Jumanne, 26 Machi 2024

DIVISHENI ZAUNGANA KUFANYA MATENDO YA HURUMA

 

Na Mwanaidi Msekwa-Divisheni Kazi

 

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Ardhi na Kituo cha Usuluhishi waungana na kufanya matendo ya huruma katika Taasisi ya Saratani Ocean Road  ya  mwishoni mwa wiki iliyopita

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina aliongoza jopo la Majaji wanne, Naibu Wasajili wawili na watumishi kutoka katika Divisheni hizo. Msafara uliwasili majira ya asubuhi katika viwanja vya taasisi ulipokelewa na mwenyeji wao Afisa Ustawi wa Jamii katika Taasisi ya Saratani Ocean Road Bw. Michael Pantaleo.

 

Katika ziara waliweza kuwafariji na kuwapa mkono wa pole wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi hiyo kwa kuwapelekea baadhi ya vifaa vya matibabu na vifaa muhimu vya matumizi ya kawaida. 

 

Aidha Mhe. Mlyambina aliwapongeza na kuwashukuru viongozi na watumishi wote waliohudhuria na kushiriki kwa hali na mali katika kufanikisha ziara hiyo iliyoleta hamasa kubwa na kuongeza ushirikiano baina ya viongozi na watumishi wa kada mbalimbali wa Divisheni hizo. Alisema “ziara hii imeleta furaha kubwa kwetu na kwa wagonjwa, ni jambo la kujivunia,”.

 

Ziara hiyo imehudhuriwa na Viongozi kadhaa wa Divisheni za Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina, Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Angela Bahati, Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Alafa Msafiri, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale.

 

Viongozi wengine ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Augostina Mmbando na Naibu Msajili Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Mary Mrio. Maofisa Utumishi wa Divisheni na watumishi wa kada mbalimbali walihudhuria.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina(wanne kushoto mstari wa mbele), Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo (watano kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Angela Bahati,wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Divisheni hizo, vikiwemo vifaa na vitu vilivyotolewa.



Majaji hao wakiwa katika   picha ya pamoja na watumishi.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni