Mahakama ya Tanzania jana tarehe 1 Februari, 2024 imeadhimisha Siku ya Sheria nchini kote, huku Wakuu wa Miko ana Wilaya wakiunga na Majaji na Mahakimu Wafawidhi na watumsihi wa Mahakama kwa ujumla katika maadhimisho hayo.
Mwandishi Wetu Francisca Swai wa Mahakama, Musoma anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, amewaasa wananchi na wadau wa Mahakama kuona umuhimu wa haki jinai na kuunga mkono juhudi za kitaifa zinazofanywa katika maboresho ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo.
‘‘Wadau wote wa haki jinai tunashirikiana kwa pamoja kuwajenga upya watendaji wa makosa na kuwafanya kutoyarudia ili kujenga maadili katika jamii nzima kwa ustawi wa Taifa kwa ujumla’’ amesema Mhe. Mtulya.
Alieleza kuwa, mfumo wa haki jinai umetengenezwa kwa namna ya kutoa haki kwa wote, watenda uhalifu na waliotendewa uhalifu na mfumo huo hufanya watu kuwa na amani kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa kuamini kuwa wako salama.
Alisema haki ni msingi wa ustawi wa Taifa na pale kunapokuwa na ukiukwaji wa haki jinai kunakuwa na madhara ya moja kwa moja kwenye uchumi na kimaadili.
Akizungumzia ripoti ya Tume ya Haki Jinai, Mhe, Mtulya alisema mapendekezo iliyotoa yanathibitisha dhahiri kuwa Mahakama na wadau wake, hasa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Jeshi la Polisi wanalo jukumu la moja kwa moja katika kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati kwa ustawi wa Taifa.
Jaji Mfawidhi alisema kuwa katika kuhakikisha mashauri ya jinai yanasikilizwa kwa wakati, Mahakama imeweka nguvu katika maboresho ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyowajumuisha wadau, ikiwemo Jeshi la Magereza.
“Katika kanda ya Musoma magereza zote zimewezeshwa vifaa vya simu na televisheni za kisasa zenye uwezo mkubwa kwa ajili ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya simu na televisheni (tele/video conference) ili kusiwe na sababu yoyote ya kuzuia usikilizwaji wa mashauri kwa wakati,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya Musoma, Mhe. Dkt. Halfan Haule ,akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, ameishukuru Mahakama kwa utaratibu wa Wiki ya Sheria na kutoa mfano wa namna alivyoweza kutatua malalamiko ya wananchi juu ya utaratibu wa dhamana.
Pia alitoa wito kwa Mahakama na wadau wake kuendelea kutoa elimu zaidi ya masuala mbalimbali ya kisheria kwa jamii, jambo litakalo saidia kupunguza malalamiko mengi ambayo yanatokana na uelewa mdogo wa sheria.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Kitia Turoke kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, katika hotuba yake ameipongeza Mahakama kwa ushirikiano mzuri na Taasisi nyingine za haki jinai.
Alisisitiza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu 2024 inawataka wadau wote wa haki kuonesha namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kuboresha mfumo wa Haki Jinai kwa mujibu wa majukumu waliyopewa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Mara, Wakili Onyango Otieno, katika hotuba yake alizungumzia mambo makubwa matatu ikiwemo, nafasi ya chama hicho katika kutekeleza mapendekezo ya tume ya kuboresha mifumo na taasisi za haki jinnia.
Pia alielezea nafasi ya chama hicho katika kusaidia wananchi, watuhumiwa wasiokuwa na uwezo wa kuwalipa Mawakili na wajibu wa chama hicho kusimamia utawala wa sheria na kupambana na uhalifu mamboleo na unaovuka mipaka ya nchi.
Alisema Chama cha Wanasheria Tanganyika kimejizatiti kimkakati ili kuhakikisha kinatoa mchango wa kitaalam kadri iwezekanavyo ili kutekeleza kwa tija na ufanisi mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai kwa kuendelea kuboresha mahusiano mazuri na wadau mbalimbali wa haki jinai.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yamekuwa ya kipekee kwa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, kwani imeadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019.
Mahakama hiyo imejivunia mambo mbalimbali, ikiwemo kasi nzuri ya usikilizaji wamashauri, kwani kwa miaka hiyo imesajili mashauri 4,689 na kumaliza mashauri 4,327, kutokuwa na mashauri mlundikano, kuimarisha ushirikiano mzuri kati ya Mahakama na wadau wake, kuwa na umoja, upendo na ushirikiano kati ya Viongozi na watumishi ndani ya Kanda.
Msafara wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati mbele), Majaji wa Mahakama Kuu Musoma na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na Mahakimu na Mawakili wakiwa tayari kwa maandamano ya ukaguzi wa gwaride lililoandaliwa.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Salome Mshasha akisema neno wakati wa shughuli za maadhimisho ya siku ya sheria nchini.
Wakili Kitia Turoke kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisoma hotuba katika sherehe hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Mara, Wakili Onyango Otieno akisoma hotuba yake sherehe za Siku ya Sheria nchini.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati mbele) akiwa na Viongozi wengine walioshiriki kwenye maadhimisho hayo.
Meza Kuu pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma.
Kutoka Mahakama, Bukoba, Mwandishi Wetu Ahmed Mbilinyi anaripoti kuwaJaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imaculata Banzi amesema maendeleo na ustawi wa Taifa yanategemea uwepo wa amani, usalama na utulivu.
Amesema kuwa katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, usalama na utulivu, maboresho ya kimkakati katika tasnia ya utoaji haki yanatakiwa kuwa jumuishi katika kuboresha Sera, Sheria na Kanuni kwenye Sekta ya Sheria na mfumo wa makosa ya jinai nchini kwa ujumla wake.
Mhe. Banzi aliyasema hayo jana tarehe 01 Februari, 2024 wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria iliyofanyika katika Viwanja Mahakama Kuu Bukoba Mkoani Kagera, ambapo Mgeni Mwalikwa akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa.
Jaji Mfawidhi amesema kuwa kwa mwaka huu kauli mbiu ni:” Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa:Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa Haki Jinai.”
Mhe Banzi amesema “dhana ya Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai inajitokeza kuanzia kwenye Katiba kupitia Ibara ya 13 (3). Aidha, zipo Sheria, Kanuni, na Miongozo mbalimbali zinazofafanua kuhusu dhana ya mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.
“Miongoni mwa Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Huduma ya Mashtaka nchini Sura ya 430 Toleo la 2022 (National Prosecutions Service Act) ambapo kifungu cha 27 cha Sheria hiyo, kimeanzisha Jukwaa la Haki Jinai kitaifa ambalo hujumuisha Wakuu wa Taasisi zote zinazohusika na masuala ya Haki Jinai.”
Kwa msingi huo, Jaji Mfawidhi amesema Mahakama imekuwa ikishirikiana na Wadau mbalimbali wa Haki Jinai ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanganyika (TLS), Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza, TAKUKURU, Ustawi wa Jamii na wengine wengi katika kutekeleza jukumu lake la utoaji haki, hivyo kudumisha amani, utulivu, usalama na umoja wa kitaifa na hivyo kuboresha Ustawi wa Taifa”.
Awali, Mhe. Mwasa alipata nafasi ya kutoa hutoba yake na kuwapongeza Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel kwa jitihada kubwa wanazofanya kuboresha Mhimili wa Mahakama kwa kujenga miundombinu ya Mahakama pamoja na matumizi ya Technolojia ya Habari ya Mawasiliano (TEHAMA) ili kutoa haki kwa wananchi kwa wakati.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculate Banzi akisoma hotuba katika sherehe za kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria.
Mgeni Mwalikwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Mwasa akisoma hotuba katika sherehe hizo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculate Banzi akikagua gwaride katika sherehe za kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria katika viwanja vya Mahakama Kuu Bukoba.
Pichani katika juu na chini Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculate Banzi akiwa pamoja na Mgeni Mwalikwa, (kushoto kwake, Mhe. Fatma Mwasa, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba pamoja na Mawakili wa Serikali na Mahakimu.
Naye Iman Mzumbwe wa Mahakama, Songwe anaripoti kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube amewashukuru wadau wote walioshriki kutoa elimu katika Wiki ya Sheria na kuwapongeza Wananchi wote waliojitikeza kupata elimu hiyo muhimu.
Mhe. Makube ameielezea kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa; Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai” kuwa imekuja kwa wakati muafuaka ambapo Taifa linaanda Dira ya Taifa ya Maendeleao ya mwaka 2025/2030.
Alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa ikiongozwa na dira yake ya utoaji haki kwa wakati na kwa wote na imekuwa ikizingatia matakwa mengine ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama yalivyoanishwa katika Ibara ya 107A (2) (a)-(e).
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa Songwe, Mhe. Francis Michael ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji mzuri wa kazi na kusisitiza kuwa mashauri yasikilizwe kwa wakati, hasa kesi za ubakaji, ulawiti na unyanyasaji ili kupunguza vitendo hivyo viovu katika jamii.
Aliiasa jamii iepukane na imani potofu ambazo zinaweza kupelekea kutokea vitendo visivyo faa kwenye jamii.
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ameeleza kuwa chama chao kimejizatiti kimkakati ili kuhakikisha kinatoa mchango wa kitaalamu kadri iwezekanvyo na kama itakavyohitajika ili kutekeleza kwa tija na ufanisi mapendekezo yaliyotolewa na tume ya haki jinai.
Amesema chama kitahakikisha wanatoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi wasiojiweza kiuchumi na kumudu gharama za kumulipa Wakili ili kuwakilishwa mahakamani katika mashauri yanawakabili.
Sehemu ya Meza Kuu katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria Mkoa wa Songwe.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube akihutubia wananchi katika sherehe hizo.
Wakili kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) akiwasilisha hotuba yake.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Francis Michael akihutubia wadau katika Siku ya Sheria.
Sehemu ya wageni waalikwa wakisikiliza hotuba.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama wakisalimia meza kuu.
(Habari hizi zimehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni