Alhamisi, 1 Februari 2024

JAJI MAGHIMBI USHIRIKIANO WA WADAU WA HAKI JINAI WASAIDIA KUPUNGUZA WAFUNGWA

 Na Magreth Kinabo -Mahakama

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,Mhe.Salma  Maghimbi amesema ushirikiano mkubwa na wadau wa mfumo wa haki jinai  umesaidia kupungua kwa  idadi ya wafungwa  waliokuwa magerezani wakisubiri rufaa zao kusikilizwa kutoka wafungwa 1,822 hadi 1,256.

 

Hayo yamesemwa na Jaji Maghimbi wakati wa kilele cha Siku ya Sheria kwa kanda hiyo, kilichofanyika kwenye kiwanja cha Mahakama Kuu eneo la mwuembeni jiji Dar es Salaam,ikiwa ni kutambua nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai,hivyo wamefanikiwa kuondoa mashauri mengi ya jinai ya mlundikano.

 

Alisema ushirikiano huo umetoka kwa wadau hao wakiwemo mawakili wa Serikali, mawakili binafsi pamoja na Magereza katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba mahabusu, wafungwa pamoja na wateja wengine wa Mahakama.

 

 Aidha Mhe. Maghimbi  aliongeza kwamba ushirikiano huo ambao umechangiwa zaidi na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) umeleta mafanikio makubwa pia  kwa upande wa mahabusu waliokuwa wakisikiliza usikilizwaji wa mashauri yao, idadi yao imepungua kutoka mahabusu 2,552 mwezi Desemba 2022 hadi mahabusu 1552 kwa Desemba 2023, huku mahabusu wenye zaidi ya miaka mitano wakipungua kutoka mahabusu 118 Desemba 2022 hadi 50 kwa Desemba 2023.

 

” Lengo ni kuhakikisha mahabusu walioko gerezani kwa zaidi ya miaka mitano bila kesi zao kusikilizwa kutokuwepo kabisa ifikapo mwezi Juni, 2024. Hii ni kwa magereza yote makuu matatu yaliyoko mkoa wa Dar-es-salaam yaani Gereza Kuu Ukonga na Magereza ya Mahabusu ya Ukonga na Keko”,alisema Jaji Maghimbi.

 

Alisema  pia wameanzisha Whatsap Group la wadau wa Haki Jinai na la Haki Jinai linalojumuisha Wahe. Naibu Wasajili, Mahakimu Wafawidhi, Mawakili wa Serikali pamoja na wale wa kujitegemea. 

 

Jukwaa  hilo hutumika kwa matumizi mbalimbali katika kutekeleza majukumu ya utoaji haki ikiwemo kutoa taarifa za vikao vya awali kabla ya kuanza vikao maalumu usikilizwaji mashauri. Vilevile mawasiliano hayo yamesaidia kupata majina ya mawakili ambao wanakuwa na utayari kutoa msaada wa kisheria kwa walioko magerezani. 

 

”Hii imesaidia kuepuka mgongano wa mawakili kwa mashauri tofauti kunakoweza kukwamisha usikilizwaji wa shauri. Matokeo chanya yaliyoonekana ni pamoja na matokeo makubwa kwenye vikao vinavyoendeshwa na Mahakama.

 

Alisema jambo lingine lilofanyika ni kutembelea magereza kwa gharama za Mahakama, tunaandaa huduma ya usafari na miundombinu wezeshi wafikapo magerezani. Hivyo hatua hiyo imesaidia kiasi kikubwa urahisi wa kuwapatia haki wenzetu wa magerezani na kurahisisha uendeshaji wa mashauri. 

 

Haya yamefanyika kujibu malalamiko ya mahabusu ya kutopatiwa muda wa kutosha ili kuonana na mawakili wao wanaopewa na serikali hivyo kujiona kama hawapewi haki ya kutosha ya utetezi. 

 

Aliongeza kwamba wamejenga tabia ya kushirikiana na wadau wengine wa haki jinai kutembelea na kukagua  mahabusu kitendo kilichosaidia kutambua changamoto nyingi wanazozipitia wafungwa na mahabusu na hivyo kuwa rahisi kupanga mikakati ya kukabiliana nayo.

 

Mhe. Jaji Maghimbi alifafanua kuwa kutokana na kauli mbiu yetu ya mwaka huu, ya wajibu wetu Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai, Mahakama Kuu Kanda ya Dar-es-salaam imejipanga kuweka historia kwa kufanya jumla ya vikao maalum 64 kwa mara moja, vikao hivi vitasikiliza mashauri ya mauaji pamoja na yale yanayohusu madawa ya kulevya. 

 

Alisema vikao hivyo vitaanza tarehe 19 Februari, 2024 na kumalizika 22 Machi 2024, ambapo jumla ya mahabusu 111 watapata haki ya kusikilizwa na hatima ya haki yao kujulikana. Vilevile kuanzia tarehe 11 Machi hadi 11 Aprili kutakuwa  vikao vinne vitakavyosikiliza mashauri ya Ugaidi. Jumla ya mahabusu takriban 47 watapata haki ya kusikilizwa na hatma yao kujulikana. Mahabusu hawa ni kati ya wale 50 ambao wamekaa gerezani zaidi ya miaka mitano. 

 

Alisema  idadi hiyo ya mashauri ya jinai yanayosikilizwa kwa vikao maalumu haijawahi kufanyika kwa wakati mmoja kwa Kanda yetu, lakini kutokana na uimarikaji wa matumizi ya mifumo mbalimbali na uboreshwaji wa huduma, hili litawezekana kwa mwaka huu. Mashahidi wataoshindwa kufika Mahakamani pia watasikilizwa kwa njia ya mtandao hivyo ni matumaini yetu kuwa mashauri haya yatamalizika kwa kiwango kikubwa. 

 

Alisema jambo hilo ni katika kutekeleza kwa vitendo yale yalioainishwa kwenye ripoti ya Tume ya Haki Jinai pamoja na taarifa ya Kamati ya Mhe Jaji Mkuu iliyopitia mapendekezo ya ripoti ya Tume hiyo.

 

Mgeni maalum ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila   alisema bado upo umuhimu wa Serikali na Mahakama kutatua changamoto pamoja mfano tatizo la usafiri wa mahabusu mna wafungwa. 

 

Naye Bi. Wema Pumzi ambaye ni mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na Mahakama ili iweze kutimiza jukumu lake la utoaji haki 

 

Kwa upande mwakilishi kutoka Chama WanasheriaTanganyika (TLS),Wilngton Rwebinyasi alisema  chama hicho kina wajibu wa kuboresha mifumo ya haki jinai ili iweze kuwa na tija na ufanisi.  



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,Mhe.Salma Maghimbi akitoa hotuba yake ya kilele cha Siku ya Sheria.


 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,Mhe.Salma Maghimbi (aliyesimama mbele)akiwa na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania  wakijiandaa   kwa ajili ya  kilele cha Siku ya Sheria.

Wageni waalikwa, na watumishi wa Mahakama wa Kanda hiyo wakiwa katika hafla ya kilele hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,Mhe.Salma Maghimbi akikagua gwaride la  kilele cha Siku ya Sheria.


 Wanafunzi Shule ya Sekondari ya Jitegemee wakiimba  wimbo maalum wa siku hiyo.

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad akiomba dua kwa ajili ya kuanza kwa shughuli za Mahakama.

 Padre Nicolaus Masamba  akiomba sala.

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni