Ijumaa, 2 Februari 2024

MAADHIMISHO SIKU YA SHERIA YAFANA KATIKA MAHAKAMA KUU KANDA, MIKOA

Maadhimisho ya Siku ya Sheria yamefanyika kote nchini jana tarehe 1 Februari, 2024 huku Viongozi mbalimbali wa Serikali wakishiriki kikamilifu kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa.

Mwandishi wetu Lusako Mwang’onda anaripoti kutoka Mahakama Kuu, Iringa kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania imeahidiwa kupata kiwanja kikubwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la Mahakama Kuu. 

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego. Amesema Mahakama Kuu Iringa inatakiwa kuwa na eneo kubwa linalostahili na kuendeana na maboresho mbalimbali yanayoendelea mahakamani. 

Mkuu wa Mkoa amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Iringa kuanza mchakato huo mapema.

Mhe. Halima alikuwa ni Mgeni Maluumu katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria ambayo kwa Mkoa wa Iringa yamefanyika katika Viwanja vya Mahakama Kuu Iringa maeneo ya Gangilonga katika Manispaaa ya Iringa.

Akiongea katika maadhimisho hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuliona hitaji hilo la Mahakama la kuwapatia ardhi kwa ajili ujenzi wa jengo lingine la Mahakama Kuu. 

Jaji Mugeta, ambaye alikuwa ndio Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo, alisema wataifuatilia ahadi hiyo ya Mkuu wa Mkoa, maana wana kiu kubwa ya kupata eneo lingine. 

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tutakusumbua sana katika kipindi hiki maana tunauhitaji sana wa hilo eneo. Hivyo ujue kuwa kumwahidi chakula mtu mwenye njaa ni kujiahidia usumbufu mwenyewe,” Jaji Mugeta alisema.

Maadhimisho ya Siku ya SherianNchini kwa Mahakama Kuu Mkoa wa Iringa yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Viongozi wa Dini, vyama vya siasa pamoja na wadau mbalimbali wa haki. 


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta (aliyesimama juu) akikaribishwa kukagua gwaride maalumu liliandaliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya madhimisho ya Siku ya Sheria. Nyuma ya Jaji Mgeta ni Majaji wengine wa Mahakama Kuu Iringa ambao ni Mhe. Angaza Mwipopo, Mhe. Saidi Kalunde na Mhe. Dkt. Eliaman Laltaika.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta akikagua gwaride maalumu lililoandaliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta akizungumza na umati wa watu (hawapo pichani) uliojitokeza katika maadhimisho hayo katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa maeneo ya Gangilonga.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego akizungumza na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo.

Watumishi wa Mahakama wakiimba shairi maalumu mbele ya Meza Kuu katika kuadhimisha hayo lililotungwa na Jaji wa Mahakama Kuu Iringa, Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika.

Sehemu ya umati wa watu uliojitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria ukimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta. 

Kutoka Mahakama Kuu Songea, Mwandishi Wetu Hasani Haufi anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha ameeleza kuwa maboresho yaliyofanywa na Mahakama katika suala la miundombinu muhimu, hususan matumizi ya mifumo ya TEHAMA, hayatakuwa na maana iwapo Taasisi zingine zilizopo kwenye mnyororo wa haki jinai hazitafungamanisha mifumo yao isomane na ile ya kimahakama ili kurahisisha uendeshaji na utaratibu wa mashauri.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria kwa Kanda ya Songea, yaliyofanyika katika viunga vya Mahakama Kuu mkoani humo, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa kama Taasisi hizo zikitekeleza wajibu wake ipasavyo haki itapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Aidha, Jaji Karayemaha alitanabaisha kuwa kuanzishwa kwa mfumo huo jumuishi wa taasisi za haki jinai kutaondoa urasimu wa utendaji kazi katika hatua mbalimbali sambamba na kuongeza ufanisi wa uendeshaji na usimamizi wa utoaji haki jinai.

Sambamba na hayo, alieleza kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea uwepo wa amani, usalama na utulivu, hivyo hakuna budi kufanyika maboresho ya kisera, sheria na kanuni kwenye sekta ya sheria na mfumo wa makosa ya jinai nchini kwa ujumla wake.

Kilele cha maadhimisho hayo yaliyohudhuruiwa na wadau wote muhimu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas, yakibeba kauli mbiu inayosema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akizungumza na wadau wa haki jinai (hawapo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Sheria katika viunga vya Mahakama Kuu Songea


Mahakimu wa ngazi zote, Mawakili wa Serikali na Kujitegemea na wadau wengine wa haki jinai waliohudhuria sherehe hizo.

Kutoka Mahakama Kuu Sumbawanga, Mwandishi wetu Mayanga Someke  anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dkt. Deo Nangela, amewakaribisha na kuwashukuru wageni wote kwa kuitikia mwaliko na kujumuika pamoja katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

“Katika Wiki ya Sheria mwaka huu, wengi mmepata fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama ikishirikiana na wadau wake,” alisema. 

Alieleza kuwa Dhana ya Uhuru wa Mahakama ni katika kusikiliza na kutoa maamuzi mbalimbali kwa mujibu wa ibara ya 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si vinginevyo.

“Shughuli zetu ni sehemu tu ya mgawanyiko wa majukumu kati ya mihimili hii mitatu ya dola, mgawanyiko huu ni muhimu katika Nchi yoyote inayojali na kuheshimu Demokrasia na utawala bora wa sheria,” Jaji Mfawidhi alisema.

Mhe. Dkt. Nangela alieleza kuwa maendeleo na ustawi wa Taifa lolote yanategemea uwepo wa amani, usalama na utulivu.

‘Katika kuhakikisha Nchi inaeandelea kuwa na amani, usalama na utulivu maboresho ya kimkakati katika tasnia ya utoaji haki yanatakiwa kuwa jumuishi katika kuboresha sera, sheria na kanuni kwenye sekta ya sheria na mfumo wa makosa ya jinai Nchini kwa ujumla wake,” alisema.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere ameipongeza Mahakama kwa kuweka Wiki na Siku ya Sheria katika mwaka wake wa shughuli na kupitia kauli mbiu imekuwa ni muhimu ikiwa na lengo la kujenga ushirikiano baina ya Mahakama na wadau wake.

“Napenda kutoa wito kwetu sote tuenzi mfumo wa utoaji haki, kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama ni chombo pekee ambacho kimekasimiwa mamlaka ya mwisho katika utoaji haki kwa mwananchi,” alisema.

Alibainisha kuwa katika utoaji haki Mahakama haifanyi kazi pekee yake, bali inashirikiana na wadau mbalimbali na ushirikiano huo ndio ambao unatengeneza mfumo jumuishi wa utoaji haki nchini.

Mhe. Makongoro alisema kuwa kuanzishwa kwa mfumo Jumuishi wa Taasisi za Haki Jinai kutasaidia upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kuondoa urasimu wa utendaji kazi katika hatua mbalimbali kwenye taasisi za haki jinai.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dkt. Deo Nangela akisoma hotuba katika kilele cha Siku ya Sheria.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe Charles Makongoro Nyerere akitoa salamu katika maadhimisho hayo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dkt. Deo Nangela akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake.


Viongozi na wadau wa Mahakama.


Watumishi wa Mahakama wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mgeni rasmi.

 Naye James Kapele wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ambaye alikuwa mgeni maalum, ameongoza mamia ya wananchi waliojitokeza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kilichofanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi.

Akiongoza hafla hiyole iliyopambwa na hotuba pamoja na burudani mbalimbali, Mhe Mrindoko ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) pamoja na miundombinu ya majengo ambayo kwayo itazidi kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwapunguzia gharama pamoja kupatikana kwa haki kwa wakati.

“Naomba nitumie fursa hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho ya mifumo mbalimbali ya uendeshaji wa mashauri pamoja na miundombinu ambayo naamini itawasaidia wananchi wetu katika kuzipata haki zao…

 “… kwani kusimikwa na kujengwa kwa majengo haya mazuri ambayo yatakuwa na ngazi zote za Mahakama itawasaidia wananchi wetu kupata haki zao kwa wakati na kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri yanayowakabiri. Lakini pia wananchi nanyi tumieni TEHAMA kujifunza mambo mbalimbali ya sheria ili kuzijua haki zenu,” alisema.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye amewapongeza wadau wa haki wote walioshiriki kikamilifu katika siku zote zilipangwa kwa ajili ya utoaji wa elimu na kuwaomba wadau wote kuendelea kutumia TEHAMA katika kuendesha mashauri yao ili kutopitwa na maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania katika kusogeza na kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini.

Katika maadhimisho ya kilele hicho, jumla ya hotuba nne zimewasilishwa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chama cha Mawakili Tanganyika, Ofisi ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi na ile ya mgeni maalum.

Katika Picha ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko akiwasilisha hotuba yake ambaye pia ndiye aliyekuwa mgeni maalum katika kilele cha Siku ya Sheria mkoani Katavi.

Pichani ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Mhe, Gway Sumaye akiwasilisha hotuba yake.

Pichani Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,Valence Mayenga alipokuwa akiwasilisha hotuba kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika picha ni Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika waa Mkoa wa Katavi, Msomi Sekela Amulike alipokuwa aliwasilisha hotuba ya Chama cha Mawakili nchini.

Katika picha ni sehemu ya wageni waalikwa na baadhi ya watumishi wa Mahakama wakifuatilia matukio mbalimbali katika hafla hiyo.

Sehemu ya wageni waalikwa wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilika kwa hafla hiyo.

Pichani ni sehemu ya kikundi cha burudani wakitumbuiza katika hafla hiyo.

Kutoka Mahakama Njombe, Abdallah Salum anaripoti kuwa Mgeni Rasmi ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa   Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama aliwaongoza wananchi kuanzimisha Siku ya Sheria katika Mkoa wa Njombe.

Mgeni maalum katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Juma Swadi, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Mhe. Chamshama alisisitiza matumizi ya TEHAMA miongoni mwa wadau katika mnyororo wa utoaji haki ili wadau pamoja na Mahakama waweze kwenda pamoja.

“Lazima akili zetu ziwe tayari kujua Dunia inaendaje, kwani sasa TEHAMA ipo kila mahali unapokwenda kwenye Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa wananchi, hivyo kwa sisi ambao tupo kwenye mifumo ya kutoa haki lazima tukubaliane na hili ili twende sambamba,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya alishukuru kwa kukaribishwa na pia amejifunza mengi kuhusu sheria na utendaji wa shunghuli nyingi za kimahakama, huku akitoa  salamu kutoka kwa Mkuu wa Mkoa  wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka kwa kutoa pongezi kwa  Mahakama pamoja na wadau wake kwa kazi na ushirikiano wake

Sherehe hizo zilipambwa kwa kway ana maigizo, huku wadau mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashataka, vyombo vya usalama na ulizi  na Mawakili wa Kujitegemea.

Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa   Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama akisoma hotuba katika maadhi isho ya Siku ya Sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Juma Swadi akiwa mgeni mahsusi.

Wageni mbalimbali wakiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa   Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama.

Watumishi wa Mahakama na wananchi (juu na chini) wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa maadhimisho hayo.

(Haberi sizi zimehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni