Jumatano, 27 Machi 2024

MWAROBAINI WA MIGOGORO YA UCHAGUZI WAIVA

Na Seth Kazimoto, Mahakama Kuu Arusha

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amefungua Kikao Kazi cha Kuthibitisha Mpango wa Mafunzo juu ya Namna Nzuri ya Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi. 


Akifungua kikao kazi hicho cha siku mbili tarehe 25 Machi, 2024 kilichofanyika katika Hoteli ya ‘Palace’  jijini Arusha, Mhe. Kihwelo alisema, “Tumekusanyika hapa leo sio tu kama watu binafsi lakini kama wafanyakazi walio mstari wa mbele katika haki ya uchaguzi ambayo inaweka msingi wa demokrasia na Utawala wa Sheria kwa lengo la kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya uchaguzi na kuongeza uaminifu, uadilifu na uhalali wa michakato yetu ya uchaguzi.” 

 

Mkuu huyo wa Chuo alisisitiza kuwa uundaji wa nyenzo hizo umetokana na majadiliano ya kina yaliyofanywa na Maafisa wa Mahakama na Wadau Wataalam huku akieleza kuwa, Mpango huo wa mafunzo umejikita katika uhalisia wa mifumo ya sheria na uchaguzi inayolenga kushughulikia changamoto zinazojitokeza kama vile ukosefu wa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa na hitaji la uwazi katika taratibu za kukata rufaa.

 

Kadhalika, alisema kwamba Mpango huo wa Mafunzo umezingatia mazingira yanayoendelea ya teknolojia katika chaguzi, ikisisitiza haja ya miongozo ya kushughulikia ushahidi wa kielektroniki na kujumuisha mitazamo ya kijinsia na mienendo ya watumishi wa umma katika chaguzi akisisitiza kuwa, nyenzo hizo zitasaidia kuiongoza Mahakama katika kusimamia haki, uwazi na ufanisi katika utatuzi wa migogoro inayohusiana na uchaguzi.

 

Kikao Kazi hicho, kimelenga kurasimisha Mpango wa kina wa Mafunzo kwa Majaji na Mahakimu na kuwapa maarifa juu ya namna ya kusimamia na kuendesha mashauri yatokanayo na uchaguzi na hasa kwa kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kote Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Jaji Kihwelo alitaja mada zitakazofundishwa katika kikao kazi hicho kuwa ni pamoja na Rasimu ya Mpango wa mafunzo juu ya Utatuzi wa Migogoro wakati wa uchaguzi,   Rasimu ya Mwongozo wa Mafunzo kwa waendeshaji wa mashauri ya uchaguzi katika Mahakama za wilaya, na Rejea rahisi ya Mahakimu katika kuendesha mashauri ya Uchaguzi katika ngazi ya Serikali za Mitaa.

 

Kikao kazi hicho kimefanyika kwa ushirikiano baina ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Taasisi ya Kimataifa ya Mifumo ya Uchaguzi (IFES) na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Paul Kihwelo, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda na Watoa mada ambao ni  Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Wahe. Emanuel Kawishe na Hamidu Mwanga; na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba.



Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akifungua Kikao Kazi cha Kuthibitisha Mpango wa Mafunzo juu ya Namna Nzuri ya Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi kilichofanyika tarehe 25 Machi 2024 jijini Arusha.

 

 


Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizungumza wakati wa Kikao Kazi cha Kuthibitisha Mpango wa Mafunzo juu ya Namna Nzuri ya Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi kilichofunguliwa tarehe 25 Machi, 2024 jijini Arusha.

 


Wajumbe walioshiriki Kikao Kazi cha Kuthibitisha Mpango wa Mafunzo juu ya Namna Nzuri ya Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi tarehe 25 Machi 2024 wakiwa katika kikao hicho kilichofanyika katika Hoteli ya ‘Palace’ jijini Arusha.


  




Picha ya pamoja ya washiriki wa Kikao Kazi cha Kuthibitisha Mpango wa Mafunzo juu ya Namna Nzuri ya Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi kilichofanyika tarehe 25 Machi, 2024 jijini Arusha. Walioketi ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati), Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba (kulia) na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (kushoto).



Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba akitoa mada wakati wa Kikao kazi cha Kuthibitisha Mpango wa Mafunzo juu ya Namna Nzuri ya Uendeshaji Mashauri ya Uchaguzi kilichofanyika tarehe 25 Machi 2024 jijini Arusha.

 

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni