Na. Eunice Lugiana – Mahakama, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ametoa
wito kwa Mahakama kuishirikisha Serikali kuelezea kuhusu maboresho yanayofanywa
na Mahakama ili kurahisisha utoaji wa elimu kwa wananchi kwani Serikali ina
mtandao mkubwa wa kuwafikia wanachi.
Akizungumza
katika hafla ya kuadhimisha Wiki na siku ya Sheria nchini jana tarehe Mosi
Februari, 2024 mkoani Pwani alipokuwa akiwahutubia wananchi na wadau wa
Mahakama Mhe. Kunenge alisema, bado wananchi wengi hawajui mipaka ya Serikali na
Mahakama hivyo ni wajibu wa Viongozi wa Mahakama na Serikali tuwafahamishe mipaka
hiyo ili kuepuka kuingilia utendaji kazi wa Muhimili.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mkoa wa Pwani Mhe. Joyce Mkhoi katika hotuba yake alisema kauli mbiu ya
mwaka huu imekua na malengo makuu
mawili kuhamasisha Mahakama na wadau juu
ya umuhimu wa kufungamanisha na kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai
unaosomana ili kusaidia katika
kubadilishana taarifa kuanzia hatua ya upelelezi, uendeshaji wa mashtaka
na utoaji wa maamuzi.
“Kauli mbiu hii ina lengo la kuikumbusha Mahakama na Taasisi nyingine za haki jinai kuwa zinawajibika katika kufungamanisha na kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai. Hivyo nakuwataka wadau kuongeza juhudi ya kuwekeza kwenye eneo la miundo mbinu ya TEHAMA na usimikaji wa mifumo ya kidigitali”, alisisitiza Mhe. Mkhoi.
Mhe. Mkhoi ameongeza kuwa, wadau wa Mahakama
wanawajibika kuendana na kasi ya mabadiliko ya nchi kwa kufanya maboresho
katika ujenzi wa mifumo kwa taasisi zote zinazoshirikiana na Mahakama katika
Mnyororo wa haki jinai ili utendaji kazi uweze kuleta tija na uwe wa ufanisi
mkubwa ambao utaweza kukabiliana na
changamoto ambazo zimekuwa zinaukabili mfumo wa haki jinai.
Akisikiliza kesi ya kwanza inayoashiria uzinduzi rasmi
wa Mwaka wa kimahakama wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibaha Mhe. Emmael Lukumai amesema Mahakama imepiga
hatua katika kusikiliza mashauri kutoka kwenye nyaraka ngumu na sasa Mahakama
inasikiliza kesi katika nyaraka laini na zama za nyaraka ngumu zimeisha.
Akionyesha jinsi haki jinai ilivyo rafiki ametoa
masharti rahisi ya dhamani ya mshtakiwa aliyekua na kosa la kusafirsha kiwango
kidogo cha madawa ya kulevya aina ya bhangi Mhe. Lukumai amesema masharti hayo
ni wadhamini wawili walio na barua za utambulisho wa makazi na mali kauli ya
shiligi milioni moja.
Kilele cha siku ya sheria kimeadhimishwa katika
viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani na Mgeni wa Heshima alikua
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge aliye ambatana na kamati ya
ulinzi na usalama ya Mkoa, sherehe hizo
pia zimehudhuriwa na viongozi wa dini taasisi za serikali na viongozi wa vyama
vya siasa mawakili wa kujitegemea pamoja na wananchi wa Kibaha.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge akihutubia Wananchi na Wadau
wa Mahakama (hawapo pichani) Katika Sherehe za Siku ya Sheria nchini katika
Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani
Hakimu Makazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani Mhe. Joyce
Mkhoi akitoa Hotuba yake mbele ya Mgeni wa Heshima (hayupo pichani) katika
Kilele cha Siku ya Sheria Nchini Mkoa Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge (katika) akiwa meza kuu na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Pwani (Kushoto) Ni Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Pwani Bi. Faraja Kiula, Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Mahakama Ya Hakimu Mkazi Kibaha Mhe, Joyce Mkhoi (wa pili kushoto), wengine ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mawakili Wakujitegemea Bi, Rita Ntagazwa (wa kwanza kulia) na Hakimu Mkazi Mfawidhi Wa Mahakama Ya Wilaya Kibaha Mhe. Emmael Lukumai (wa pili kulia) .
Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge (katikati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Makimu wa Mkoa wa PwaniMeza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge (katikati) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mawakili wa Serikali Mkoa wa Pwani
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni