Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai ameongoza kikao cha Kusukuma Mashauri katika Mahakama ya Wilaya hiyo huku akipongeza ushirikiano wa Wadau.
Akizungumza leo tarehe 22 Machi 2024 katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, wakati akiongoza kikao hicho, Mhe. Lukumai amewashukuru pia kwa kufanya kazi kwa bidii na kuiwezesha Mahakama hiyo kutokuwa na mashauri ya mlundikano.
Naye, Wakili wa Serikali, Bi. Elizabeth Olomi akitoa mchango wake wa namna bora ya kumaliza mashauri kwa wakati amesema ushirikiano baina ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Polisi, Upelelezi na Mahakama kutasababisha kumalizika kwa mashauri kwa wakati.
“Kama upelelezi utafanyika kwa wakati mashahidi wakafika kwa wakati na Mahakama itakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusikiliza mashauri kwa wakati mlundikano wa mashauri hautakuwepo,” alisema Bi. Elizabeth.
Akijibu hoja iliyoibuka katika kikao hicho kwamba upelelezi umekuwa ukicheleweshwa na Polisi kwa kutokufika mahakamani tarehe husika ya kusikiliza shauri, Mwakilishi wa OC-CID, Mkaguzi wa Polisi Tamimu amesema Ofisi ya Mashtaka ya Taifa itoe wito kwa wakati kwa askari anayetakiwa kufika mahakamani kutoa Ushahidi na sio kupiga simu ya kutoa taarifa kwa muda mfupi wakati askari husika anakua amepangiwa kazi nyingine.
Akichangia hoja hiyo, Mhe. Lukumai ameshauri kwamba kama kuna ahirisho fupi shahidi ajulishwe kwa simu na pia wito wake utumwe kwa barua pepe na akifika siku ya kesi atapata wito wake kwa kumbukumbu zaidi.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mkoa wa Pwani, Bi. Rita Ntagazwa ameshauri kwa upande wa Mashtaka kuwa na mawasiliano na Mawakili na pia wawe na uthibitisho kuwa shahidi amepata wito na kama hatafika kwa tarehe husika aseme sababu na uthibitisho wa sababu yake.
Naye Afisa kutoka Ofisi ya Huduma kwa Jamii (Probation Officer), Bw. Deogratius Njuu amewaomba Mahakimu kwa mashauri ambayo sheria inaruhusu kutoa adhabu mbadala watoe adhabu hizo ili kupunguza msongamano kwenye Magereza.
Sambamba na kikao hicho cha Kusukuma Mashauri kilichowahusisha Wadau wa Haki Jinai pia kimefanyika kikao cha kusukuma mashauri ya madai kilichowahusisha wadau wa mashauri ya madai (Bench Bar).
Katika kikao hicho, Mhe. Lukumai pia amewataka Mahakimu kupanga mashauri kwa muda tofauti kuliko kupanga mashauri yote saa mbili asubuhi na kuwaweka wateja kwa muda mrefu wakisubiri kwa kuwa tu mashauri ya madai yanaanza asubuhi.
Naye Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Mailimoja, Mhe. Roselyne Mwakilasa amewaomba Mawakili kuangalia shauri la kupeleka mahakamani kwa kuwa Sheria za Mahakama ya Mwanzo haziruhusu kufanya usuluhishi wao wana nafasi ya kuwasuluhisha wadaawa kama shauri lao linasuluhishika ili kuokoa muda wa wadaawa na wa Mahakama pia.
Kadhalika Hakimu Mfawidhi huyo aliwaomba Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuwakumbusha kila wakati Mawakili wanapokuwa na mashauri Mahakama za Mwanzo kutotumia Sheria na taratibu za Mahakama za juu.
(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni