Jumamosi, 23 Machi 2024

JAJI MKUU AZINDUA KITABU CHA TAFSIRI HADITHI 40 ZA IMAM NNAWAWY

·      Kimesheheni mafundisho, miongozo katika maisha

·      Kinakumbushia haki, amani, upendo

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 23 Machi, 2024 amezindua Kitabu cha Hadithi 40 za Imam Nnawawy, Tafsiri, Ufafanuzi, Sherehe na Maana na kuwahimiza Watanzania kujipatia nakala ili kujiongezea maarifa kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo haki, amani na kumjua Mungu.

Akizungumza kabla ya kuzindua Kitabu hicho katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam ambacho kimeandikwa na Sheikh Issa Othman Issa, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa Kitabu hicho siyo tu kina manufaa makubwa katika eneo la utoaji haki, ambalo amelisimamia kwa miaka mingi, bali pia katika maisha na kazi za kila siku anazozifanya binadamu.

“Kitabu hiki ni msingi wa mambo mengi katika maisha yetu, kazi zetu za kila siku na hadithi hizi zitatusaidia sana sisi tunaofanya kazi za utoaji haki katika kuweka msingi wa kuelewa Sheria. Sheria ambayo inajengwa katika misingi ya imani inakuwa na nguvu zaidi kuliko ambayo inatengenezwa kwa shuruti,” amesema. 

Jaji Mkuu amebainisha kuwa mafunzo yanayotolewa kupitia hadithi 40 zilizoelezewa katika Kitabu hicho, iwapo yatazingatiwa ipasavyo, matukio ya uvunjifu wa sheria na migogoro miongoni mwa wanadamu yangepungua.

Hivyo, anaeleza kuwa alipoupata mwaliko wa hafla hiyo hakusita hata kidogo kuukubali, kwani alielewa vyema mchango ambao Kitabu hicho kitatoa katika kuelimisha, kutoa mwongozo thabiti na rejea mahususi katika kushughulikia masuala mbalimbali ya maisha ya kila siku ya mwanadamu.

“Kitabu hiki kinaimarisha imani miongoni mwa Waislam na wasomaji wengine kwani mtu mchamungu ni aghalabu kumkuta upande mbaya wa Sheria na hivyo kuwa chachu ya kujenga utengamano, kuepusha taharuki, uhasama na dhulma zinazojitokeza,” Mhe. Prof. Juma amesema.

Jaji Mkuu ametolea mfano wa Hadithi ya 32 ambayo inasema, “Usidhuru wala Usidhurike,” inayojenga msingi wa uhuru wa binadamu kufanya chochote ili mradi kitendo chake kisiwe na madhara kwa wengine.

“Hadithi hii imeweka msingi madhubuti wa maisha mazuri kwa kila mmoja kama atazingatia kwa kuishi huku akijiepusha na kudhuru wengine na wakati huo huo akihakikisha kuwa yeye mwenyewe pia hadhuriwi,” amesema.

Jaji Mkuu pia alieleza mafundisho kutoka kwenye hadithi ya 24 kuwa Mwenyezi Mungu, yeye mwenyewe, anatuhakikishia kuwa hafanyi dhulma lakini pia ameifanya dhulma kuwa ni katika mambo ya haramu na anatutaka sisi waja wake tusidhulumiane, kama anavyosema, “Enyi waja wangu, mimi nimejiharamishia dhulma kwangu na nikaifanya dhulma kuwa ni haramu, basi msidhulumiane.”

Mhe. Prof. Juma akasisitiza kuwa Kitabu hicho kitatoa mchango mkubwa katika kutoa elimu na muongozo thabiti kwa waumini wa Dini ya Kiislam, Walimu wa Dini, Mashekh na wasomaji wengine wenye kupenda kuijua Dini hiyo.

Hafla ya uzinduzi wa Kitabu hicho imehudhuriwa na Viongozi kadhaa wa Mahakama ya Tanzania, akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Amour Khamis na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kifungu Kariho. Alikuwepo pia Jaji Kiongozi Mstaafu, Mhe. Amir Manento.

Viongozi wengine ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali na wengine ambao wamempomgeza Sheikh Issa kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuandika Kitabu hicho.

Mhe. Nnauye alienda mbali zaidi kwa kuomba Kitabu hicho kuwekwa katika mfumo wa sauti ili kuwawezesha watu wengi zaidi kusikiliza wakati wakiwa na shughuli zingine. “Nadhani wakati umefika, pamoja na kuweka katika maandishi tuweke pia kwenye sauti ili watu wengi zaidi waweze kujifunza na kupata huu ufahamu na kutakuwa tumewasaidia sana,” amesema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kitabu cha Hadithi 40 za Imam Nnawawy leo tarehe 23 Machi, 2024.  Wengine wanaosaidiana naye ni Mwandishi wa Kitabu hicho, Sheikh Issa Othman Issa (kushoto) na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad Omar. Picha chini, Viongozi hao wakionyesha Kitabu hicho baada ya kuzinduliwa.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza kabla ya kuzindua Kitabu hicho.


Sehemu ya wageni waalikwa (juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) wakati wa ufunguzi huo.


Sehemu nyingine ya wageni waalikwa (juu na mbili chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) wakati wa ufunguzi huo.




Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Masheikh mbalimbali baada ya ufunguzi wa Kitabu hicho.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya Viongozi na Masheikh mbalimbali (juu na chini)baada ya ufunguzi huo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni