalika Wadau wa Haki Jinai, ambapo amesema, “Mahakama ya Tanzania milango iko wazi kwa Mahakama ya Tanzania kwa yeyote anayehitaji kujifunza kuhusu masuala ya maboresho na TEHAMA kwa ujumla, tuko tayari kusaidia.”
Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa rai kwa Majaji na Mahakimu nchini kushughulikia mashauri ya biashara kwa wakati ili kuwezesha wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuendelea na shughuli zao za kukuza uchumi wa nchi.
“Upo uhusiano mkubwa kati ya haki na uwekezaji, mwekezaji anathamini zaidi muda kwa kuwa muda ni mali hivyo, Mahakama zijielekeze kupunguza muda wa mashauri mahakamani”, alisema.
Mbali ya uboreshaji wa Mfumo wa Haki Jinai, Rais Samia amesema pia kuna haja ya kuangalia upande wa Haki madai kwakuwa nako bado kuna malalamiko.
“Tukiwa tunaangazia katika uboreshaji wa mfumo wa Haki Jinai tusisahau pia kutupia jicho upande wa haki madai kwa kuwa nako bado kuna malalamiko ikiwemo ya mashauri kuchukua muda mrefu,” ameeleza Rais Samia.
Kuhusu kazi ya utoaji, Rais Samia amewakumbusha Majaji na Mahakimu kutoa hukumu kwa haki kwakuwa Mahakama ina dhima kubwa katika kutekeleza kazi ya utoaji haki.
“Waheshimiwa Majaji na Mahakimu katika utendaji kazi wenu mnapaswa kukumbuka kwamba kazi ya kutoa haki ni kazi ya Mungu, hivyo mnawajibika kuifanya kwa uadilifu mkubwa bila dhuluma,” amesema Mhe. Dkt. Samia.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria yameadhimishwa leo katika Mahakama zote nchini, maadhimisho ya Siku hii yalitanguliwa na Wiki nzima ya utoaji elimu ya Sheria ambapo Mahakama pamoja na Wadau waliungana kuuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya Mhimili huo na sheria kwa ujumla.
Kaulimbiu ya Wiki na Siku ya Sheria ya mwaka huu; ‘Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.’
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (kushoto), Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kulia) pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi, Mhe. Dkt. Pindi Chana wakiwa katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini.
Mawaziri na Viongozi mbalimbali wa Serikali walioshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni